Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatatu tarehe 16 Februari 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatatu tarehe 16 Februari 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha.  (@VATICAN MEDIA)

Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha!

Kauli mbiu: “Huduma ya Afya kwa Wote. Uendelevu na Usawa.” Papa Leo XIV katika hotuba yake amekazia kuhusu uhusiano uliopo kati ya afya ya wote sanjari na afya ya kila mmoja; kukinga kama mbegu ya matumaini sanjari na afya moja! Hii kauli mbiu imekuja kwa wakati muafaka katika ulimwengu uliokumbwa na kinzani pamoja na miigogoro ya kivita inayokomba rasilimali nyingi sana za kiuchumi, kiteknolojia, na zinazojihusisha na kutengeneza silaha na vifaa vya kivita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Kipapa ya Maisha “Pontifical Academy for Life” (PAV) ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo tarehe 11 Februari 1994, kwa Motu Proprio, yaani Barua binafsi ya “Vitae mysterium, Fumbo la maisha.” Lengo la taasisi hii ni kusimama kidete kulinda na kutetea thamani ya maisha na utu wa binadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Taasisi hii ina dhamana ya kutafiti, kuunda utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo na kuhabarisha wadau mbalimbali changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai duniani! Ni wajibu wa taasisi hii kutenda katika hali ya uwazi na kwa haraka na kwamba, inapaswa kuwajulisha viongozi wa Kanisa, taasisi za elimu maumbile na sayansi ya biolojia ya binadamu; taasisi za kiafya; vyombo vya mawasiliano ya jamii na jumuiya za kiraia kuhusu shughuli na tafiti zake kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Taasisi ya Kipapa ya Maisha, inawajibika kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, utu na heshima yake, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kudumisha heshima kati ya vizazi. Ni wajibu wa taasisi hii kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu; kwa kuendeleza tunu msingi za maisha: kiroho na kimwili, ili kudumisha Ikolojia ya binadamu kwa kumpatia mwanadamu nafasi yake katika Kazi ya Uumbaji. Taasisi hii inapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na Sekretarieti kuu ya Vatican, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kuheshimu na kuzingatia dhamana na wajibu wa kila taasisi katika ari na moyo wa kushirikiana, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa maisha. Taasisi pia inashirikiana pia na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazojihusisha na tafiti kuhusiana na maisha ya binadamu!

Taasisi ya Kipapa Kwa ajili ya Maisha: Utu, heshima na haki msingi
Taasisi ya Kipapa Kwa ajili ya Maisha: Utu, heshima na haki msingi   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa utekelezaji wa dhamana na majukumu yake, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatatu tarehe 16 Februari 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha chini ya uongozi wa Monsinyo Renzo Pegoraro aliyeteuliwa na Papa Leo XIV tarehe 27 Mei 2025 kuwa ni Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha. Taasisi hii kuanzia tarehe 16 hadi 17 Februari 2026 inaadhimisha Warsha ya Kimataifa inayonogeshwa na kauli mbiu: “Huduma ya Afya kwa Wote. Uendelevu na Usawa.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amekazia kuhusu uhusiano uliopo kati ya afya ya wote sanjari na afya ya kila mmoja; kukinga kama mbegu ya matumaini sanjari na afya moja! Hii kauli mbiu imekuja kwa wakati muafaka katika ulimwengu uliokumbwa na kinzani pamoja na miigogoro ya kivita inayokomba rasilimali nyingi sana za kiuchumi, kiteknolojia, na zinazojihusisha na kutengeneza silaha na vifaa vya kivita. Kumbe, kuna umuhimu sana wakati huu kuhakikisha kwamba, rasilimali za dunia, nguvu na ustadi mkubwa vinatumika kwa ajili ya kulinda na kudumisha uhai na afya ya binadamu, si tu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya walaji, bali hi ni haki ya wote na kamwe huduma ya afya haiwezi kugeuzwa kuwa ni fursa. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha kwa kuamua kuchagua mada hii na kwamba, kuna uhusiano uliopo kati ya afya ya wote sanjari na afya ya kila mmoja; afya na maisha, hali inayotaka kufanyike majadiliano ya kina kati ya: Dawa, Siasa; Kanuni maadili na utu wema, kwa kuchunguza na kuangalia mifumo ya huduma ya afya binafsi sanjari na huduma ya afya kwa ajili ya umma.

Taasisisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha: Kuboresha maisha
Taasisisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha: Kuboresha maisha   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, kuna haja ya kufahamu mchakato mzima pamoja na kuchagua mbinu mkakati wa utekelezaji wa sera na mikakati hii: Kisiasa, kijamii, kiteknolojia mintarafu familia, kazi pamoja na mazingira yote ya kijamii, kwani maamuzi bora ya utekelezaji wa afya bora unategemea na mambo mengi yanayopaswa kuchunguzwa na kufanyiwa maamuzi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si faida ya “chapuchapu inayoweza kupatikana” hali hii inahitaji uvumilivu, ukarimu na mshikamano, kwa kutenda kama mtandao wa afya, ili kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia umuhimu wa Jamii kujenga utamaduni wa kinga, kama chemchemi ya matumaini ya maisha, ambayo leo hii inakosa uwiano mzuri hata katikati ya miji yenyewe. Vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia imekuwa ni chanzo cha kudhorota kwa huduma za afya kutokana na miundo mbinu ya afya kushambuliwa mara kwa mara na hivyo kusababisha huduma ya afya kuwa ni tenge. Binadamu wote wakiwa wamefungamanishwa na vifungo visivyoonekana na kuunda familia ya ulimwengu, ambayo ni ushirika mtukufu unaowajaza watu wa Mungu utakatifu, upendo na heshima. Huu ni utume ambao Taasisi ya Kipapa ya Maisha imesimika uzoefu wake, kumbe, haina budi kujielekeza huko.

Huduma ya Afya kwa wote: Uendelevu na usawa
Huduma ya Afya kwa wote: Uendelevu na usawa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu anasema, dhana ya afya moja ni mwingiliano wa sera mbalimbali kwa kutambua kwamba, afya ya binadamu inagusa sekta mbalimbali za maisha; kumbe, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo msingi ya kuzingatiwa katika ngazi ya mtu binafsi na katika ngazi ya Kitaifa na kwamba, mafao ya wengi ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa na hivyo kukuza na kudumisha ufanisi, mshikamano wa udugu wa kibinadamu pamoja na haki, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Jamii inajenga mifumo ya afya endelevu na yenye uwezo wa kukidhi mahitaji msingi ya huduma ya afya, kwa kuzingatia rasilimali zilizopo; sanjari na kuonesha imani kwa dawa, wafanyakazi wa sekta a afya, hata kama bado hakuna taarifa sahihi za kisayansi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inazuia vita, kinzani na mashambulizi yawe ya nguvu za kivita, maneno au kijeshi na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa ishirikiane na kushikamana kwa ajili ya kulinda, kutetea sanjari na kuragibisha afya ya binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, huduma muhimu ya Taasisi ya Kipapa ya Maisha itafanikiwa kuwa ni shuhuda wa huduma makini ya afya inayoonesha huduma ya Mungu kwa mwanadamu, ambao ni viumbe vyake.

Taasisi ya Maisha
16 Februari 2026, 14:32