Papa Leo XIV Akutana na Kuzungumza na Vijana wa Jimbo Kuu la Roma 2026
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, ni fursa kwa Mama Kanisa kukuza na kudumisha utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya: kwa kujenga sanaa na utamaduni wa: kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia kufanya maamuzi magumu katika safari ya maisha yao kadiri ya mwanga wa Injili ya Kristo Yesu na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Vijana wanatamani kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha na utume wao ndani ya jamii na wanataka wapewe rasilimali na mtaji wa mambo msingi, tayari kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wanataka kulindwa na kutunzwa; kueleweka na kupendwa! Vijana wengi ni watu wenye ujasiri na uwezo wa kujifunza kikamilifu, tayari kuzama katika tunu msingi za maisha ya imani, matumaini na mapendo kamili kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wote! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni nafasi ya kusikiliza kwa makini ujumbe wa Neno la Mungu, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vya watu. Hapa kuna haja ya kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama binadamu, kwa kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo.
Vijana wanayo mengi ya kujifunza kutoka kwa waamini ambao licha ya patashika nguo kuchanika, wameendelea kusimama imara katika imani, wakiwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Imani thabiti iwasaidie vijana kukutana na vijana wenzao, wakiwa tayari kupambana na changamoto mamboleo, hususan juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na upweke hasi unaowazamisha vijana katika dimbwi la kifo. Bado kuna mizizi ya imani inayopaswa kumwilishwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko hata katika ulimwengu mamboleo, kama njia ya kujibu kikamilifu changamoto mamboleo. Kwa kukutana na vijana wenzao, wanagundua umuhimu wa kutoka na kwenda kushiriki katika tukio hili kama ilivyokuwa kwa Ibrahim, Baba wa imani. Vijana wanapaswa kuwa tayari daima ili kuandika kurasa mpya za maisha yao kwa njia ya ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, kwa kuwa na mvuto kwa wale wote wanaowazunguka. Kwa hakika, vijana wanapaswa kuwa ni chemchemi ya: Imani, mapendo, furaha na matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa “Leo ya Mungu katika maisha yao” kwa kutumia vyema nguvu na kipaji chao cha ubunifu.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV hivi karibuni alikutana na kuzungumza na vijana kutoka Jimbo kuu la Roma; akapata nafasi ya kusikiliza shuhuda zao kuhusu: upweke hasi, matumaini na kiu ya haki na amani; na hatimaye, akawapatia neno la kuwaongoza katika hija ya maisha yao. Hili lilikuwa ni tukio la: Imani, Matumaini; Mapendo; Katekesi, Sala na Sherehe ya Vijana, hasa baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Lengo anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV ni kuwawezesha vijana kukutana na hatimaye, kutembea kwa pamoja, ili kujenga na kudumisha ari na moyo wa urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu; tunu msingi zinazowawezesha vijana wa kizazi kipya kupata ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazowaandama katika hija ya maisha yao hapa duniani. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kushinda kishawishi cha upweke hasi ambao wakati mwingine, unawafanya vijana wa kizazi kipya kuchungulia kaburi.
Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Kristo Yesu daima yuko kati yao na anapenda kutembea pamoja nao katika maisha ya: Sala, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, Katika Neno lake na hasa zaidi katika historia ya maisha ya kila mmoja wao, changamoto na mwaliko kwa vijana kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu katika maisha yao! Vijana katika shida, magumu na changamoto za maisha, wanapaswa kusimika maisha yao katika imani! Baba Mtakatifu Leo XIV alitumia fursa hii, kuonesha masikitiko yake na hatimaye, kutoa salam za rambirambi kutokana na maafa yaliyosababisha vijana 40 kupoteza maisha yao huko Crans Montana, nchini Uswis! Hiki ni kipindi kwa wazazi na walezi wa vijana waliofariki dunia, kujitahidi kusahau, na watambue kwamba, wako pamoja.
