Miaka 97 ya Mkataba wa Lateran: 1929-2026: Siku ya Wagonjwa & Papa Benedikto XVI
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tarehe 11 Februari 2026 inabeba matukio mazito katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni Siku ya Kumbukizi ya Mkataba wa Lateran “Patti Lateranensi: Lateran Treaty” uliotenganisha Kanisa na Serikali ya Italia na hivyo kuondoa kinzani na mwingiliano wa majukumu kati ya Taasisi hizi mbili zenye dhamana na majukumu tofauti, lakini zote zikiwa ni kwa ajili ya huduma kwa mwanadamu. Tangu wakati huo, Mama Kanisa akajikita zaidi katika masuala ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu. Ni uinjilishaji unaojielekeza zaidi katika ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili. Pili ni kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 13 Mei 1992 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes nchini Ufaransa kunako tarehe 11 Februari 1993. Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yanaadhimishwa Jumatano tarehe 11 Februari 2026. Kimataifa maadhimisho haya yanafanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Amani, Jimbo Katoliki la Chiclayo, nchini Perù: “Nuestra Señora de la Paz en Chiclayo.” Ujenzi wa Madhabahu haya ni jitihada za maisha ya kiroho na kichungaji zilizoasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu “Huruma ya Msamaria Mwema: Kupenda kwa Kubeba Maumivu ya Mwingine.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anakazia zaidi: Zawadi ya kukutana, furaha ya kuonesha ujirani mwema na uwapo katika huduma; Utume shirikishi katika huduma kwa wagonjwa; Kwa kusukumwa na upendo wa Mungu, ili kuwawezesha watu kukutana wao kwa wao sanjari na ndugu zao katika Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kauli mbiu hii inalenga kupyaisha sura ya Msamaria Mwema, wakati huu, kugundua uzuri wa upendo na mwelekeo wa kijamii wa huruma ya Mungu kwa ajili ya wahitaji, wagonjwa na wale wanaoteseka. Kilele cha maadhimisho haya, kimeyashirika Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Perù, sanjari na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, bila kuwasahau wagonjwa ambao ndio wahusika wakuu. Wagonjwa na wazee, katika maadhimisho haya, wamepewa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa, kwani kwa hakika upendo hauna budi kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wagonjwa. Magonjwa haya, kwa sehemu kubwa ni matokeo ya umaskini, upweke hasi, ndiyo maana wote hawa wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwa ufupi kabisa, Msamaria mwema: Alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake; akazitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Huu ndio mwelekeo alionao Kristo Yesu kwa binadamu, anayewaonesha huruma, upendo na ujirani mwema na kwamba, kwa njia ya huruma na upendo, waamini wanaweza kugeuka na kuwa ni majirani wema kwa wagonjwa na wenye shida. Kristo Yesu ni Msamaria kutoka mbinguni aliyemwonea huruma mwanadamu akamsogelea, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfunga mwanadamu majeraha yake. Upendo huu unarutubishwa kwa mwanadamu kukutana na Kristo Yesu, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi katika huduma kwa wakoma, akapata furaha ya kupenda kama ilivyokuwa kwa Msamaria Mwema. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee katika: Maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Sakramenti ya Upatanisho inawaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha, tayari kuwaonjesha majirani huruma na upendo huo kama ilivyokuwa kwa mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema.
Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013 Baba Mtakatifu Benedikto XVI alipotangaza kung’atuka kutoka madarakani kutokana na hali yake ya afya kuanza kudhorota. Walimwengu wakapigwa bumbuwazi. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akafariki dunia tarehe 31 Desemba 2023. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 5 Januari 2023, akaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Hayati Benedikto XVI kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani “Ultima Commendatio & Valedictio” na mazishi kufanyika kwenye Makaburi yaliyoko chini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican “Grotte Vaticane.” Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake alikazia umuhimu wa kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma na kuendelea kupata faraja kutoka kwa Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia uzuri na furaha ya Injili, Sheria ya shughuli za kichungaji. “Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho.” Lk. 23:46. Vatican ni kati ya nchi ndogo kabisa duniani, tarehe 11 Februari, 2026 inafanya kumbukizi ya miaka 97 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana saini Mkataba na Serikali ya Italia “Inter Sanctam Sedem e Italiae Regnum Conventiones” kwa kifupi “Patti Lateranensi” yaani “Mkataba wa Lateran” unaoratibiwa na kusimamiwa na Sheria za Kimataifa na hivyo kuhitimisha kile kilichojulikana “Masuala ya Roma, Questione Roman.” Hii ni Italia iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha shughuli za Kanisa na Serikali ya Italia. Kardinali Pietro Gasparri, Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati huo, kwa niaba ya Kanisa pamoja na Bwana Benito Mussolini, Waziri Mkuu wa Italia kwa niaba ya Serikali ya Italia, walitiliana saini Mkataba wa Lateran maarufu kama “Patti Lateranensi.” Mkataba huu ulikuwa na sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuhitimisha kinzani na mpasuko uliokuwa umejitokeza baada ya Serikali ya Italia kuvamia mji wa Roma kunako mwaka 1870. Mkataba huu ulitoa uhuru kwa Kanisa Katoliki nchini Italia kuweza kujiamria mambo yake bila kuingiliwa na Serikali.
