Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 6 Februari 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 6 Februari 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha.   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Umuhimu wa Malezi na Majiundo ya Kikristo Ndani ya Kanisa

Papa Leo XIV, Ijumaa tarehe 6 Februari 2026 amekutana na wajumbe Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha na mekazia: Malezi ya waamini walei katika maisha ya Kikristo na uzoefu wa maadhimisho ya mikutano ya Kimataifa, matukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini hawana budi kufundwa, ili wafanane na Yesu, hata aumbike ndani yao, kwani Yesu ana uwezo wa kuwafunda katika hali ya mwili; Rej. Rum 7:5 kwani yuko ndani mwao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko kunako 15 Agosti 2016 katika barua yake binafsi, “Motu Proprio” “Sedula mater” alianzisha Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kama sehemu ya mchakato wa Sekretarieti kuu ya Vatican kusoma alama za nyakati na kujibu kwa ufasaha na weledi mkubwa changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika maisha ya ndoa na familia, vijana pamoja na vyama na mashirika ya kitume. Baba Mtakatifu Francisko katika barua hii anasema, Mama Kanisa, mwingi wa huruma na mapendo, katika historia ya maisha na utume wake, amekuwa karibu sana kwa waamini walei, familia pamoja na kuhimiza Injili ya uhai, kama kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa walimwengu. Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa waamini walei katika maisha na utume wake, kwani hawa wamepewa changamoto ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Baraza linawahamasisha waamini walei kuhakikisha kwamba, wanalitegemeza Kanisa kwa karama na mapaji yao sanjari na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei watambue: dhamana, wajibu na haki zao msingi ndani ya Kanisa. Vyama na mashirika ya kitume ni muhimu sana katika kufunda, kulea, kukuza na kudumisha imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahamasisha waamini walei kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza liko mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha utume wa vijana wa kizazi kipya, kwa kutambua kwamba, vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa kwa leo na kwa siku za usoni.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha
Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha   (@VATICAN MEDIA)

Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Tatu wa Baraza hili la Kipapa umenogeshwa na kauli mbiu: “Viungo vyote lazima viundwe ili kufanana na Kristo Yesu, hata yeye aumbike ndani yao” (Gal 4:19) Wajumbe wamekazia kuhusu: Malezi ya waamini walei katika maisha ya Kikristo na uzoefu wa maadhimisho ya mikutano ya Kimataifa, matukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mikutano inayohitaji maandalizi makini, ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, ushirikiano na watu na taasisi katika ngazi mbalimbali ambazo kimsingi ni amana na utajiri mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wajumbe wamejadili pamoja na mambo mengine: Kuhusu utume wa waamini walei katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Umuhimu wa Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo; Mwongozo wa Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni kwenye Makanisa Mahalia, Hija za Kitume za Maaskofu Mahalia mjini Vatican sanjari na umuhimu wa malezi na majiundo ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu: Katekisimu, Maisha ya Kisakramenti, Liturujia, Maisha ya Sala, Neno la Mungu na Huduma ya Upendo mintarafu malezi na majiundo ya Kiimani. Hii ni changamoto kwa Makanisa mahalia kuhakikisha kwamba, imani inapandikizwa, inapaliliwa na kudumishwa. Maaskofu mahalia waweke sera na mbinu mkakati wa malezi na makuzi ya imani kwa kukazia mambo msingi katika imani ya Kikristo.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha: 15 Agosti 2016
Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha: 15 Agosti 2016   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 6 Februari 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Katika hotuba yake amekazia: Malezi ya waamini walei katika maisha ya Kikristo na uzoefu wa maadhimisho ya mikutano ya Kimataifa, matukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini hawana budi kufundwa, ili wafanane na Kristo Yesu, hata aumbike ndani yao, kwani Yesu ana uwezo wa kuwafunda katika hali ya mwili; Rej. Rum 7:5 kwani Kristo Yesu yuko ndani mwao; Rej. 2Kor 13:5; Gal 2:20. Majiundo makini ya waamini ndani ya Kristo Yesu ni kati ya tema ambazo Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa alizipatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake huku akisema: “Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.” 1Kor 4:15. Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia dhana ya Mwalimu, kama mlezi anayejisadaka katika mchakato wa kufundisha, kulea na kudumisha mang’amuzi ya maisha ya kiroho ambayo ni muhimu sana kuliko ile dhana ya “Baba” anayezalisha watu katika imani. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha lina dhamana na wajibu mkubwa wa kufundisha: Mafundisho tanzu ya Kanisa; Kanuni maadili na utu wema, lakini zaidi ya haya, wanapaswa kuwashirikisha wengine kile ambacho wao wanakiishi kwa ukarimu, upendo wa kweli pamoja na kuwajibika, kiasi hata cha kuteseka kwa ajili ya wengine. Wanapaswa kuwajibika bila kujibakiza, kama wazazi na walezi wanavyojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wao.

