Angelo Gugel alibahatika katika maisha yake kutoa huduma kwa Mapapa watatu yaani: Yohane Paulo wa kwanza, Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Angelo Gugel alibahatika katika maisha yake kutoa huduma kwa Mapapa watatu yaani: Yohane Paulo wa kwanza, Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Benedikto XVI.   (©Riccardo Capobianco)

Marehemu Angelo Gugel Alibahatika Kuwahudumia Mapapa Watatu!

Angelo Gugel, aliyekuwa na umri wa miaka 90 amefariki dunia tarehe 15 Januari 2026 na anazikwa huko Miane, Jimbo la Treviso alikozaliwa, Jumatatu 19 Januari 2026. Angelo Gugel alibahatika katika maisha yake kutoa huduma kwa Mapapa watatu yaani: Yohane Paulo wa kwanza, Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Alikuwa ni shuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo; Mtume mwaminifu wa Kristo na Kanisa, akajiaminisha mbele ya Mungu katika huduma

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la mateso na Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao! Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi! Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ameganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu. Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo.

Marehemu Angelo Gugel amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90
Marehemu Angelo Gugel amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90

Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.

Marehemu Angelo Gugel ni mtume na shuhuda wa tunu za Kiinjili
Marehemu Angelo Gugel ni mtume na shuhuda wa tunu za Kiinjili   (©Riccardo Capobianco)

Angelo Gugel, aliyekuwa na umri wa miaka 90 amefariki dunia tarehe 15 Januari 2026 na anazikwa huko Miane, Jimbo la Treviso alikozaliwa, Jumatatu 19 Januari 2026. Angelo Gugel alibahatika katika maisha yake kutoa huduma kwa Mapapa watatu yaani: Yohane Paulo wa kwanza, Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake za rambirambi kwa mke na watoto wake anasema, kwa hakika Angelo Gugel alikuwa ni mtumishi na shuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo katika huduma kwa Kanisa. Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu Angelo Gugel, mtume mwaminifu wa Kristo Yesu, ili aweze kupokelewa katika makao ya uzima wa milele. Anapenda kuwafariji wale wote wanaoomboleza kwa msiba huu mkubwa. Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenye Kanisa la “Santa Maria delle Grazie alle Fornaci” Jimbo kuu la Roma, karibu kabisa na Vatican; imehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Vatican, waliomwelezea Marehemu Angelo Gugel, kwamba, alikuwa ni: Mtu mwema, Baba aliyewajibika, mpole na mtu wa haki; mtu mwenye furaha, mwamini mwaminifu mwenye imani thabiti, hata kama alizaliwa na kukulia kwenye umaskini. Ni mtu katika maisha na utume wake, aliyejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, akashirikiana na wengine katika huduma kwa viongozi wa Kanisa.

Marehemu Angelo Gugel amewahudumia Mapapa watatu katika maisha yake
Marehemu Angelo Gugel amewahudumia Mapapa watatu katika maisha yake   (©Riccardo Capobianco)

Licha ya changamoto ya afya kwa miezi ya hivi karibuni, anasema, Kardinali Pietro Parolin, aliendelea kuwa na utulivu na amani ya ndani, ushuhuda kwamba, kwake, hii ilikuwa ni fursa ya kushuhudia imani iliyomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Kusali Ibada ya Misa kwa ajili ya kumwombea marehemu, ni ushuhuda wa imani na fursa ya kupyaisha tena imani na matumaini juu ya Fumbo la Kifo na Ufufuko wa wafu uletao maisha na uzima wa milele.Kwa upande wake Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Krakow, na ambaye alikuwa Katibu muhtasi wa zamani wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika salam zake za rambirambi kwa familia ya Angelo Gugel, ameukumbuka utumishi wake kwa Kanisa Takatifu, kama kielelezo cha mtumishi mwaminifu na mwenye busara ya Kiinjili, aliyejitosa bila ya kujibakiza; mtu mwenye busara, nidhamu na bidii ya kazi. Sasa, apokelewe mbinguni na Baba mwenye huruma, akitambua thawabu ya wenye haki. Amemshukuru Marehemu Angelo Gugel, kwa kuonyesha shukrani zake za dhati kwa ajili ya utumishi wake wa uaminifu katika kipindi chote cha maisha na utume wa Mtakatifu  Yohane Paulo wa Pili, uliotekelezwa kwa hisia za wajibu na uaminifu kwa Kanisa.

Fumbo la Kifo

 

18 Januari 2026, 14:40