Kardinali Polycarp Pengo: Jabali la Maadili; Mshumaa Ulioacha Mwanga Usiozimika!
Na Mama Evaline Malisa Ntenga, Dar es Salaam, Tanzania.
Kanisa limempoteza Jabali wa maadili na utu wema, kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Katika makala haya, Radio Vatican inapenda kukushirikisha changamoto za afya zilizopelekea kifo cha Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam: Upasuaji mkubwa wa moyo na hatimaye kuwekewa “Pacemaker” pamoja na Upasuaji mkubwa kwenye uti wa mgongo uliodumu kwa takribani masaa 13 na uzee kama anavyosimulia Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam; Mchango wake katika kuwawezesha Wanawake Wakatoliki kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Makanisa mahalia ndani na nje ya Tanzania, Salam za rambirambi kutoka kwa Askofu Charles Kasonde wa Jimbo Katoliki Solwezi, Zambia ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA na takwimu kutoka Vatican baada ya kifo cha Kardinali Polycarp Pengo. Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA kwa niaba ya Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika WUCWO, “Unión Mundial de las Organizaciones Femeninas Católicas, UMOFC.” Tunamshukuru Mungu kwa maisha na utume wa Kardinali Polycarp Pengo, Askofu Mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, mchungaji ambaye huduma yake iliilimarisha Kanisa nchini Tanzania na kusaidia kutoa mwelekeo wa ushuhuda wa Kanisa Barani Afrika. Akiwa amezaliwa tarehe 5 Agosti 1944. Baba yake alikuwa anaitwa Mzee Joseph Pengo na Mama yake Bibi Rosaria Nzyungu na alizawaliwa katika Parokia ya Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, nchini Tanzania na alikuwa ni Mtoto wa sita kati ya watoto tisa wa Familia ya Mzee Joseph Pengo.
Kardinali Pengo aliyatoa maisha yake kwa Kanisa tangu alipowekwa wakfu kuwa Padre tarehe 20 Juni 1971, na baadaye kupitia miongo mingi ya uongozi wa Kikasisi uliotawaliwa na bidii ya kitume na nidhamu ya kichungaji, kina cha maisha ya kiroho, uadilifu, utu wema, na uaminifu usiotetereka kwa Injili, Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 11 Novemba 1983 akamteuwa kuwa Askofu wa Nachingwea; na tarehe 17 Oktoba 1986 Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Tunduru–Masasi, na baadaye Askofu Mkuu wa Jimbo kuu Katoliki Dar es Salaam (1992–2019), huko kote aliwatumikia watu wa Mungu kwa unyenyekevu, uwazi wa fikra, na uongozi thabiti, akijenga Kanisa lililojikita katika sala, malezi ya kiimani, na ushuhuda wa kweli, huku akiwahamasisha watu wa Mungu kulitegemeza Kanisa mahalia kwa hali na mali. Aliongozwa na kauli mbiu yake ya Kiaskofu: “Ecce Ego Domine, Yaani “Mimi hapa Bwana.” Akiwa msomi wa taalimungu maadili, alililetea Kanisani kipawa adimu: uwezo wa kuunganisha msimamo imara wa maadili, utu wema na moyo wa kichungaji wenye huruma na mapendo. Wengi Barani Afrika wanamkumbuka kwa sauti yake tulivu lakini yenye ujasiri, hasa katika nyakati ambazo Kanisa na jamii vilihitaji ukweli usemwe kwa hekima. Uongozi wake ulichangia kuimarisha misingi ya Kanisa, ikiwemo: majiundo, makuzi sanjari na malezi ya mapadre na hivyo, kukuza na kudumisha imani inayobadili maisha ya kila siku. Alipoteuliwa kuwa Kardinali mwaka 1998, alilitumikia si tu Kanisa la mahalia, bali pia Kanisa la Ulimwengu mzima, akileta sauti na uzoefu wa Afrika katika umoja mpana wa imani ya Kanisa Katoliki.
