Papa Leo XIV: Njia ya Ukatekumeni Mpya: Mashuhuda wa Injili na Katekesi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Njia ya Ukatekumeni Mpya ilianzishwa kunako mwaka 1968 huko Madrid, nchini Hispania. Wanachama wake wa kwanza ni watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini pamoja na changamoto mbalimbali walizokumbana nazo katika maisha. Njia ya Ukatekumeni Mpya ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto iliyotolewa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Paulo VI, akiwataka wanachama hawa kukita maisha yao katika ukweli wa maisha ya Kikristo, chemchemi ya furaha, matumaini na ushuhuda. Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu wa kimisionari, akiwataka pia kulea na kukuza miito ya kimisionari. Mtakatifu Yohane Paulo II akatambua na kuandika kwamba, asili ya chama hiki cha kitume cha Njia ya Ukatekumeni Mpya ni mwendelezo wa mchakato wa majiundo makini ya kikatoliki, muhimu sana kwa watu wa Mungu katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Mtakatifu Yohane Paulo II akawataka Maaskofu kuthamini mchango na huduma iliyokuwa inatolewa na wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!
Njia hii inapata chimbuko lake katika Neno la Mungu, Liturujia ya Kanisa na Maisha ya Kijumuiya yanayosaidia kurutubisha na kujenga udugu wa kibinadamu na ukomavu wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, imani ambayo inapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Huu ni uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa, changamoto iliyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ikapokelewa kwa moyo wa shukrani na unyenyekevu mkuu na Askofu mkuu Casimiro Morcillo wa Jimbo kuu la Madrid kwa wakati ule na hatimaye, kama moshi wa ubani, Njia ya Ukatekumeni Mpya ikaenea pole pole na harufu yake kuijaza Hispania hadi kufikia “miisho ya dunia.”
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, jumuiya inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo thabiti inakuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, ari na mwamko mpya wa kimisionari. Hii inatokana na ukweli kwamba, neema ya utume inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia waamini ari na nguvu ya kuwa kweli ni wamisionari. Waamini walei wanahamasishwa kuwa ni wamisionari kwa watu wanaowazunguka kwa kuwasikiliza na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili; kwani ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni chachu ya Uinjilishaji mpya inayokolezwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Bwana Francisco Josè Gomes Arguello Wirtz, maarufu kama “Kiko” alijitosa bila ya kujibakiza: kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka na kwa msaada wa Roho Mtakatifu akaanzisha Njia ya Ukatekumeni Mpya, mchakato wa maisha ya Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Bwana Francisco Josè Gomes Arguello katika safari ya maisha yake, alitikiswa sana, hatimaye, akagundua mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto iliyomfanya kuacha yote na kuanza kuandamana na maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 19 Januari 2026 amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Njia ya Ukatekumeni Mpya na kuwatia shime kujizatiti katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia; kwa kumwilisha karama yao katika mchakato wa uinjilishaji na katekesi kwani huu ni mchango mkubwa sana kwa maisha na utume wa Kanisa; unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, mwaliko wa kuwa ni wafuasi wa Kristo Yesu na mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili sehemu mbalimbali za dunia; waendelee kuwa ni mashuhuda wa furaha ya imani, ili kuwasaidia watu wengine kutambua uzuri wa kumfahamu Kristo Yesu, ili hatimaye waweze kukua na kukomaa katika dhamana yao ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza viongozi wote wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kwa ushuhuda na ushiriki wao katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaolenga pamoja na mambo mengine, kupyaisha imani ya Kikristo.
Huu ni mwaliko kwa waamini kugundua tena Sakramenti ya Ubatizo inayowawezesha waamini kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, ili kushiriki maisha na utume wake katika upendo na umoja; kwa kumfahamu Kristo Yesu, na hivyo kuendelea kuheshimu safari ya kila mtu na dhamiri nyofu, mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake kutoka katika undani wa maisha. Baba Mtakatifu anawahimiza wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kuwa ni sehemu ya Kanisa mahalia, kwa kushirikiana na kushikamana na Mapadre pamoja na Maaskofu wao, huku wakionesha furaha, unyenyekevu na kama wajumbe, vyombo na mashuhuda wa ushirika wa Kanisa. Mama Kanisa anawasindikiza, anawaenzi na kuwashukuru kwa mchango wao wa hali na mali na wakati huohuo, Mama Kanisa anamkumbusha kila mtu kwamba “alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru” 2 Wakor 3:17. Kumbe, utangazaji na ushuhuda wa Injili; Katekesi pamoja na shughuli mbalimbali za kichungaji hazina budi kuwa huru kutokana na vikwazo, ugumu, ukosefu wa uadilifu, ili zisije zikaamsha hisia za hatia na woga badala ya kukuza na kudumisha ukombozi wa ndani. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kwa majitoleo, ushuhuda, furaha na huduma mbalimbali wanazozitekeleza katika Kanisa na Ulimwenguni na kwamba, anawatia shime kuendelea na ari na mwamko huu, na hatimaye, akawabariki na kuwaweka chini ya ulinzi na maombezi ya Bikira Maria, ili aendelee kuandamanapamoja na kuwalinda.
