Waasisi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wamekuwa ni mashuhuda wa Neno la Mungu ambalo limemwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Waasisi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wamekuwa ni mashuhuda wa Neno la Mungu ambalo limemwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.  (ANSA)

Papa Leo XIV: Watawa Ni Manabii, Mashuhuda na Vyombo Vya Haki, Amani Na Maridhiano!

Waasisi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, wameacha amana, utajiri na urithi mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa; kwa ujasiri mkubwa, wakajikita katika maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, katika ukimya, wakalitafakari Neno la Mungu; kwa hekima na busara, wakasimama chini ya Msalaba, ili kujichotea neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni watu waliothubutu hata kuhatarisha maisha yao, ili wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Watawa Ulimwenguni ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 na kwa Mwaka 2026, Kanisa linaadhimisha Siku ya 30 ya Watawa Ulimwenguni kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Watawa Katika Mchakato wa Kueneza Maelewano na Amani.” Lengo la Maadhimisho haya katika maisha na utume wa Kanisa ni kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa huduma inayotolewa na watawa sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni Siku ambayo watawa hushiriki katika matukio mbalimbali ya Kiliturujia, kama alama ya shukrani. Ni muda muafaka wa kutafakari juu ya maisha na wito wa kitawa; kukuza mang’amuzi na uelewa zaidi ndani ya Kanisa! Watawa ni mashuhuda na vyombo vya neema ya Mungu inayomwilishwa katika maisha ya kidugu katika Jumuiya, huku wakishuhudia furaha ya Injili na upendo wa kidugu. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, lengo kuu la Siku ya Watawa Ulimwenguni ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwepo wa watawa ambao wameamua kumfuasa Kristo Yesu kwa kuishi mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Ni fursa kwa watawa kurudia tena nadhiri zao, ili kupyaisha maisha na utume wao mintarafu karama za mashirika yao ambayo ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa. Hii ni nafasi ya kuragibisha maisha na utume wa watawa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima sanjari na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao ili kukoleza utakatifu wa maisha.

Kristo Yesu ni Mwanga na nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni Mwanga na nuru ya Mataifa   (ANSA)

Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari ni changamoto na mwaliko kwa Wakristo wote kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mwenyezi Mungu sanjari na kushuhudia upendo wa huduma kwa jirani. Hii ni sikukuu ya mwanga na watu kukutana na Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa.Kimsingi Kristo Yesu anakutana na watu wake, wanaowakilishwa na Mzee Simeoni na Nabii Ana, Binti ya Fanueli. Manabii hawa wanamtambua Yesu kuwa ni Masiha, Kristo wa Bwana. Rej. Lk 2:22-40. Hapa upendo wa Baba wa milele anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, vinakutana na mwanadamu anayekesha na kungojea kwa imani ujio wa Mkombozi wa Ulimwengu, anayekuja kushiriki katika umaskini na udhaifu wa watu wake; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza! Lengo ni kurejesha tena ushirika kati ya Mwenyezi Mungu na viumbe vyake. Kristo Yesu ni nuru ya Mataifa.

Mashauri ya Kiinjili: Utii, Ufukara na Usafi Kamili
Mashauri ya Kiinjili: Utii, Ufukara na Usafi Kamili   (@VATICAN MEDIA)

Ndiyo maana, Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka thelathini tangu kuanzishwa kwake, Jumatatu tarehe 2 Februari 2026 watawa walianza maadhimisho haya kwa maandamano, huku wakiwa wamebeba mishumaa inayowaka mikononi mwao, changamoto na mwaliko kwa watawa, kuwaamsha walimwengu, kwa kutambua kwamba, wamekabidhiwa na Mama Kanisa utume wa kinabii, wao ni wajumbe na vyombo vya kutangaza na kushuhudia uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu, tayari kumwandalia njia kama Maandiko yasemavyo: “Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema BWANA wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Mal 3:1-2. Kristo Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu pekee, Mjumbe wa Agano jipya anayemtakasa mwanadamu kwa njia ya upendo, neema na huruma yake ya milele. Huu ndio utume ambao watawa katika maisha yao wanapaswa kuumwilisha kwa kujikita katika maisha ya sala na matendo, ili kueneza Ufalme wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Rej LG 44.

