2026.01.29 Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Toledo,Hispania. 2026.01.29 Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Toledo,Hispania. 

Papa Leo XIV kwa Jimbo Kuu la Toledo:Na iwe wakati wa neema,msamaha na Huruma

Katika Maadhimisho ya Jubilei ya Shukrani ya Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Toledo,nchini Hispania,Papa alituma Ujumbe wake,kwa Kanisa linalochukuliwa kuwa moja ya kazi bora za mtindo wa Kigothic,ambalo pia litaadhimisha Mwaka wa Jubilei.Papa anawashukuru"waamini kwa kulinda na kutetea imani na ushirika na Kiti cha Petro kwa karne nyingi na kuwaomba wasiwasahau maskini."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV alituma ujumbe kwa waamini wa Jimbo Kuu la Toledo, nchini Hispania, ambao mwaka huu 2026 wanaadhimisha Jubilei ya miaka 800, tangu kuwekwa Jiwe na Msingi wa  Kanisa Kuu hilo la Mji na Mwaka wa Jubilei. Papa katika ujumbe huo  anabainisha kuwa: “Wapendwa waamini wa Jimbo Kuu la Toledo: Ni furaha kwangu kuzungumza nanyi leo, mnapotangaza hadharani shughuli zilizopangwa na Kanisa Kuu la Toledo kusherehekea miaka 800 ya ujenzi wa Kanisa kuu la Kigothic.

Mwaka huu wa Jubilei uwe wa neema, msamaha na huruma

Ni matumaini kwamba mwaka huu, 2026, na hasa Mwaka wa Jubilei wa Kanisa Kuu, utakuwa wakati wa neema, msamaha, na huruma; mwaka wa shukrani kwa kile ambacho Kanisa la Toledo limechangia katika historia ya Hispania, Ulaya, na Amerika Kusini.” Papa alielezea historia ya Kanisa hilo kuwa “Mnamo 1226, Askofu Mkuu Rodrigo Jiménez de Rada na Mfalme Mtakatifu Fernando III wa Castile waliweka msingi wa Kanisa kuu la Kigothic la sasa kwenye eneo la Kanisa la awali la Visigothi la Mtakatifu Maria. Kwa hivyo, mwaka huu, 2026, tunasherehekea miaka mia nane ya siku hiyo ya kukumbukwa.”

Kanisa limeshuhudia matukio mengi ya kihistoria

 “Kwa karne nyingi, Papa Leo alibainisha kuwa, Kanisa Kuu hilo limeshuhudia matukio mengi, hasa kilele cha ushindi mpya wa Wafalme Wakatoliki wa Ufalme wa Granada na uinjilishaji wa Ulimwengu Mpya, matukio ambayo hayatakufa katika sanaa ya Kanisa kuu.” Katika mwaka huu wote, “Kanisa kuu litaonesha, kupitia sherehe muhimu za kiliturujia na matukio ya kiutamaduni, urithi tajiri wa kiroho wa Kanisa hili maalum na maono yake ya mustakabali wenye matumaini.”

Thamani ya liturujia ya Hispania-Mozarabic

Katika suala hili, Papa alisema “ningependa kusisitiza thamani ya liturujia ya Hispania-Mozarabic inayoadhimishwa kila siku katika Kanisa Kuu. Kama "mawe yaliyo hai," mmelinda na kutetea imani na ushirika na Kiti cha Petro kwa karne nyingi. Asante kwa ushuhuda wenu.” Pia Papa Leo alipenda kutoa shukrani zake kwa kazi ya upendo na kijamii inayofanywa na “Kanisa Kuu la Toledo, inayojali aina mpya za umaskini zinazojitokeza katika jamii yetu leo.”

Uvumilivu kwa sababu haiwezekani kuwasahau maskini

Papa aliwahimiza wavumilie kwa sababu "haiwezekani kuwasahau maskini ikiwa hatutaki kujiondoa kwenye mkondo hai wa Kanisa unaotiririka kutoka Injili na kufanya kila wakati wa historia kuwa na matunda" (Wosia wa Kitume Dilexi te, 15). Katika wakati huu wa neema na upyaisho  kwa Kanisa katika hija ya kwenda Toledo, Papa anawasindikiza na sala zake. “Bwana na Mama yake Mtakatifu, Bikira wa Hema, Mlinzi wao, awalinde kila wakati. Kwa upendo, aliwapa baraka zake.

PAPA JIMBO KUU TOLEDO

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here.

29 Januari 2026, 17:49