Siku ya Watawa Ulimwenguni ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 na kwa Mwaka 2026, Kanisa linaadhimisha Siku ya 30 ya Watawa Ulimwenguni Siku ya Watawa Ulimwenguni ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 na kwa Mwaka 2026, Kanisa linaadhimisha Siku ya 30 ya Watawa Ulimwenguni   (Vatican Media)

Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni: Siku ya 30 ya Watawa Ulimwenguni 2026

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, lengo kuu la Siku ya Watawa Ulimwenguni ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwepo wa watawa ambao wameamua kumfuasa Kristo Yesu kwa kuishi mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Ni fursa kwa watawa kurudia tena nadhiri zao, ili kupyaisha maisha na utume wao mintarafu karama za mashirika yao ambayo ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa. Watawa ni mashuhuda wa uwepo wa Kanisa Ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika Waraka wake kwa watawa kwa Mwaka 2026 linasema, katika ziara zake za kitume sehemu mbalimbali za dunia, limebahatika kugusa na kuruhusu maisha ya watu hawa yawaguse; wamekutana na nyuso za watawa wengi wanaoitwa kushiriki hali ngumu na tete katika mazingira yaliyokumbwa na migogoro, ukosefu: haki, amani na wa utulivu wa kijamii na kisiasa; umaskini wa hali ya juu, hali kutengwa, uhamiaji wa shuruti, kinzani za kidini; vurugu, mipasuko na mivutano ambayo wakati mwingine hujaribu uhuru wa watu na kutikisa imani yao wenyewe. Matukio haya yote yanadhihirisha nguvu ya mwelekeo wa kinabii wa maisha ya Kitawa kama "uwepo unaodumu": pamoja na watu waliojeruhiwa, watu binafsi, na mahali ambapo Injili mara nyingi humwilishwa katika hali dhaifu na ya majaribu. Ni katika muktadha wa hali tete ya maisha; ukosefu wa uhakika wa usalama; upweke hasi; mifumo mipya ya umaskini na hali ya kutojali inapojionesha kwa wazi; ukosefu wa haki, amani na usawa; uhamiaji pamoja na kinzani na migogoro ya kijamii ni mambo ambayo kwa watawa wengi yamekuwa ni sehemu ya utambulisho na vinasaba vya maisha na utume wao, kielelezo kwamba, kwa hakika, Mwenyezi Mungu hawezi kuwatelekeza watu wake. Watawa wameendelea kuwepo na kustahimili katika mchakato wa kutafuta: haki, amani na maridhiano; kwa kuendelea kujikita katika utamaduni wa kusikiliza, sala pamoja na kusimama kidete: kulinda, kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Na kwa njia hii, Mama Kanisa ameendelea kuonesha uwepo wake wa kinabii katika ulimwengu mamboleo kama sehemu ya mchakato wa kutafuta na kudumisha amani; na kama mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili. Hawa ni watawa wanaoamua kubaki huku wakisimika maisha yao katika: upendo na bila kunyamaza.

Watawa ni mashuhuda  na sauti ya kinabii ulimwenguni
Watawa ni mashuhuda na sauti ya kinabii ulimwenguni   (© fra Mate Šakić)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema amani ni mchakato wenye madai yanayosimikwa katika uhalisia wa kila siku; mchakato unaohitaji majadiliano katika ukweli na uwazi; Uvumilivu; toba na wongofu wa ndani; kwa watu kukutana na kuzungumza, ili kuweza kusikilizana na hivyo kuwa na uwajibikaji wa pamoja. Hii ni sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika upendo unaowajali wote kama ndugu wamoja. Ni mchakato unaowahimiza watawa kutangaza na kushuhudia ukweli, kama vyombo na wajenzi wa amani. Watawa waendelee kuwa ni mahujaji wa matumaini katika njia ya amani, ili waweze kuwa kweli manabii wa uwepo na mbegu ya amani Kanisa na katika Ulimwengu mamboleo. Siku ya Watawa Ulimwenguni ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 na kwa Mwaka 2026, Kanisa linaadhimisha Siku ya 30 ya Watawa Ulimwenguni kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Watawa Katika Mchakato wa Kueneza Maelewano na Amani.” Lengo la Maadhimisho haya katika maisha na utume wa Kanisa ni kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa huduma inayotolewa na watawa sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni Siku ambayo watawa hushiriki katika matukio mbalimbali ya Kiliturujia, kama alama ya shukrani. Ni muda muafaka wa kutafakari juu ya maisha na wito wa kitawa; kukuza mang’amuzi na uelewa zaidi ndani ya Kanisa! Watawa ni mashuhuda na vyombo vya neema ya Mungu inayomwilishwa katika maisha ya kidugu katika Jumuiya, huku wakishuhudia furaha ya Injili na upendo wa kidugu.

Watawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu.
Watawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu.   (@Vatican Media)

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, lengo kuu la Siku ya Watawa Ulimwenguni ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwepo wa watawa ambao wameamua kumfuasa Kristo Yesu kwa kuishi mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Ni fursa kwa watawa kurudia tena nadhiri zao, ili kupyaisha maisha na utume wao mintarafu karama za mashirika yao ambayo ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa. Hii ni nafasi ya kuragibisha maisha na utume wa watawa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima sanjari na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao ili kukoleza utakatifu wa maisha. Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari ni changamoto na mwaliko kwa Wakristo wote kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mwenyezi Mungu sanjari na kushuhudia upendo wa huduma kwa jirani. Hii ni sikukuu ya mwanga na watu kukutana na Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. Kimsingi Kristo Yesu anakutana na watu wake, wanaowakilishwa na Mzee Simeoni na Nabii Ana, Binti ya Fanueli. Dhamana ya Roho Mtakatifu katika maisha ya kitawa; Umuhimu wa kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wa kitawa ili kuupyaisha, tayari kukutana na Kristo Yesu katika mambo msingi ya maisha ya kitawa. Mzee Simeoni na Nabii Ana, Binti ya Fanueli waliongozwa na Roho Mtakatifu, aliyeamsha ile ari na kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu. Roho Mtakatifu akawaongoza hadi Hekaluni wakakutana na kumwona Masiha wa Bwana, aliyejifunua kwao kama Mtoto mdogo na maskini, mwaliko wa kumtambua na kumpokea Mwenyezi Mungu katika hali ya kawaida na kwenye mambo madogo madogo; yanayoonesha ukuu na utakatifu wa maisha kama ilivyo hata katika Fumbo la Msalaba. Waamini wanahimizwa kumsikiliza Roho Mtakatifu anayezungumza kutoka katika undani wa maisha yao.

Watawa ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili katika maisha na utume wao
Watawa ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili katika maisha na utume wao   (@Vatican Media)

Watawa wanaweza kuingiwa na kishawishi cha kutaka kutafuta nafasi, ili waonekane pamoja na kuwa na idadi kubwa zaidi. Roho Mtakatifu anawataka watawa kujenga na kudumisha uaminifu, kwa kuendelea kujikita katika maisha ya sala ili kunogesha matumaini yaliyomo ndani mwao. Wajiulize swali msingi ni jambo gani linalowasukuma kutoka katika undani wa maisha yao, kwa sababu hata katika matendo mema, wakati mwingine yanageuka kuwa ni “kichaka cha kuficha ubinafsi na uchoyo na wakati mwingine watawa kutaka kujimwambafai.” Licha ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na watawa, wakati mwingine, zinafanywa kwa mazoea bila ya kuwa na mguso kutoka ndani ya maisha. Hii ni changamoto ya kupyaisha maisha na utume wa kitawa ndani ya Kanisa kwa kuangalia mambo msingi yanayowasukuma kutoka katika undani wa maisha yao. Imani inachipuka kwa kukutana na Kristo Yesu, anayependa kuwaangalia waja wake kwa jicho la huruma na upendo, mwaliko kwa watawa kuwa na mwelekeo mpya wa kujiangalia na kuangalia mambo ya ulimwengu. Watawa wawe na uthubutu wa kuangalia matukio ya maisha ndani na nje kwa kuwa na jicho la busara; kwa kuzama na kugusa udhaifu na mapungufu ya binadamu, ili kutambua uwepo angavu na endelevu wa Mungu katika maisha yao. Watawa wamwombe Roho Mtakatifu ili awawezeshe kuwa na hekima na busara ya kuangalia, kupanga na kupima vyema, ili kutambua ukweli wa mambo, daima wakiwa na furaha katika maisha. Watawa wajenge utamaduni wa kuwatembelea wazee na kuzungumza nao, ili hatimaye, waweze kuwa na mwono uliopyaishwa zaidi. Kuna hatari ya watawa kujirudisha nyuma kwa sababu ya wasiwasi, woga na hofu ya usalama, kwa kudhani kwamba, wanalinda imani na karama ya mwanzilishi wa Shirika. Watawa wawe na macho ya matumaini, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Watawa waendelee kuwa ni vyombo na mahujaji wa matumaini
Watawa waendelee kuwa ni vyombo na mahujaji wa matumaini   (@Vatican Media)

Mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa watawa ndiyo dawa mchunguti itakayosaidia kuongeza miito, vinginevyo watatangatanga kutafuta walelewa kutoka sehemu mbalimbali za dunia bila mafanikio. Watawa katika sala na kuabudu Ekaristi Takatifu, wathubutu kumwomba Mungu neema ya kuwa na mwono mpya katika maisha. Huu ni mwaliko kwa watawa kumpokea Kristo Yesu kama kiini cha imani ya Kanisa na Bwana wa maisha yao, ili kugundua maajabu ya Mungu yaliyofichwa katika maisha. Watawa wakijifungia katika uchoyo na ubinafsi wao, hawataweza kupyaisha mwono wa maisha yao na matokeo yake watajikuta wakielemewa na machungu. Kwa mara nyingine tena, watawa wanapaswa kuachana na tabia ya “kupika majungu” kwani ni hatari kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni ni muda muafaka wa kupyaisha maisha na utume wa Mashirika ya kitawa na yale ya kazi za kitume, daima wakiwa na furaha. Leo hii kuna idadi kubwa ya watawa wanaoamua kuacha maisha ya kitawa na kipadre na kurejea uraiani. Kumbe, maadhimisho ya Siku ya Watawa Uimwenguni ni nafasi ya kukutana na kushuhudia uaminifu wa Mungu kwa njia ya udumifu wa mifumo mbalimbali ya maisha kitawa na kazi za kitume. Lengo ni kumwilisha tasaufi na ushirika wa watawa katika maisha ya Kanisa mahalia, kwani hata wao wanahusika. Hii ni changamoto ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana, ili kufanya hija ya pamoja ya watoto wa Mungu, kwa furaha na moyo mkuu.

Siku ya 30 ya Watawa

 

01 Februari 2026, 15:53