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yalinogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kadiri ya takwimu zilizotolewa, kuna waamini zaidi ya milioni 33.5 kutoka katika nchi 185 waliopitia katika Lango la Jubilei. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yalizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Desemba 2024. Kwa hakika mahujaji wa matumaini kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamepitia katika Lango hili, ambalo litaendelea kubaki wazi katika maisha ya kiroho kwa wale ambao bado wametia nia ya kuhatarisha maisha yao, wanaosikia hamu ya kuondoka na kutafuta ukweli wa maisha katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu anayejifunua kwa walimwengu na mganga wa maisha ya kiroho kwa waja wake. Hawa ni watu kutoka katika: mataifa, lugha na tamaduni mbalimbali waliokusanyika kwa ajili ya sala, wakiombea amani sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, kwa sasa vijana wanaitwa na kutumwa kuwa si tu mahujaji bali mashuhuda wa matumaini kwa kushinda upweke hasi na hivyo kujitahidi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mahusiano ambayo kimsingi ni sehemu ya maisha, upendo na wokovu.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru waamini wa Jimbo kuu la Roma kwa wema na ukarimu wao kwa mahujaji waliofika kwa ajili ya hija, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Jua la haki linalowapatia joto la upendo, tayari kuleta mabadiliko katika jamii, yatakayowawezesha kuwa ni mashuhuda wa urafiki wa kijamii, changamoto na mwaliko kwa vijana kuwa na maisha mema na bora, tayari kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha. Huu ni upendo ambao hauna machweo yake; upendo unaowang’oa kutoka katika wasi wasi na hivyo kukuza ndani mwao amani ya kweli. Amewataka vijana kuendelea kuwajibika katika jamii, siasa, familia na Kanisa kwa kupata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya maisha yao na kwamba, yatazaa matunda na kutoka kwa Mungu, yatazaa utakatifu. Urafiki na Kristo Yesu ni msingi wa imani. Urafiki na Kristo Yesu ni msingi wa imani unaoweza kuwasaidia kujikita katika mchakato wa ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi na hasa ikiwa kama upendo huu ni mwangwi wa mahusiano na mafungamano na upendo wa Mungu, ili kupata ukamilifu wa maisha!
Vijana wanapaswa kuondoa utupu wa ndani katika maisha yao kwa kujikita katika maisha ya: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; Kusoma, Kutafakari na Kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha; kwa kutekeleza matendo ya huruma kiroho na kimwili, ushuhuda wa imani tendaji na hivyo Kristo Yesu anawawezesha kuwa nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia na kwamba, Bikira Maria awe ni mfano bora wa kuigwa. Rej Lk 1:46-47. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuwa kweli ni mashuhuda wa furaha ya Injili inayobubujika kutoka katika upendo wa Kristo Yesu. Vijana wajitahidi kutoa kipaumbele cha pekee kwa uwepo wa Kristo katika maisha yao; kwa kujenga utamaduni wa kumsikiliza kama Mwalimu wao wa maisha na kumfuasa kama Mchungaji wao mkuu. Watakatifu katika maisha na utume wao, walikuwa huru, wakawa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu na kwamba, Mwenyezi Mungu anawakirimia upendo usiokuwa na mipaka. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya kwa pamoja kulipenda Kanisa na kuendelea kulipyaisha! Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwapatia vijana wa kizazi kipya baraka zake za kitume, wao pamoja na wapendwa wao!
Kwa upande wake, Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma katika hotuba yake ya utangulizi, ili kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV kuzungumza na vijana wa Jimbo kuu la Roma, alipenda kumwonesha “Uso wa ujana wa Kanisa” kutoka kwa vijana wa Jimbo kuu la Roma waliofika kwa wingi kama sehemu ya utekelezaji wa nia yao ya kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro; nia ambayo waliionesha mara baada ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, iliyoadhimishwa mwezi Agosti, 2025 kwenye viwanja vya Tor Vergata, Roma. Vijana wa Roma wameonesha na kushuhudia ukarimu kwa vijana wenzao kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofika mjini Roma kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Amewashukuru wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Jubilei. Sera na shughuli za kichungaji zinatoa kipaumbele cha kwanza kwa vijana wa kizazi kipya! Kanisa linataka kuwapatia matumaini mapya vijana waliotumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo bila kuwasahau vijana wanaoteseka kutokana na changamoto mbalimbali za maisha!
