Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026   (ANSA)

Ujumbe wa Papa Leo XIV wa Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani 2026

Ujumbe wa Papa Leo Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na inayopokonya Silaha." Hii pia ni Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Mama Kanisa tarehe Mosi Januari ya kila Mwaka anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu: Mwaliko wa kudumisha imani inayosimikwa katika ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanuni ya Baraka: “Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia; BWANA akubarikie, na kukulinda; BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani. Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.” Hes 6:22-27. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na inayopokonya Silaha." Hii pia ni Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Mama Kanisa tarehe Mosi Januari ya kila Mwaka anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu: Kwa lugha ya Kigiriki: Theotokos, Θεοτόκος; kwa Kilatini "Deipara" au "Dei genitrix." Kiri ya imani kwa Bikira Maria Mama wa Mungu, na Bikira Maria Mama wa Kristo ni mfano bora wa kuigwa katika kulinda na kudumisha imani inayomwilishwa katika ushuhuda. Ilikuwa ni tarehe 26 Juni 431 katika maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso, Mababa wa Kanisa walipotamka kwamba, yule ambaye Bikira Maria amemchukua mimba kama mtu na ambaye amekuwa ni Mwana wake kadiri ya mwili, ndiye Mwana wa milele wa Baba, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kwamba, kweli Bikira Maria ni "Mama wa Mungu" "Theotokos, Θεοτόκος." Hiki ndicho kiini cha Taalimungu na Ibada kwa Bikira kwa sababu mhusika mkuu ni Mwenyezi Mungu. Katika Agano Jipya, Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Yesu. Tangu mwanzo, Kanisa lilimtambua Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu lakini kiri hii ya imani ikaendelezwa na kufikia kilele chake kwenye Mtaguso wa Efeso wa Mwaka 431 ili kukabiliana na changamoto zilizoibuliwa na wazushi wa nyakati zile, waliokuwa wanapinga Umungu wa Kristo. Mtaguso wa Efeso ukaweka mafundisho haya kuwa ni sehemu ya Kanuni ya Imani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kanisa. Kristo Yesu alitungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, tarehe Mosi Januari 2026
Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, tarehe Mosi Januari 2026

Kumbe, Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli. Katika karne ya tatu kulizuka mgogoro kuhusu Umungu wa Kristo na Ubinadamu wake. Mtaguso wa Efeso ulifafanua kwa kina na mapana kuhusu imani ya Kanisa na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Waamini wa Efeso wakashangilia sana na huo ukawa ni mwanzo wa kukua na kuendelea kuimarika kwa Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu tangu wakati huo hadi sasa. Bikira Maria ni Mama pia wa maisha ya kiroho kama alivyofafanua Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Bikira Maria alitekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, akawa ni zaidi ya mfuasi wa Kristo Yesu kwa sababu alikuwa kwanza kabisa ni Mama wa Kristo. Huu ni uhusiano wa ndani kabisa uliojengeka kati ya Bikira Maria na Kristo Yesu kutokana na imani thabiti ya Bikira Maria. Bikira Maria Mama wa Mungu ni cheo kikubwa kutokana na upendeleo na neema aliyopata kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hiki ni kiini cha imani ya Kanisa. Bikira Maria Mama wa Mungu kama anavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu anapaswa kuwa ni kiungo cha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo na kamwe asiwe ni sababu ya mipasuko, kinzani, migawanyiko na utengano.

Heri na Baraka za Mwaka Mpya 2026
Heri na Baraka za Mwaka Mpya 2026   (AFP or licensors)