Huu ni msingi wa uhuru wa kuabudu. Vatican ikapewa mamlaka kamili ya kujisimamia yenyewe katika shughuli zake na Serikali ya Italia, tangu wakati huo ikatambua uhuru na mamlaka ya mji wa Vatican hata katika udogo wake. Mkataba huu, uliiwezesha Vatican “Kiti Kitakatifu-Holy See” kuwa na uhuru kamili kuhusiana na masuala ya dini na imani. Sehemu ya Pili ya Mkataba huu, uliitaka Serikali ya Italia kulipa fidia kwa Vatican kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na Serikali wakati wa kuvamia mji wa Roma ambao ulikuwa ni ngome ya Kanisa Katoliki, kunako mwaka 1870. Serikali ikailipa Vatican fidia.Sehemu ya tatu ya Mkataba huu ni kuhusu: “Makubaliano ya Kifedha” “Convenzionale Finanzarie.” Huu ni utaratibu na kanuni zinazoratibu mchakato wa mahusiano ya ndani kati ya Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki nchini Italia. Katika sehemu hii, Maaskofu walipaswa kula kiapo cha utii kwa Serikali. Na Serikali kwa upande wake, ikalipatia Kanisa upendeleo wa kufundisha dini na kumwilisha Mafundisho tanzu ya Kanisa katika maisha ya hadhara. Serikali ya Italia ikatambua Sakramenti ya Ndoa na utenguzi wake kufanyika kwenye Mahakama za Kanisa. Mkataba wa Lateran uliifanya Vatican kutambuliwa rasmi kama nchi huru yenye uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe katika medani za Kimataifa bila kuingiliwa na Serikali ya Italia. Papa Pio XI alilitaka Kanisa kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia: kiroho na kimwili; kwa kutumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kitamaduni na kisanaa; mambo yanayofumbatwa katika Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihakikishia Italia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili kweli nchi ya Italia, iendelee kuwa aminifu kwa Mapokeo pamoja kupyaisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu ambao umeipambanua Italia kwa miaka mingi.
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Ikumbukwe kwamba, Haki msingi za binadamu zinazozungumziwa hapa ni zile zinazofafanuliwa katika Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na wala si ukoloni wa kiitikadi unaotaka kupenyezwa kwa mataifa maskini duniani! Mkataba huu, umekuwa ni ngome na ulinzi thabiti kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kuweza kutekeleza dhamana na utume wake kwa uhuru zaidi, bila kuingiliwa na chombo chochote kile! Dhamana na wito wa Vatican katika diplomasia, unafumbatwa katika utume wake wa maisha ya kiroho, kimaadili na utu wema kwa ajili ya familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Vatican haipendi kuingilia mambo ya ndani ya nchi, bali inapenda kusikilizwa kwa makini, kama chombo cha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, dhamana inayotekelezwa kwa unyoofu na unyenyekevu mkuu!