Papa Leo XIV: Umuhimu wa Malezi na Makuzi ndani ya Kanisa
Papa Leo XIV: Umuhimu wa Malezi na Makuzi ndani ya Kanisa   (@VATICAN MEDIA)

Malezi haya hayana budi kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika unaofumbatwa katika upendo wa Kikristo kwa kutambua kwamba, Mama Kanisa ndiye chemchemi ya imani kwa waamini na wala si Padre au Katekista na hivyo Taifa zima la Mungu lina wajibu wa kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Uinjilishaji ni kazi na dhamana ya Kanisa na ni wakala wa uinjilishaji. Kanisa ni Fumbo linalokita mizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, amana na wajibu wa Taifa lote la Mungu kutangaza na kushuhudia Injili, na hasa kwa vijana wa kizazi kipya. Taifa la Mungu lioneshe ule utashi wa kutoa na kuchangia Injili ya upendo, chemchemi ya furaha inayokita mizizi yake katika shughuli nzima ya malezi na majiundo ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Kristo Yesu baada ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu aliwatuma Mitume wake akisema: “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt 28:19-20.

Malezi, makuzi na majiundi ya walei ni muhimu sana
Malezi, makuzi na majiundi ya walei ni muhimu sana   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu anasema, huu ni muhtasari wa maisha na utume wa mlezi unaofumbatwa katika ushuhuda wa medani mbalimbali za maisha ya Kikristo. Wajibu huu unakwenda sanjari na waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika. Ni wajibu wa Jumuiya za waamini kuhakikisha kwamba, zinakuwa makini ili kusitokee tena nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo sanjari na kuendelea kuwasindikiza na kuwasaidia waathirika. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Sanaa ya Malezi na Majiundo ya Kikristo inakita mizizi yake katika fadhila ya: Uvumilivu, Kusikiliza, Kusindikiza na Kuhakiki, katika ngazi ya mtu binafsi, Jumuiya na wale walioishi tunu hizi msingi, ili kuweza kujifunza na kuiga mifano bora ya maisha yao. Mama Kanisa anayo mifano hai ya watakatifu waliojisadaka kwa ajili malezi na makuzi ya Kikristo. Hawa ni: Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Mtakatifu Filipo Neri, Mtakatifu Joseph Calasanzio, Mtakatifu Gaspari del Bufalo pamoja na Mtakatifu Yohane Leonardi na kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Augustino, baada ya kuteuliwa kuwa Askofu aliandika Katelisimu yake “De catechizandis rudibus, ambayo mafundisho yake bado ni hai hata leo hii. Baba MtakatifuLeo XIV amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Kwa dhamana na mchango wao kwa Baraza, Jinsi ambavyo wanapambana na changamoto mamboleo na kamwe wasikate tamaa, hata kile kidogo wanachochangia katika imani kama “mbegu ya haradali” Kristo Bwana atawapatia msaada kwa wakati muafaka. Wamwangalie Bikira Maria aliyewajalia Kristo Yesu na kuwashirikisha upendo unaowazalisha waamini ndani ya Kanisa wanaounda Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.

Malezi na Makuzi ya Kikristo
06 Februari 2026, 16:25