2026.02.05Kamati ya Uongozi ya Shirika Kutoka migoror hadi Utunzji:Matendo ya kikatoliki kwa ajili ya  Watoto. 2026.02.05Kamati ya Uongozi ya Shirika Kutoka migoror hadi Utunzji:Matendo ya kikatoliki kwa ajili ya Watoto.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV:Tujitahidi kulinda watoto na kuwa na maono makali ya maisha!

Papa Leo XIV katika hotuba yake kwa Kamati ya Shirika la"Kutoka Mgogoro hadi Utunzaji:Matendo ya Kikatoliki kwa Watoto,"aliwaalika kuhoji kama ahadi za Kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu imetengwa.Papa alisema Maendeleo hayajapatikana katika mkasa wa watoto wasio na matunzo na haki.Alikumbusha matashi ya watoto,yaliyotolewa katika barua ya mkutano kuhusu haki zao,ulioitishwa na Papa Francisko,Vatican 2025:"kusafisha ulimwengu kutokana na mambo mabaya,kuupaka rangi ya urafiki na heshima.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo  XIV, Alhamisi tarehe 5 Februari 2026, alikutana mjini Vatican na Kamati ya Shirika la "Kutoka Mgogoro hadi Utunzaji: Matendo ya Kikatoliki kwa Watoto." Akianza hotuba yake alisema: "Mnapokusanyika ili kuendeleza ahadi zilizokuwa matunda ya Mkutano wa Kimataifa wa Haki za Watoto, ulioitishwa na mtangulizi wangu, Papa Francisko, wakati kama huu mwaka jana(2025), ninawakaribisha kwa uchangamfu nyote." Kwa kuongeza Papa alisema "Tafadhali muwe na uhakika wa maombi yangu mnapotafuta kutambua mapenzi ya Bwana na kusoma "ishara za nyakati" zinazohusiana na athari za migogoro ya dunia kwa "watoto" wa Mungu. Kiukweli ni mkasa kwamba watoto na vijana wa ulimwengu wetu, wale ambao Yesu alitaka waende kwake, mara nyingi hunyimwa huduma na upatikanaji wa mahitaji ya msingi ya maisha. Vivyo hivyo, mara nyingi huwa na fursa chache za kufikia uwezo wao waliopewa na Mungu."

Mkutano wa Matendo ya kikatoliki kwa Watoto
Mkutano wa Matendo ya kikatoliki kwa Watoto   (@Vatican Media)

Hali ya Watoto leo hii inakosa maendeleo

Kwa masikitiko, Papa anaona “ kwamba hali ya watoto leo haijaboreka katika mwaka uliopita, na pia ni jambo la wasiwasi mkubwa kujifunza kuhusu ukosefu wa maendeleo katika kuwalinda watoto kutokana na hatari. Mtu lazima ajiulize kama ahadi za kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu zimetupiliwa mbali tunapoona katika familia yetu ya kibinadamu duniani kwamba watoto wengi bado wanaishi katika umaskini uliokithiri, wanateswa na kulazimishwa kuhama, bila kusahau kwamba hawana elimu sahihi na wametengwa au kutengwa na familia zao.” Hili linatukumbusha msisitizo mkubwa wa Papa Francisko kuhusu "haki ya mtoto ya kupokea upendo kutoka kwa mama na baba; zote mbili ni muhimu kwa ukuaji kamili na wenye usawa wa mtoto" (Amoris Laetitia, 172).

Tujitahidi kulinda na kuwa na maono makali ya maisha

Tuthibitishe na kutetea "maono ya kina ya maisha kama zawadi ya kuthaminiwa, na ya familia kama mlezi wake anayewajibika," tukizingatia "ni jambo la kusikitisha kwamba rasilimali za umma zinatengwa kukandamiza maisha, badala ya kuwekezwa kusaidia akina mama na familia" (Hotuba kwa Wanachama wa Kikosi cha Kidiplomasia Kilichoidhinishwa na Vatican, 9 Januari 2026). Katika suala hili, Papa alikaribisha kujitolea kwao kutengeneza njia bora za kushughulikia masuala yaliyotolewa katika Mkutano wa Haki za Watoto. Wanapotekeleza kazi hiyo, Papa alipenda kutaja mambo mawili muhimu. Kwanza, wao wanazungumza kwa niaba ya wale ambao hawana sauti. “Hii ni kazi nzuri kweli. Kumbukeni  hilo wakati kishawishi cha kukata tamaa kinapotokea kwa sababu ya mipango iliyoshindwa, ukosefu wa nia kutoka kwa wengine au hisia kwamba hali haiboreki. Acheni mema mnayojua na mnayofanya yawasogeze mbele.”

Mkutano wa Matendo ya kikatoliki kwa ajili ya watoto
Mkutano wa Matendo ya kikatoliki kwa ajili ya watoto   (@Vatican Media)

Kutafuta njia ya kufanya kazi pamoja kwa maelewano

Jambo la pili, Papa Leo alisema linahusu hitaji la kuzingatia mahitaji ya watoto, ambayo yanaweza kupuuzwa kwa urahisi wakati utunzaji unazingatia eneo moja tu la hitaji. Kwa maana hii,” ninatambua kwamba njia mahususi ambayo kila mmoja wenu anashughulikia mahitaji ya watoto inalingana na karama na utaalamu wenu maalum ndani ya miundo ya Kanisa lenu, Mashirika ya Kitawa na mashirika yaliyoongozwa kikatoliki. Hata hivyo, ninawasihi kutafuta njia za kufanya kazi pamoja kwa amani zaidi ili watoto wapate utunzaji ulio sawa, kwa kuzingatia ustawi wao wa kimwili, kisaikolojia na kiroho. Baraza la Kipapa la Kukuza Maendeleo Jumuishi ya Binadamu, pamoja na Taasisi ya  Kipapa cha Maisha, Umoja wa Mama Wakuu wa Mashirika ya Kike na Umoja wa Kimataifa wa Wakuu wa Mashirika ya Kiume ambao unawasindikiza  katika juhudi hii, na ninawahimiza nyote kuandaa hatua madhubuti na mipango ya utekelezaji ili kushughulikia mahitaji ya watoto.”

Papa Francisko anatukumbusha umuhimu wa kusikiliza Watoto

Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kwamba, “Papa Francisko mara nyingi alitukumbusha kuhusu hitaji la kuwasikiliza watoto na alithibitisha kuwa walimu wazuri katika suala hili. Kwa hivyo, Papa alihitimisha kwa kunukuu katika barua ambayo watoto walimkabidhi katika Mkutano Mkuu wa mwaka jana 2025 kuwa:"Pamoja nanyi, tunataka kusafisha ulimwengu kutokana na mambo mabaya, kuupaka rangi ya urafiki na heshima, na kuwasaidia kujenga mustakabali mzuri kwa kila mtu!" Akimwomba Maria, Mama wa Kanisa, anaomba  kwamba Mungu awabariki wote na awape nguvu na ujasiri wanapowasaidia watoto katika kutimiza ndoto hizo.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here

 

05 Februari 2026, 17:12