Siku ya Kuombea Amani Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Paulo VI, tarehe Mosi, Januari 1968. Mtakatifu Yohane XXIII katika Wosia wake wa Kitume, "Pacem in terris" yaani "Amani Duniani": Kuhusu Kuimarisha Amani Kati ya Watu Wote. Katika ukweli, haki, upendo na uhuru anasema: Amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Naye Mtakatifu Paulo VI anasema, amani ni jina jipya la maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani kwa kuzingatia: Utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi. Ujumbe Baba Mtakatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani hutumwa kwa wakuu wa nchi na Jumuiya ya Kimataifa. Ujumbe huu huonesha dira na mwelekeo wa utendaji wa shughuli za kidiplomasia zitakazotekelezwa na Vatican katika kipindi cha Mwaka mzima. Amani kama tunda la haki, linamtazama mwanadamu katika ujumla wake, kiroho, kimwili, kisiasa, kiuchumi na hata kiutamaduni. Na kwamba, mwanadamu anapaswa kupata haki yake ya msingi katika hayo, ile haki ya kuzaliwa nayo, kinyume cha hapo tayari mwanadamu anakosa haki yake ya msingi, na ndio chanzo cha vurugu na kukosekana kwa amani katika jamii. Ni wazi kwamba, binadamu anapokosa haki yake, na utu wake unaposhindwa kuheshimiwa hupandwa na jazba na kuchanganyikiwa na hata kuwa chanzo cha vurugu. Kunakuwa na tishio la amani mtu anapopewa baadhi tu ya yale anayopaswa kuyapata kama binadamu, pale hadhi yake inaposhindwa kuheshimiwa na kuthaminiwa; na pale maisha yake ya kiraia yasipoelekezwa kwenye: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Heri na Baraka Kwa Mwaka Mpya 2026
Heri na Baraka Kwa Mwaka Mpya 2026   (@VATICAN MEDIA)

Ulinzi wa ukuzaji wa haki za binadamu ni muhimu kwa ujenzi wa jamii yenye utulivu na amani, na yenye maendeleo yaliyokamilika kwa kila mmoja na kwa watu wote kwa ujumla wao. Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika hotuba yake ya tarehe 22 Oktoba 1987 kwenye Mkutano mkuu wa tatu wa CCM alisema haki ni msingi wa amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, siasa inawajibu na inapaswa kuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa haki na amani jamii.Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na Inayopokonya Silaha.” Takwimu zinaonesha kwamba, gharama za manunuzi ya silaha yameongezeka kwa asilimia 9.4%, ikilinganishwa na kipindi cha Mwaka 2024. Kiwango hiki ni sawa na Dola za Kimarekani bilioni 2, 718 sawa na Aslimia 2.5% ya Pato Ghafi la Ulimwengu. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kuelekea kwenye amani isiyo na silaha, na inayopokonya silaha. Hii ni amani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Mfufuka, changamoto kwa wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano. Amani ni mchakato, ni safari na mwanga wa mapito katika maisha. Amani ni zawadi kutoka kwa Kristo Yesu: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” Yn 14:27. Hata katika hali ya kutisha, Kristo Yesu alimwambia Mtume Petro: “Rudisha upanga alani mwake.” Yn 18:11.

Madhara ya Vita katika katika Ulimwengu mamboleo
Madhara ya Vita katika katika Ulimwengu mamboleo   (AFP or licensors)

Amani ni ukweli unaopaswa kumwilishwa katika maisha. Mabilioni ya Dola za Kimarekani yanayotumika kununulia silaha yangeweza kusaidia kuboresha maisha ya watu wengi duniani, kumbe kuna haja ya kuzuia ukatili wa vita kwa sababu maendeleo ya silaha za kisayansi yameongeza sana ubaya na ukatili wa vita. Rej. Gauium et spes, 80. Baba Mtakatifu Leo XIV anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza katika amani inayopokonya Silaha; amani inayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili; kwa kuheshimiana, kuthamininiana pamoja na kuheshimiana. Huu ni mwaliko wa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi na kwamba, amani si swala la kufirikika tu, bali ni jambo linalo simikwa katika: maelewano na utekelezaji wa majukumu yanyofikiwa. Ni amani inayosimikwa katika diplomasia, majadiliano, kanuni na sheria za Kimataifa kwa kuimarisha taasisi za Kimataifa katika utekelezaji wa majukumu yake. Haki, Amani, Utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee, ili kurejesha tena Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; binadamu wajifunze kusaidiana! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na inayopokonya Silaha."

Siku ya 59 ya Kuombea Amani
31 Desemba 2025, 16:53