Papa Leo XIV: Wasaidizi wa Karibu wa Papa: Imani Thabiti Na Ushuhuda Amini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni heshima kubwa inayokita mizizi yake katika imani thabiti na ushuhuda wa maisha ya kiroho yanayopata chapa yake katika Ibada kwa Kanisa la Kristo Yesu na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni sehemu ya salamu na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV alipokutana na kuzungumza na wasaidizi wake wa karibu; Dominika tarehe Mosi Februari 2026 na kwamba, ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwatia shime katika maisha na utume wao; uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro; unaomsaidia na kumwezesha kutekeleza dhamana na majukumu yake ya: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Hawa ni watu wanaomtembelea Baba Mtakatifu mjini Vatican, wakati wa Katekesi zake na anapokutana na makundi ya watu wa Mungu.
Hii ni huduma inayoweza kuwekwa kwa muhtasari katika maneno makuu matatu: Uwepo, Ukarimu na Kusalimia mambo muhimu sana yanayomwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kukutana na kusalimiana na makundi mbalimbali ya watu wa Mungu. Hii ni huduma ya kale inayokita mizizi yake katika sanaa ya uangalifu na unyenyekevu wa moyo; Ukarimu na Salamu kwa watu mbalimbali. Hata kama ni Mahujaji, Wakuu wa nchi, Viongozi wa Kanisa, wote hawa wanapaswa kuonjesha ukarimu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ushuhuda wa Protokali ya Kipapa inayoshuhudiwa kwa vitendo vyao.
Huu ni mwaliko kwa wasaidizi wa karibu wa Baba Mtakatifu Leo XIV kuhakikisha kwamba, maisha yao yanakuwa ni ushuhuda wa imani thabiti, tasaufi ya maisha inayopata chapa yake katika Ibada kwa Kanisa la Kristo Yesu na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Leo XIV amewasihi wasaidizi wake wa karibu kuhakikisha kwamba, matendo yao na mtazamo wao wa kila siku uwe ni kioo kinachoangaza hali hii. Anawataka waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma mbalimbali wanazoshiriki, kila mmoja kadiri ya nafasi yake na mwishowe, akawapatia baraka zake za kitume, wao wenyewe, familia pamoja na wapendwa wao.
