Papa XIV:Neno ni jipya daima linatufunulia siri ya Mungu,halina mwisho
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tunaishi tukizungukwa na maneno mengi, lakini ni mangapi kati yake ni matupu! Wakati mwingine hata tunasikia maneno ya busara, lakini hayagusi hatima yetu ya mwisho. Hata hivyo, Neno la Mungu linakidhi kiu yetu ya maana, ukweli kuhusu maisha yetu. Ni Neno pekee ambalo ni jipya kila wakati: likitufunulia siri ya Mungu, halina mwisho, haliachi kamwe kutoa utajiri wake. Kanisa ni mahali pazuri pa Maandiko Matakatifu ambapo kazi yake inastawi: Kumtangaza Kristo na kufungua mazungumzo na Mungu. Neno linalolisha safari ya imani ya kila mtu, linalosukuma Kanisa hata zaidi ya lenyewe, likirudisha ukweli kwenye maisha ambayo yamezama katika mlio mkubwa wa maneno mengi matupu. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Leo XIV alivyosema katika Katekesi yake mbele ya Waamini na mahujaji 8,000 waliofika kutoka Ulimwenguni kote, Jumatano tarehe 11Februari 2026, katika Ukumbi wa Paulo VI. Kwa mara nyingine tena ni mwendelezo wa tafaka ya Katiba ya Mtaguso II wa Vatican ( Costituzione conciliare Dei Verbum.)
Kanisa ndilo mahalo pazuri pa Maandiko Matakatifu.
Katika kipengele cha tano cha Neno la Mungu katika maisha ya Kanisa, lilisomwa awali neno la Mungu kutoka Barua ya Mtakatifu Paulo kwa wathesalonike: “ Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini 1 Ts 2,13.” Baba Mtakatifu alianza kusema: “Katika katekesi ya leo, tutazingatia uhusiano mkubwa na muhimu kati ya Neno la Mungu na Kanisa, uhusiano uliooneshwa katika Katiba ya Dei Verbum, katika sura yake ya sita. Kanisa ndilo mahali pazuri pa Maandiko Matakatifu. Chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, Biblia ilizaliwa kutoka kwa watu wa Mungu na imekusudiwa kwa ajili ya watu wa Mungu. Kwa kusema, ina makazi yake katika jumuiya ya Kikristo: katika maisha na imani ya Kanisa, na hupata nafasi ya kufichua maana yake na kudhihirisha nguvu yake.
Kanisa haliachi kamwe kutafakari thamani ya maandiko matakatifu
Mtaguso wa II wa Vatican unakumbuka kwamba "Kanisa limekuwa likiheshimu Maandiko Matakatifu kila wakati linapoheshimu Mwili wa Bwana wenyewe, bila kushindwa kamwe, hasa katika liturujia Takatifu, ili kupata chakula kutoka katika mkate wa uzima katika meza ya Neno la Mungu na Mwili wa Kristo na kuwapa waamini." Zaidi ya hayo, "pamoja na Mapokeo Matakatifu, Kanisa limekuwa likiyazingatia na linaendelea kuyazingatia kama kanuni kuu ya imani yake" (Dei Verbum, 21). Kanisa haliachi kamwe kutafakari thamani ya Maandiko Matakatifu. Baada ya Mtaguso, wakati muhimu sana katika suala hili ulikuwa Mkutano Mkuu wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu mada "Neno la Mungu katika Maisha na Utume wa Kanisa," mnamo Oktoba 2008. Papa Benedikto XVI alikusanya matunda ya tafakari hii katika Wosia wa Baada ya Sinodi: "Verbum Domini" (Septemba 30, 2010), ambapo anasema:"Uhusiano wa ndani kati ya Neno na imani unaangazia kwamba hemenetiki halisi ya Biblia inaweza kupatikana tu katika imani ya Kanisa, ambayo ina dhana yake katika 'ndiyo' ya Maria. [...] Mahali pa asili pa tafsiri ya maandiko ni maisha ya Kanisa" (na. 29).
Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo
Katika jumuiya ya Kanisa, Maandiko Matakatifu hupata muktadha wa kutekeleza kazi yake maalum na kufikia kusudi lake: kumfanya Kristo ajulikane na kuwa wazi kwa mazungumzo na Mungu. "Kutojua Maandiko Matakatifu," kiukweli, "ni kutokumjua Kristo." Usemi huu maarufu wa Mtakatifu Yeronimo unatukumbusha kusudi kuu la kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu: kumjua Kristo na, kupitia Yeye, kuingia katika uhusiano na Mungu, uhusiano ambao unaweza kueleweka kama mazungumzo. Na Katiba ya Dei Verbum ilitupatia Ufunuo hasa kama mazungumzo, ambapo Mungu huzungumza na wanadamu kama marafiki (rej. DV, 2). Hii hutokea tunaposoma Biblia katika mtazamo wa ndani wa maombi: kisha Mungu huja kukutana nasi na kuingia katika mazungumzo nasi.
Waamini wameitwa kunywa koka chanzo cha Ekaristi na Sakramenti nyingine
Maandiko Matakatifu, yaliyokabidhiwa Kanisa na kulindwa na kuelezwa nalo, yana jukumu kubwa: kiukweli, kwa ufanisi na nguvu zake, hutoa msaada na nguvu kwa jumuiya ya Kikristo. Waamini wote wameitwa kunywa kutoka chanzo hiki, kwanza kabisa katika maadhimisho ya Ekaristi na Sakramenti zingine. Kupenda na kufahamiana na Maandiko Matakatifu lazima kuwaongoza wale wanaotekeleza huduma ya Neno: maaskofu, makuhani, mashemasi, na makatekista. Kazi ya wafafanuzi na wale wanaofanya masomo ya Biblia ni muhimu sana; na Maandiko ni muhimu kwa Taalimungu, ambayo hupata msingi na roho yake katika Neno la Mungu. Kile ambacho Kanisa linatamani kwa dhati ni kwamba Neno la Mungu liweze kumfikia kila mshiriki na kulisha safari yao ya imani. Lakini Neno la Mungu pia hulisukuma Kanisa zaidi ya lenyewe, likiendelea kulifungua kwa utume kwa wote.
Tunaishi tukizungukwa na maneno mengi lakini je ni mangapi matupu?
Hakika, tunaishi tukizungukwa na maneno mengi, lakini ni mangapi kati yake ni matupu! Wakati mwingine hata tunasikia maneno ya busara, lakini hayagusi hatima yetu ya mwisho. Hata hivyo, Neno la Mungu linakidhi kiu yetu ya maana, ukweli kuhusu maisha yetu. Ni Neno pekee ambalo ni jipya kila wakati: likitufunulia siri ya Mungu, halina mwisho, haliachi kamwe kutoa utajiri wake. Baba Mtakatifu aliendelea kusema kuwa “kwa kuishi ndani ya Kanisa, tunajifunza kwamba Maandiko Matakatifu yanahusiana kabisa na Yesu Kristo, na tunaona kwamba hii ndiyo sababu kubwa ya thamani na nguvu yake. Kristo ndiye Neno lililo hai la Baba, Neno la Mungu aliyefanyika mwili. Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu alisema kuwa “ Maandiko yote yanatangaza Utu wake na uwepo wake wa kuokoa, kwa kila mmoja wetu na kwa wanadamu wote. Kwa hivyo, hebu tufungue mioyo na akili zetu ili kukaribisha zawadi hii, katika shule ya Maria Mama wa Kanisa.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here.
