Papa Leo XIV: Kutokujua Maandiko Matakatifu Ni Kutomfahamu Kristo Yesu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 5 Februari, anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Agatha, Bikira na Shahidi aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Februari 2026 amesema, Jina Agatha maana yake ni “Wema” na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wema mkuu (Summum bonum), na lengo la mwisho la maisha ya binadamu (Finis ultimus). Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitahidi kuwa watu wema, yaani “Vyombo na Mashuhuda wa Huruma na Upendo wa Baba wa Milele” anayewakirimia waja wake mema mengi na hivyo kuwaalika kushiriki katika furaha yake isiyokuwa na mwisho!
Hati ya Kusikiliza kwa Uchaji Ufunuo wa Neno la Mungu “Dei verbum” inagusia kwa undani kuhusu: Ufunuo wenyewe; Urithishaji wa Ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na Ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale, Agano Jipya; pamoja na Maandiko Matakatifu Katika Maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Ufunuo wa Baba wa milele, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na kujikita katika maisha ya sala!
Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kuomba mwanga wa Roho Mtakatifu wanaposoma Maandiko Matakatifu, ili waweze kuyaelewa na hatimaye, kuyamwilisha katika maisha na vipaumbele vyao. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kujitahidi kusoma Neno la Mungu kila siku, ili waweze kumtambua Mwenyezi Mungu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanawahamasisha waamini kujenga utamaduni wa kusoma Neno la Mungu na kuwashirikisha jirani zao amana na utajiri unaofumbatwa katika Neno la Mungu na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia mambo, kama sehemu mchakato angavu na endelevu wa Mungu anayeondoa vikwazo na kuboresha dunia ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi za pa kuishi. Familia zijenge utamaduni wa kusali na kusoma Maandiko Matakatifu pamoja na kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maskini. Baba Mtakatifu Leo XIV anawakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi kuhusu usomaji wa Maandiko Matakatifu ni mwanzo wa kumfahamu Kristo Yesu. "Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo" ni nukuu maarufu ya Mtakatifu Jerome (kwa Kilatini: Ignoratio Scripturarum ignoratio Christi est), ikisisitiza kuwa kusoma Biblia ni muhimu kwa kumfahamu Yesu Yesu. Baba huyo wa Kanisa na mtafsiri wa Biblia (Vulgata) alisisitiza kwamba Neno la Mungu ni kama mwanga na msingi wa imani.
