2026.02.08 Angelus 2026.02.08 Angelus  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV:Bwana anatuita tufanye uzoefu wa ishara halisi za mshikamano

Ni ushirika na Yesu unaotuletea nuru ya amani kwa ulimwengu,ndivyo Papa ametafakari Injili ya Siku kabla ya Sala Malaika wa Bwana katika Dominika ya tano ya Kipindi cha Kawaida cha Mwaka,tarehe 8 Februari 2026 na kusisitiza kwamba hata wakati majeraha ya maisha yanapopunguza furaha ya kukutana na Bwana,Yeye hatatutupi kamwe.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, katika Dominika ya 5 ya Kipindi cha Kawaida cha mwaka, tarehe 8 Februari 2026, alitoa tafakari yake kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana kwa kuwageukia Waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican. Papa alisema kuwa “Baada ya kutangaza Heri, Yesu anawageukia wale wanaoishi ndani yake, akisema kwamba kwa sababu yao, dunia haiko vile vile na ulimwengu hauko gizani tena. "Ninyi ni chumvi ya dunia. [...] Ninyi ni nuru ya ulimwengu" (Mt 5:13-14). Kiukweli, ni furaha ya kweli inayotoa ladha kwenye uzima na kuakisi kile ambacho hakikuwepo hapo awali. Furaha hii inatokana na mtindo wa maisha, njia ya kuishi duniani na kuishi pamoja ambayo lazima itamaniwe na kuchaguliwa. Papa Leo XIV aliendelea kususutiza kwamba ni uzima unaong'aa ndani ya Yesu, ladha mpya ya ishara na maneno yake. Baada ya kukutana naye, chochote kinachojitenga na umaskini wake wa roho, upole wake na unyenyekevu wa moyo, njaa yake na kiu ya haki, ambayo huamsha rehema na amani kama mienendo ya mabadiliko na upatanisho, inaonekana kuwa isiyo na ladha na isiyoonekana.

Waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu kadhalika alisema kwamba Nabii Isaya anaorodhesha ishara halisi zinazokomesha dhuluma: kushiriki mkate na wenye njaa, kuwaleta maskini na wasio na makazi katika nyumba zetu, kuwavika walio uchi, na bila kuwapuuza majirani zetu na nyumba zetu wenyewe (Is 58:7). "Ndipo," nabii anaendelea, "mwanga wako utang'aa kama alfajiri, na jeraha lako litapona haraka". Kwa upande mmoja, mwanga, ambao hauwezi kufichwa, kwa sababu ni mkubwa kama jua ambalo kila asubuhi hufukuza giza; kwa upande mwingine, jeraha, ambalo hapo awali liliwaka na sasa linapona.

Sala ya Malaika wa Bwana 8 Februari 2026

Kiukweli, Papa alisema " ni chungu kupoteza ladha na kuacha furaha; lakini, inawezekana kuwa na jeraha hili mioyoni mwetu. Inaonekana Yesu anawaonya wale wanaomsikiliza wasiache furaha. Anasema, chumvi ambayo imepoteza ladha yake, "haifai tena kwa chochote ila kutupwa nje na kukanyagwa chini ya miguu" (Mt 5:13). Ni watu wangapi, labda tumepitia, wanahisi kama wanastahili kutupwa, kana kwamba wamekosea. Ni kana kwamba nuru yao imefichwa."

Waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Hata hivyo, Papa aliongeza “Yesu anatutangazia Mungu ambaye hatatutupa kamwe, Baba anayelinda jina letu, upekee wetu. Kila jeraha, hata liwe kubwa kiasi gani, litapona kwa kukumbatia maneno ya Heri na kuturudisha kwenye njia ya Injili. Hakika, ni ishara za uwazi kwa wengine na za usikivu zinazoamsha furaha tena. Hakika, katika unyenyekevu wao, zinatuweka dhidi ya wimbi. Yesu mwenyewe alijaribiwa, jangwani, na njia zingine: akidai utambulisho wake, akiuonesha, akiwa na ulimwengu miguuni pake. Hata hivyo, alikataa njia ambazo zingepoteza maana yake ya kweli, ile tunayogundua upya kila Dominika katika Mkate Uliovunjwa: uzima uliotolewa, upendo unaobaki kimya.

Papa akihitimisha alisema “Kaka na dada, hebu tujiruhusu kulishwa na kuangazwa na ushirika na Yesu. Bila onesho lolote, tutakuwa kama mji ulio juu ya kilima, sio tu unaoonekana, bali pia unaokaribisha na kukarimu: mji wa Mungu ambao kila mtu, hatimaye, anatamani kukaa na kupata amani.” Kwa njia hiyo tugeuze macho yetu na maombi yetu kwa Maria, lango la Mbinguni, ili atusaidie kuwa na kubaki wanafunzi wa Mwanawe.”

Waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here.

 

08 Februari 2026, 12:30