Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 16 Februari 2026 alikutana na kuzungumza na Maafisa wakuu wa Serikali ya Italia “Prefetti dìItalia” Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 16 Februari 2026 alikutana na kuzungumza na Maafisa wakuu wa Serikali ya Italia “Prefetti dìItalia”   (@VATICAN MEDIA)

Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Maafisa Wakuu wa Italia: Huduma Kwa Watu wa Mungu

Papa Leo XIV katika hotuba yake, alikazia sana umuhimu wa: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza, na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji; msaada kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii na kwamba, amani na utulivu wa kijamii ni matokeo ya utekelezaji wa uhuru na haki msingi za kiraia. Mkutano huu, uliongozwa na Matteo Piantedosi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Italia. Serikali na Kanisa vinaweza kushirikiana katika huduma

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maafisa wakuu wa Serikali ya Italia “Prefetti dìItalia” ni wawakilishi wa Serikali katika ngazi ya mkoa na wilaya, wanao ratibu shughuli za utawala na usalama katika maeneo yao na hawa ni viungo wakuu kati ya Serikali kuu na Serikali za mitaa. Ni viongozi wanaosimamamia: usalama, amani na utulivu wa ndani; Ustawi na maendeleo ya kiuchumi; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Huduma za kijamii na kwamba, viongozi hawa wanawajibika moja kwa moja kwa Wizara ya Mambo ya Ndani. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 16 Februari 2026 alikutana na kuzungumza na Maafisa wakuu wa Serikali ya Italia “Prefetti dìItalia” katika hotuba yake, alikazia sana umuhimu wa: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza, na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji; msaada kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii na kwamba, amani na utulivu wa kijamii ni matokeo ya utekelezaji wa uhuru na haki msingi za kiraia. Mkutano huu, uliongozwa na Matteo Piantedosi, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Italia.

Hawa ni viongozi wanaowajibika kulinda uhuru na haki msingi za raia
Hawa ni viongozi wanaowajibika kulinda uhuru na haki msingi za raia   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV aliwasifu, kuwapongeza na kuwashukuru kwa kumtembelea mjini Vatican hali inayoonesha dhamiri yao ya kushirikiana na Vatican katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, kila upande ukiheshimu na kuzingatia dhamana na majukumu yake katika jamii na kwamba, Kanisa na Serikali vinaweza kushirikiana kwa karibu kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Kanisa linatekeleza dhamana hii kwa uongozi wake katika maisha ya kiroho, kama alivyowahi kukazia Mtakatifu Ambrose wa Jimbo kuu la Milano. Kutokana na Mapokeo ya kale ya Mama Kanisa kama sehemu ya uongozi wa watu wa Mungu, kukaibuka uongozi wa Majimbo “Diocesi” na Mkuu wa Jimbo akajulikana kama Askofu “Episkopoi.” Leo hii, Maafisa wakuu wa Serikali ya Italia katika utume na dhamana yao wanajizatiti zaidi katika kuhakikisha kwamba, kuna ulinzi na usalama wa raia na mali zao sanjari na ulinzi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mambo yanayofumbatwa katika amana na urithi wa watu wa Mungu nchini Italia mintarafu: kanuni maadili, utu wema na maisha ya kiroho.

Maafisa hawa wanapaswa kujizatiti katika ulinzi wa raia na mali zao
Maafisa hawa wanapaswa kujizatiti katika ulinzi wa raia na mali zao   (@Vatican Media)

Hawa ni viongozi wanaowajibika kulinda na kudumisha: Uhuru, haki msingi za raia na mali zao, kipaumbele cha kwanza kikiwa ni watu wadhaifu na wanyonge katika jamii. Pale ambapo kuna vurugu, kinzani na mipasuko ya kijamii, waathirika wakuu ni wanawake, wazee na watoto. Amani na utilivu unawawezesha wazee, kuwa na utulivu wa ndani pamoja na kupata huduma stahiki. Hali hii pia inapaswa kuwa ni kwa ajili ya familia, wagonjwa na vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuwa na mtazamo wa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Ulinzi na usalama wa raia na mali zao ni mambo yanayopaswa kukita mizizi yake katika mchakato wa kudhibiti mambo yote yanayopelekea makosa ya jinai, lugha chafu na matusi na kwamba, kama viongozi wanapaswa kutambua kwamba, hii ni huduma kwa watu wa Mungu inayotolewa kwa kuzingatia wema na ukarimu; Sheria, Kanuni na Katiba ya nchi ya Italia; kwa kuongozwa na dhamiri nyofu, mahali muafaka ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake pamoja na kuzingita usawa.

Serikali na Kanisa vinaweza kushirikiana katika huduma kwa watu
Serikali na Kanisa vinaweza kushirikiana katika huduma kwa watu   (@VATICAN MEDIA)

Kama viongozi wanapaswa kutawala na kukuza utulivu wa ndani kwa kukazia akili safi, uadilifu na dhamiri nyofu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hali inayohitaji ushirikiano na mshikamano na vyombo vya utawala katika ngazi mbalimbali; na pili kwa kuunganisha uwajibikaji wa kitaaluma na mwenendo wa maisha kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya taswira ya urasimu ili kuiboresha jamii. Katika dharura na majanga wajikite kikamilifu katika mshikamano wa kimaadili, ujasiri na haki. Wawe na matumizi mazuri ya teknolojia ya akili unde, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia pamoja na mambo mengine: ufahamu wa raia wake, uaminifu kazini na kwamba, wanaweza kujenga ushirikiano na mshikamano na Mama Kanisa kwa ajili kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza, na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji; kwa kutoa msaada kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Wakumbuke kwamba, tunu msingi za Injili zinachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa kitamaduni na kijamii nchini Italia.

Papa Leo XIV Maafisa wa Italia
25 Februari 2026, 14:35