Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: Amani huanza na utu! Wito wa Kimataifa wa kukomesha biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: Amani huanza na utu! Wito wa Kimataifa wa kukomesha biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo.  (Siam Pukkato)

Maadhimisho ya Siku ya 12 ya Sala na Tafakari Dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu

Papa Leo XIV: “Amani huanza na utu! Wito wa Kimataifa wa Kukomesha Biashara Haramu ya Binadamu” ndiyo kauli mbiu inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo! Kila mwaka tarehe 8 Februari, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara ya Binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: “Amani huanza na utu! Wito wa Kimataifa wa Kukomesha Biashara Haramu ya Binadamu” ndiyo kauli mbiu inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo! Kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. “Amani iwe kwenu.” Yn 20:19. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo kwamba: Hii ni salam ya Kristo Yesu Mfufuka kwa wafuasi wake, sehemu ya mchakato wa upyaisho wa ubinadamu unaotambua ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika Ulimwengu mamboleo, binadamu anajikuta akitafuta amani kwa njia ya “Mtutu wa bunduki.” Vita, kinzani na misigano ni mambo yanayosababishwa na watu wenye uchu wa mali, fedha na madaraka; ni watu wanaotanguliza masilahi yao binafsi katika siasa au masuala ya kiuchumi. Biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo inashamiri sana kwenye maeneo ya vita, kinzani na migogoro ya kijamii; miongoni mwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum na kwamba, waathirika wakuu ni wanawake, wasichana na watoto. Kupanuka kwa pengo kubwa kati ya Nchi Tajiri na Nchi Zinazoendelea duniani ni kati ya mambo yanayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika biashara haramu ya binadamu, viungo vyake sanjari na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.

Biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo
Biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, wahusika wakuu wa biashara haramu ya binadamu wamesahau Injili ya huruma na mapendo, kama anavyofundisha Kristo Yesu. Kumbe, Sala na Uragibishaji wa vitendo hivi ni muhimu sana kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ili waweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo inaweza kushinda ikiwa kama binadamu atakuwa na maono mapya ya kwamba, kila binadamu ni mwana mpendwa wa Mungu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawatia shime wale wote wanaosimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaweza kufanya kazi kwa dhati kuondoa visababishi vya janga hili linalosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kila mtu anapaswa kuwa ni sauti ya wale wote wanaodhalilishwa katika utu wao kwa kuwa na ujasiri, uaminifu pasi na kuchoka wala kukatishwa tamaa.

Utumwa mamboleo unasigina utu, heshima na haki msingi
Utumwa mamboleo unasigina utu, heshima na haki msingi   (AFP or licensors)

Mtakatifu Josefina Bakhita, “Mwanamke wa shoka” alibahatika kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu kugeuza mateso na mahangaiko yake yote kuwa ni chemchemi ya Injili ya matumaini iliyogeuka hatimaye, na kuwa ni mbegu ya matumaini.  Mtakatifu Josefina Bakhita “Fortunata” maana yake “Bahati” alizaliwa kunako mwaka 1868 huko mjini Darfur, Sudan Kongwe. Akatekwa nyara na “watu wasiojulikana” akauzwa utumwani, na hatimaye, akanunuliwa na Balozi wa Italia mjini Khartoum aliyempeleka mjini Venezia. Akafundishwa katekesi na hatimaye, kubatizwa. Baadaye alijiunga na Shirika la Mabinti wa Upendo wa Mtakatifu Madgalena wa Canossa akijitoa sadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma. Alifariki dunia tarehe 8 Februari 1947 huko Schio, nchini Italia. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Josefina Bakhita kuwa Mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na hatimaye, akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe Mosi Oktoba, mwaka 2000 katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Biashara haramu na mifumo yote utumwa mamboleo ni hatari
Biashara haramu na mifumo yote utumwa mamboleo ni hatari   (Siam Pukkato)

Katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko likaanzisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni muda muafaka kwa ajili ya kusali na kuwaombea waathirika wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Wanawake wenye umri kati ya miaka 24-54 wanachangia asilimia 90% ya nguvu kazi katika uzalishaji. Lakini takwimu zinazonesha pia kwamba, kuna wasichana asilimia 30% hawajui kusoma wala kuandika; na wengi wao hawana fursa za ajira. Itakumbukwa kwamba, “Talita Kum” ambao ni Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa unatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 77 sehemu mbalimbali za dunia, tarehe 8 Februari 2024 umeandaa Siku ya Sala na Tafakari kuhusu athari za biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.

Papa Leo XIV: Amani Huanza na Utu
Papa Leo XIV: Amani Huanza na Utu   (Copyright Marlon Lopez MMG1design. All rights reserved.)

Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, ukipewa ushirikiano wa dhati na vyombo vya ulinzi na usalama kitaifa na kimataifa, uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Kumbe kuna haja kuwatambua waathirika, kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hapa kuna haja ya kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kutoa elimu makini; kwa kuendesha kampeni za uragibishaji sanjari na kuwalinda watu ambao wanaweza kutumbukizwa katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.

Mtakatifu Bakhita 2026
06 Februari 2026, 16:50