Watawa ni Mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano
Watawa ni Mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano   (ANSA)

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwenye Ibada ya Misa Takatifu, Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni Sanjari na Kumbukizi ya Miaka 30 tangu siku hii ianzishwe. Waasisi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, wameacha amana, utajiri na urithi mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa; kwa ujasiri mkubwa, wakajikita katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, katika ukimya, wakalitafakari Neno la Mungu; kwa hekima na busara, wakasimama chini ya Msalaba, ili kujichotea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni watu waliothubutu hata kuhatarisha maisha yao, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wanaosigana, watu wanaoathirika kwa vita na mipasuko ya kijamii, kiasi kwamba, wakawa ni ishara inayonenewa na hata wakati mwingine, wamekuwa ni mashuhuda wa imani kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Waasisi hawa wamekuwa ni mashuhuda wa Neno la Mungu ambalo limemwilishwa katika huduma.

Watawa ni Mashuhuda wa neema na baraka ya Mungu
Watawa ni Mashuhuda wa neema na baraka ya Mungu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi Kamili yanamwilishwa katika huduma ya upendo na kwamba, watawa wanaitwa na kutumwa kushuhudia uwepo wa Mungu anayeokoa. Huu ni ushuhuda kwa vijana wa kizazi kipya, wazee, maskini, wagonjwa na wafungwa wanapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa watawa sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ndio wanaopaswa kutolewa Sadaka Altareni na katika Moyo wake Mtakatifu, huku wakitambua kwamba, wao wenyewe ni Madhabahu ya uwepo angavu na endelevu wa Mungu kati ya waja wake, mwaliko kwa watawa kupiga magoti ili kuweza kukutana naye, kumwabudu na kumtukuza kwa njia ya maisha yao! Watawa wameendelea kuwa ni ishara ya uwepo angavu wa Mungu katika maeneo ya vita, ambapo utakatifu wa maisha ya watu unasiginwa kwa vita au kwa sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo! Maandiko Matakatifu yanasema: “Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.” Mt 18:10.

Watawa wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili
Watawa wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake kuhusu Sala ya Mzee Simeoni: “Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.” Lk 2:29-32. Maisha ya kitawa ni chemchemi ya mwanga wa matumaini unaoangazia maisha na utume wao wote. Mzee Simeoni na Nabii Anna walibahatika kumwona Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, akawa huru mbele ya maisha na kifo. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema: Kanisa ni chanzo cha utakatifu na neema, halitapata utimilifu wake isipokuwa katika utukufu wa mbingu, hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote. Huu ni ushuhuda ambao unaelekeza macho yake kwa mambo ya mbinguni.

Mashuhuda wa Neno la Mungu ambalo limemwilishwa katika huduma
Mashuhuda wa Neno la Mungu ambalo limemwilishwa katika huduma   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka ili kuwakomboa waja wake kutokana na wasiwasi na woga wa kifo. Katika uhuru wa kweli, watawa wanaweza kushuhudia upendo na msamaha usiokuwa na kipimo kama njia ya kuvuka kinzani na migogoro, ili hatimaye, waweze kua ni vyombo na wajenzi wa udugu wa kibinadamu. Mama Kanisa anapenda kuwapongeza na kuwashukuru watawa wote, kwa uwepo wao na anawahimiza kwenda wanakotumwa, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na matumaini. Mwishoni, mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwaweka watawa wote chini ya ulinzi na maombezi ya Bikira Maria Mama wa Kanisa na ya watakatifu waanzilishi wa Mashirika yao na katika Altare, wamepyaisha tena sadaka na maisha yao mbele ya Mwenyezi Mungu.

Papa Leo XIV Watawa 2026
03 Februari 2026, 17:15