Huduma yake Barani Afrika ilifikia kilele muhimu alipoteuliwa kuwa Rais wa SECAM mwaka 2007 hadi mwaka 2009, jukumu lililoonesha imani na heshima kubwa aliyopewa na Maaskofu Katoliki wa Afrika na Madagascar. Kupitia wajibu huo, aliishi na kudhihirisha dhamira ya dhati ya kuimarisha umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Barani Afrika, na kusukuma mbele utume wa Kanisa Barani Afrika kama chombo na shuhuda wa: Upatanisho, haki, amani, na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Afrika walikazia pamoja na mambo mengine kuhusu ujenzi wa Kanisa Barani Afrika kama familia, ili kuepuka: Udini, Ukabila na ubinafsi na hivyo kuliekeza Kanisa kujikita katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu Barani Afrika, kwa kujielekeza pia katika utamadunisho wa Kanisa Barani Afrika. Mama Kanisa anataka kujikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Juhudi zote hizi hazina budi kwenda sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji. Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki si hoja ya msingi, bali ubora: Imani, Matumaini na Mapendo, kwa kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu. Rej. Ecclesia in africa, Yaani: “Kanisa Barani Afrika” N. 41-54. Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume mara baada ya Sinodi: Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika: Ninyi ni Chumvi ya Dunia… Ninyi ni nuru ya Ulimwengu” Mt 5:13-14 anatambua mchango mkubwa unaotolewa na wanawake Barani Afrika kwa malezi na makuzi ya kifamilia, kwa jamii na kwa Kanisa kwa kutumia karama na mapaji yao; kwa kutambua haki zao msingi, heshima na utu wao; Usawa. Zote hizi ni jitihada za kumkomboa mwanamke kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu aliyewathamini na kuwajali wanawake katika maisha na utume wake. Rej. Mt 15:21-28; Lk 7:36-50; 8:1-3, 10:38-42; Yn 4:7-42.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI alilitaka Kanisa Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanawake wanachukua nafasi yao ya pekee ya uwajibikaji na ushiriki katika maisha na utume wa Kanisa na hivyo wanawake wataweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rej Africae munus, n 55-59. Hii ni dhamana ambayo Kardinali Pengo katika maisha na utume wake aliitendea haki, kiasi cha kuiaminisha Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam katika malezi na makuzi ya waseminari walioko Visiga, Jimbo kuu la Dar es Salaam.Utume na dhamana hii ya WAWATA ya kushiriki katika malezi, makuzi na majiundo ya Mapadre sasa inatekelezwa na WAWATA katika majimbo yote ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Kama Wanawake wa Afrika, tunamkumbuka kama mchungaji mwenye moyo wa baba, ambaye huduma yake iliimarisha utu wa binadamu, heshima na haki msingi za binadamu, akasimama kidete kuimarisha familia, na kuwahimiza waamini kuishi imani yao ya Kikatoliki kwa uadilifu. Maisha yake yanabaki kuwa ushuhuda kwamba uongozi wa Kanisa lazima ujengwe juu ya sala, huduma, na upendo kwa watu wa Mungu na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma ya upendo! Tunamkabidhi Kardinali Polycarp Pengo katika huruma ya Mungu, kwa shukrani kwa kazi yake ya uaminifu katika shamba la Bwana kiasi kwamba akamjalia kuwa kweli ni jabali la maadili. Kristo Yesu, Mchungaji Mwema, amjalie pumziko la amani, amana na utajiri wake wa maisha ya kiroho na kiutu uendelee kulihamasisha Kanisa Barani Afrika kizazi baada ya kizazi kukua na kudumu katika: Kanuni maadili, Utu wema; Malezi na makuzi ya Mapadre; Umoja, upatanisho, haki na msamaha Barani Afrika.
Wakati huo huo, Askofu Charles Kasonde wa Jimbo Katoliki Solwezi, nchini Zambia ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, katika Salam zake za rambirambi kufuatia kifo cha Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, aliyefariki dunia tarehe 19 Februari 2026 majira ya Saa 4:00 Usiku, akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 81 amemtaja Kardinali Pengo kuwa ni kati ya viongozi Barani Afrika alionesha: ujasiri, hekima, ari na mwamko wa utume na shughuli za kichungaji Barani Afrika na kwamba, amana na utajiri huu, vitaendelea kulistawisha Kanisa Barani Afrika. Ni kiongozi aliyejizatiti kuhakikisha kwamba, Kanisa mahalia linajitegemea kwa kikamilifu kwa rasilimali fedha na watu; Kanisa linasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Haya ni mambo msingi yaliyomwezesha Kardinali Polycarp Pengo kuheshimiwa na watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Ni kiongozi aliyesimamia kanuni maadili na utu wema, kiasi kwamba, akawa ni jabali la maadili Barani Afrika; Sauti ya Kinabii kwa watu wasiokuwa na sauti. Ni kiongozi aliyeshimiwa na kuthaminiwa katika urika wa Maaskofu ndani na nje ya Bara la Afrika, akawa ni mshauri, chemchemi ya hekima, busara na ushauri; mambo ambayo yanaacha chapa ya kudumu kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, linapenda kuonesha mshikamano wake wa pekee kwa familia ya Mungu nchini Tanzania katika kipindi hiki cha maombezi ya Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania.
Ni katika muktadha wa Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu, Baba Mtakatifu Leo XIV amemtumia salam za rambirambi Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kufuatia kifo cha Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam kilichotokea tarehe 19 Februari 2026 majira ya Saa 4:00 Usiku, akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kutoa salama zake za rambirambi kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam. Anamshukuru Mungu kwa huduma ya Kiaskofu aliyoitekeleza katika majimbo kadhaa nchini Tanzania. Anamkumbuka hasa kwa sadaka na majitoleo yake katika malezi na majiundo ya awali na endelevu ya Makleri, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kati ya Mwaka 2007 hadi mwaka 2009 alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, akafanikiwa kuwaunganisha Maaskofu wa Kusini mwa Afrika na Kaskazini, kwa kukazia moyo wa SECAM kujitegemea kwa rasilimali watu na vitu. Na katika maisha na utume wake kama Kardinali, aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Mabaraza mbalimbali ya Kipapa kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuiweka roho ya Kardinali Polycarp Pengo, Mchungaji mnyenyekevu, katika huruma ya Kristo Yesu, Mchungaji Mwema. Kwa waombolezaji na wote walioguswa na msiba huu mzito, huku wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele, anapenda kuwapatia faraja na baraka zake za kitume! Takwimu kutoka katika Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 23 Februari 2026 Baraza la Makardinali lilikuwa na Jumla ya Makardinali 244 na kati yao 121 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hao wengine 124 kutokana na umri, wamepoteza haki ya kupiga na kupigiwa kura. Idadi ya Makardinali kutoka katika nchi 23 Barani Afrika ni Makardinali 28 na kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura ni 14 na wengine 14 wamepoteza haki kadiri ya Sheria za Kanisa.
