Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Umoja wa Afrika ulianza kunako mwaka 2000. Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Umoja wa Afrika ulianza kunako mwaka 2000.  

Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya Vatican na Umoja wa Afrika!

Katika mazungumzo yao, Askofu mkuu Udaigwe, amewasilisha salam, matashi mema na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV. Vatican na Umoja wa Afrika wanataka kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kusimama kidete kulinda na kudumisha: Utu, heshima, haki msingi za binadamu, amani pamoja na kujielekeza katika malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya. Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Umoja wa Afrika ulianza kunako mwaka 2000.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Brian Ngozi Udaigwe, hivi karibuni amewasilisha hati za utambulisho wake kama Balozi wa Vatican kwenye Umoja wa Afrika kwa Mheshimiwa Mahmoud Ali Youssouf, Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika, kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia. Katika mazungumzo yao, Askofu mkuu Udaigwe, amewasilisha salam, matashi mema na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV. Vatican na Umoja wa Afrika wanataka kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kusimama kidete kulinda na kudumisha: Utu, heshima, haki msingi za binadamu, amani pamoja na kujielekeza katika malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya. Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Umoja wa Afrika ulianza kunako mwaka 2000. Mheshimiwa Mahmoud Ali Youssouf amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa jitihada zake nyingi zinazolenga kuleta haki na amani sehemu mbalimbali za dunia. Kanisa Barani Afrika linataka kuendelea kuwa ni Sakramenti ya Wokovu, kwa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa misingi ya: haki, amani, maridhiano na ushirikiano wa kweli. Kwani maendeleo fungamani ya binadamu yanagusa mahitaji yake msingi kama ushuhuda wa haki katika maisha ya watu wa Mungu.

Askofu Mkuu Brian Udaigwe, Mwakilishi wa Vatican Umoja wa Afrika
Askofu Mkuu Brian Udaigwe, Mwakilishi wa Vatican Umoja wa Afrika

Falsafa, sera na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji za Kanisa Barani Afrika zinapania kujenga daraja la dhana ya amani na mshikamano wa dhati, ili kukidhi mahitaji msingi ya binadamu; kwa kukazia: haki, amani ya kudumu na ushirikiano wa kweli. Haki ya kweli inafumbatwa katika mshikamano unaothamini tunu msingi, utu na heshima ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Kwa hakika Kanisa Barani Afrika limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika sekta ya: Elimu, Afya sanjari na Huduma za kijamii, pamoja na kuragibisha umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kuendelea kuishi kwa: amani, umoja na maridhiano.

Watu wa Mungu Nchini Ethiopia
Watu wa Mungu Nchini Ethiopia   (© ETHIOPIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Kanisa Katoliki nchini Ethiopia limempokea kwa furaha na shangwe kubwa Askofu mkuu Brian Ngozi Udaigwe kama Balozi mpya wa Vatican nchini Ethiopia, kufuatia uteuzi uliofanywa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Aprili 2025. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Brian Ngozi Udaigwe, amewahi kuwa Balozi wa Vatican nchini Sri Lanka. Askofu mkuu Udaigwe alipokelewa rasmi hivi karibuni alipowasili mjini Addis Ababa kupitia Shirika la Ndege la Ethiopia, na baadaye katika Ubalozi wa Vatican, ambako watu wa Mungu nchini humo walikusanyika ili kumkaribisha na kuonesha furaha yao kwa ujio wake. Askofu mkuu Udaigwe ni mzaliwa wa Jimbo Katoliki la Orlu nchini Nigeria, akiwa na uzoefu mkubwa katika huduma ya kidiplomasia ya Vatican kwa zaidi ya miongo mitatu. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadri tarehe 2 Mei 1992, na baadaye aliendelea na masomo katika Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa “Pontificia Accademia Ecclesiastica, PAE.” Tarehe Mosi Julai 1994 akaanza huduma ya diplomasia ya Kanisa mjini Vatican na kubahatika kutumwa na kuhudumia: Zimbabwe, Pwani ya Pembe, Haiti, Bulgaria, Thailand na Uingereza.Tarehe 22 Februari 2013 akateuliwa na Hayati Papa Benedikto XVI kuwa Balozi wa Vatican nchini Benin na Togo na kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu tarehe 27 Aprili 2013 na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican wakati ule. Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Juni 2020 akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Sri Lanka hadi alipohamishiwa nchini Ethiopia.

Viongozi wakuu wa SECAM na Papa Leo XIV
Viongozi wakuu wa SECAM na Papa Leo XIV   (ANSA)

Wakati wa sherehe ya mapokezi, Monsinyo Massimo Catterin, Katibu wa Ubalozi wa Vatican nchini Ethiopia alitoa pongezi za dhati kwa Askofu mkuu Udaigwe na kumkaribisha nchini Ethiopia. Pia alitaja uteuzi huo kuwa maalum kwa sababu Papa Francisko, aliyefariki hivi karibuni, ndiye aliyemteua Askofu mkuu siku tisa kabla ya kifo chake ishara ya upendo wa kudumu wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa nchini Ethiopia. Monsinyori Catterin alimhakikishia Askofu mkuu umoja na ushirikiano kamili kutoka kwa timu ya Ubalozi wa Vatican nchini Ethiopia akisema kwa maneno haya: “Hakika wewe ni baba yetu, sisi ni wanao ambao tuko tayari kusikiliza na kutiwa moyo na ujuzi pamoja na uzoefu wako.” Katika hotuba yake, Askofu mkuu Udaigwe alieleza shukrani zake za dhati kwa umuhimu wa kihistoria na kiroho wa Ethiopia, akisisitiza nafasi yake kama kitovu cha Mataifa mengi Barani Afrika. Alilisifu Kanisa Katoliki nchini Ethiopia kwa juhudi zake na kusisitiza umuhimu wa kusaidiana na kushirikiana “kwa ajili ya utukufu wa Mungu.” Katika maelezo yake, aligusia upekee wa uteuzi wake, akieleza kuwa mchakato ulianza chini ya uongozi wa hayati Papa Francisko na kukamilishwa na Baba Mtakatifu Leo XIV. Alisema kuwa hilo linafanya utume wake nchini Ethiopia kuwa safari ya kipekee na yenye maana katika huduma kwa Kanisa. Kwa uteuzi wake huu mpya, Askofu mkuu Udaigwe analeta uzoefu mkubwa wa kidiplomasia na kichungaji katika eneo la Pembe ya Afrika, akiendeleza wajibu wake wa kumwakilisha Baba Mtakatifu Leo XIV na kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na Kanisa la Ethiopia.

Umoja wa Afrika
14 Februari 2026, 14:15