Itakumbukwa kwamba, Mkataba wa Lateran, ulifanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuendana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican. Ushirikiano kati ya Serikali ya Italia na Vatican unalenga kulinda, kudumisha na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mkataba unaojipambanua kwa kukazia uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Nchi ya Vatican inapaswa kuendelea kuwepo, ikiwa huru katika kujiamria mambo yake yenyewe, ili kutekeleza utume wake katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote. Mifumo ya kisiasa na sera mbali mbali zinazogusa utu, heshima na maisha ya mwanadamu na hata wakati mwingine kuzama katika undani wake. Vatican imekuwa mstari wa mbele kukemea uhuru usiokuwa na mipaka wala uwajibikaji; imekazia majadiliano katika ukweli na uwazi na mshikamano wa kidugu. Vatican ni kati ya nchi ambazo ziko mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu, kama mtu mmoja mmoja au taifa. Zote hizi ni kati ya sababu ambazo zinahalalisha uwepo wa Nchi ya Vatican ili iweze kutekeleza majukumu yake katika misingi ya ukweli, haki na uwazi. Vatican kutokana na ushiriki wake kwenye Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kutoa mchango mkubwa unaofumbata maendeleo fungamani binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, uhuru wa kuabudu na ule wa kidini unazingatiwa na kuheshimiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Mama Kanisa anapenda kutekeleza wajibu na utume wake akiwa huru kabisa, ili kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uhuru wa kidini ni haki ya kila dini au dhehebu lolote lile kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za nchi husika. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamekazia umuhimu wa Kanisa na Serikali kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu: kiroho na kimwili. Uhusiano kati ya Kanisa na Serikali unategemea kwa kiasi kikubwa: hali ya kitamaduni, kijamii, kisiasa na kihistoria kwa nchi husika. Mahali ambapo utawala wa sheria unaheshimiwa, Kanisa limekuwa likitekeleza wajibu kwa ajili ya maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Lakini, katika baadhi ya nchi, Kanisa limekuwa likikumbana na madhulumu na sera za kibaguzi zinazolibeza Kanisa kwa kudhani kwamba, linaingilia mambo yake.
Kanuni ya “mpe Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu” inapaswa kuwaongoza wanasiasa wenye misimamo mikali ya maisha. Kanisa, daima limeendelea kusoma alama za nyakati na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapaswa kutekeleza dhamana na utume wake katika mazingira huru kabisa. Kamwe, Khalifa wa Mtakatifu Petro, hatasita kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki msingi za wakimbizi na wahamiaji pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Biashara haramu ya silaha duniani, biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyavalia njuga katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Roma ya zamani ni maarufu sana kwa maendeleo ya sheria, utaratibu na ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa ujenzi imara na wakudumu, kielelezo cha uthabiti na uhakika wa usalama, mambo msingi yanayoufanya mji wa Roma kuwa ni kitovu cha ustaarabu na ukarimu kwa kuwapokea wageni na mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia na hivyo kuwashirikisha katika maisha yake ya kiraia na kijamii kiasi hata cha kuwapandisha hadhi kuwa ni sehemu ya viongozi wakuu wa Serikali. Utamaduni wa mji wa Roma ya zamani, ulisheheni tunu msingi na ujumbe uliosimikwa kwenye udugu wa kibinadamu, upendo, matumaini na uhuru wa kweli; mambo yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo. Huu ni mji ambao umesheheni shuhuda za wafiadini na waungama imani; vyombo na wajumbe wa Injili ya upendo. Kwa Warumi iliwabidi kufunga safari ya Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Golgota na hatimaye kuteremka chini kushuhudia Kaburi wazi la Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, jibu makini la ukweli, haki na upendo. Hii ndiyo Habari Njema ya Wokovu iliyotangwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu, aliyeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu na kubadili hali na mazingira ya nyakati zake. Kristo Yesu akawa ni chemchemi ya matumaini yaliyokuja kufutilia mbali kashfa ya utumwa kutoka katika sura ya nchi; utumwa unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Hali hii inajitokeza hata katika ulimwengu mamboleo, kwa kufahamu au kwa kutofahamu, kiasi cha kuhatarisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kiasi hata cha kuibuka kwa mifumo ya kibaguzi inayopelekea baadhi ya watu katika jamii kujikuta wakiwa hawana uhakika wa usalama wa maisha yao! