Papa Leo XIV kwa Polisi:gundueni upya ujumbe wa Kikristo&mfanye kazi kwa dhamiri njema!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Uongozi, amri, utii, uzoefu wenye changamoto lakini wenye utajiri wa Jubilei, jijini Roma, kutangazwa kwa habari Njema, mapinduzi yasiyo na vurugu ya Injili, kugundua upya asili muhimu ya ujumbe wa Kikristo na kufanya kazi kwa dhamiri njema, ni maneno yaliyomo kwenye hotuba ya Baba Mtakatifu Leo XIV alipokutana na Vikosi vya Polisi, Roma -Jumuiya ya Mtakatifu Petro, Ijumaa tarehe 13 Februari 2026, katika Ukumbi wa Clementine wa Jumba la Kitume la Vatican. Miongoi mwa walioudhuria mkutano ni pamoja na Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Polisi Salvatore Luongo.
Papa alifurahishwa na majibu aliyopokea kutoka kwa wanachama wa Polisi wakati wa Jubilei iliyomalizika hivi karibuni: kwani alisema kuwa ulikuwa uzoefu "wenye changamoto kubwa" lakini pia "unaotajirisha", kibinadamu na kitaaluma. “Namshukuru Bwana kwa hili. Hakika, hii imekuwa hivyo kwetu sote tunaoishi Roma: ushuhuda wa mahujaji wengi umetujenga.” Kuanzia nyakati za hivi karibuni hadi mwanzo wa Ukristo, Papa alikumbuka jinsi jijini Roma, katika vitengo vyake mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ile ya kijeshi, "Habari Njema" ya Yesu ilianza kuenea mapema: njia mpya ya kuishi na kufikiri, iliyoongozwa na Mungu ambaye amekuwa upendo, huruma, na msamaha,” Papa alisisitiza.
Udugu miongoni mwa wanaume na wanawake wote unaopita tofauti zote za kijamii na kikabila, alisistiza. Miundo ya shirika, pamoja na utumiaji wa mamlaka na nidhamu, ni ya kawaida katika mfumo wa uendeshaji wa kijeshi na, ikiwa itatafsiriwa upya kwa nuru ya Injili, pia kwa ule wa Kanisa. Hakika, kwa karne nyingi, Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea, ujumbe wa Yesu umepenya miundo, vigezo, njia za kutenda na kufikiri kwa ustaarabu mwingi. Haukufanya hivyo kupitia mapinduzi ya vurugu, bali kupitia mabadiliko ya amani, kutoka ndani, kupitia dhamiri, ubadilishaji wa mioyo. Kwa njia hiyo, Injili inaeneza "hisia ya Mungu na mwanadamu," ikithibitisha tena heshima "kamili" kwa kuwepo na utu wa mwanadamu, "pamoja na ibada ya Mungu na Yeye pekee."
Baba Mtakatifu Leo aidha aliuliza kama hili silo hasa "linaloweza na lazima litokee katika kila kizazi, hata Ulimwenguni na Roma leo hii." Jibu la kuthibitisha linalopata msingi wake katika ngazi ya "juu" ya Majisterio ya kikanisa, ni Mtaguso wa Pili wa Vatican. Tumeitwa kugundua upya kiini cha ujumbe wa Kikristo na mtindo wa Kanisa changa, ili kuvifanya viwe mwili katika ulimwengu wetu tofauti sana na mgumu zaidi. Lakini Yesu Kristo ni yule yule jana, leo, na hata milele,” Papa alibainisha. Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV aliwashukuru Polisi kwa huduma yao, hasa katika eneo la Vatican na jiji la Roma. Ni matumaini yake kwamba kila mmoja wao atimize wajibu wake kwa "dhamiri safi," waaminifu kwa kanuni za Kipolisi, na kama Wakristo, wawe waaminifu kwa Injili, "ambayo inajaza kila nia na kila tendo kwa upendo wa Kristo."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