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa Jiji la Roma. Alikazia dhamana ya Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Mkataba wa Lateran, uliofanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 na kwamba, kwa mwaka 2026, marekebisho haya yametimiza miaka 42; Umuhimu wa Mji wa Roma katika medani za Kimataifa sanjari na Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Roma ya utawala wa Kaisari ilifuatiwa na Roma ya Mapapa, warithi wa Mtume Petro, ambao "husimamia kwa upendo" juu ya Kanisa zima na ambao, katika karne kadhaa, pia walipaswa kuchukua jukumu la kubadilisha mfumo wa utawala na mamlaka ya kiraia katika mgawanyiko unaoendelea wa ulimwengu wa kale. Mambo mengi yalibadilika, lakini wito wa mji wa Roma kwa ulimwengu wote ulithibitishwa na kuinuliwa. Kwa kweli, ingawa upeo wa kijiografia wa Dola ya Kirumi ulikuwa na moyo wake katika ulimwengu wa Mediterania na, ingawa ulikuwa mkubwa sana, lakini haukuhusisha ulimwengu wote, kumbe, utume wa Kanisa hauna mipaka katika dunia hii. Kanisa halina budi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Kristo Yesu, matendo yake na maneno yake ya wokovu kwa watu wa Mataifa. Muungano wa Italia, ulifungua ukurasa na awamu mpya ilianza baada ya migogoro, kinzani na kutoelewana kati ya Vatican na Italia, hatimaye, ukafikiwa muafaka wa kile kinachoitwa “Suala la Kiroma” takribani miaka 97 iliyopita, upatanisho kati ya utawala wa kiraia pamoja na Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Roma ni mji wa pekee unaobeba historia ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, sanjari na Maadhimisho ya Miaka Mitakatifu. Mkataba wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya ICC ambayo kimsingi ni mahakama ya kwanza ya kudumu ya kimataifa ilioundwa ili kuwafikisha mahakamani watu wanaohusika na uhalifu mkubwa ikiwa ni pamoja na: uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari, Mkataba huu ulikuwa umejadiliwa kwa takribani miaka mitatu, na ulipitishwa baada ya kikao kilichofanyika mjini Roma 17 Julai1998. Baba Mtakatifu Francisko aligusia pia Michezo ya Olimpiki tangu mwaka 1960 na Roma kama makao makuu ya Mashirika ya Kimataifa kama, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO.) Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo lilinogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Yesu aliye hai na mbaye pia ni Mlango wa uzima. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hili ni tukio la maisha ya kiroho linalofumbata hija, toba na wongofu wa ndani, ili kuwakirimia waamini huruma na upatanisho.
Ni katika muktadha huu mji wa Roma ulihusika kikamilifu kuandaa miundo mbinu ili kupokea na kuwahudumia wageni, watalii na mahujaji wanaotembelea mjini Roma na hivyo maadhimisho haya yamekuwa na mchango mkubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao kwa mji wa Roma. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufanya maboresho makubwa kwa huduma za usafiri kwa mji wa Roma na hususan kwa wale walioko pembezoni mwa mji; Ulinzi na Usalama. Ni katika mwelekeo huu, uongozi wa Manispaa ya Jiji la Roma na Serikali ya Italia katika ujumla wake, ni wahusika wakuu, wanaopaswa kushirikiana na Kanisa ili maadhimisho ya Jubilei hii kama ambavyo pia Serikali ya Italia inavyopaswa kushirikiana na Vatican. Haya ni mahusiano yanayosimikwa katika utu na masuala ya fedha baadaye. Huduma hizi muhimu anasema Baba Mtakatifu Francisko zinapaswa kuwa ni ushuhuda wa Injili ya upendo: huduma ya ukarimu kwa wageni, watalii, wahamiaji na wakimbizi, maskini na watu pweke; wagonjwa na wafungwa, wawe kweli ni mashuhuda wa ari na mwamko huo wa Injili ya upendo. Mji wa Roma uendelee kuonesha uso wake wa kweli: Uso wa ukarimu uliotukuka. Umati mkubwa wa wahamiaji na wakimbizi; watalii na wageni unaweza kuonekana kama mzigo unaokwamisha mchakato wa ustawi na maendeleo ya mji wa Roma, lakini ikumbukwe kwamba, mji wa Roma ni wa kipekee sana ulimwenguni, kwani una mvuto wake mkuu na wajibu wake kwa Italia, Kanisa la kwa familia ya binadamu.
Kila shida ya mji wa Roma inaonesha ukuu wake na kwamba, shida hizi zinaweza kuwa ni fursa ya kuchochea maendeleo: kiraia, kijamii, kiuchumi na kitamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hazina kubwa ya utamaduni na historia iliyowekwa kwenye vilima vya Roma ni heshima na mzigo wa raia na watawala wake, na inangojea kuthaminiwa na kuheshimiwa vya kutosha. Kuzaliwa upya kwa asili na thamani ya Roma upyaishe kuzaliwa kwa kila mtu, ishara itakayo wasilisha mabara yote kwa kujikita katika ushirikiano wenye tija na ufanisi. Baba Mtakatifu anasema, tangu mwanzo akiwa bado Padre kijana, alikuza na kuendeleza ndani mwake Ibada kwa Bikira Maria Afya ya Warumi: “Salus Populi Romani” kumbe, Bikira Maria aendelee kuulinda Mji wa Roma na wananchi wake; awakirimie na kupyaisha matumaini, Bikira Maria afya ya Warumi aendelee kuhamasisha upendo, ili hatimaye, kuthibitisha mapokeo yake bora zaidi, na hatimaye, uendelee kuwa mwanga wa ustaarabu sanjari na kukuza amani.
