Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake kwa Sekretarieti kuu ya Vatican amekazia mambo makuu mawili: Utume na Ushirika Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake kwa Sekretarieti kuu ya Vatican amekazia mambo makuu mawili: Utume na Ushirika   (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV Salam za Noeli Kwa Sekretarieti Kuu ya Vatican: Utume na Ushirika

Papa Leo XIV amekazia mambo makuu mawili: Utume na Ushirika yanayopata chimbuko lake katika Wosia wa Kitume wa Papa Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili.” Kanisa kwa asili linaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwani limepokea zawadi ya Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa; Ujumbe unaosimikwa katika: ukweli, haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican

Nuru ya Noeli ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kugundua upya ambao kutoka katika Pango la Noeli, kielelezo cha unyenyekevu kutoka Bethlehemu na hivyo kupitia historia ya mwanadamu. Waamini wakivutwa na upya huu unaokumbatia kazi yote ya Uumbaji, wote wanatembea katika furaha na matumaini, kwa sababu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu amezaliwa kwa ajili yetu. Rej. Lk 2:11. Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili, akawa mwanadamu, ndugu na anakaa milele kama Mungu pamoja nasi! Haya ni maneno ya mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Sekretarieti kuu ya Vatican, aliyoyatoa Jumatatu tarehe 22 Desemba 2025 kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana heri na baraka katika Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli.Amemkumbuka na kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliyehitimisha hija ya maisha yake hapa duniani, tarehe 21 Aprili na kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu tarehe 26 Aprili 2025. Kwa hakika alikuwa ni sauti ya kinabii, mtindo wa maisha na shughuli zake za kichungaji, amana na utajiri mkubwa wa Mamlaka fundishi ya Kanisa ni kati ya mambo yaliyoacha chapa ya kudumu katika hija ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huruma ya Mungu, mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; mashuhuda wa Injili ya furaha; Ukarimu kwa wote bila kuwasahau maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Hayati Papa Francisko Alifariki dunia 21 Aprili na kuzikwa 26 Aprili 2025
Hayati Papa Francisko Alifariki dunia 21 Aprili na kuzikwa 26 Aprili 2025   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, amekazia mambo makuu mawili: Utume na Ushirika yanayopata chimbuko lake katika Wosia wa Kitume wa Papa Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili.” Kanisa kwa asili linaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwani limepokea zawadi ya Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa; Ujumbe unaosimikwa katika:  ukweli, haki na amani. Waraka wa Furaha ya Injili, unawahamasisha waamini kusonga mbele, katika kuleta mabadiliko ya kimisionari, kwa kukabiliana na changamoto mamboleo za uinjilishaji mpya na kwamba, waamini wote wanaitwa kushiriki kwenye huu umisionari wa kusonga mbele; utume unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kila mtu anayemwamini Kristo Yesu aweze kupata maisha na uzima wa milele. Sherehe za Noeli zinatangaza utume wa Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa Milele, aliyekuja Ulimwenguni, ukaendelezwa na Roho Mtakatifu na katika Kanisa, kigezo muhimu katika maisha ya Kanisa, safari ya imani na huduma ya Kanisa pamoja na utume unaotekelezwa na Sekretarieti kuu ya Vatican, kusaidie kupyaisha miundo mbinu kuwa ni shirikishi na wazi kwa kuendelea kuwa na mwitiko chanya.

Papa Leo XIV: Muhimu: Utume na Ushirika
Papa Leo XIV: Muhimu: Utume na Ushirika   (@VATICAN MEDIA)

Waamini wote kwa njia ya Ubatizo, wanaitwa kushiriki katika utume wa Kristo Yesu na kwamba, Sekretarieti kuu ya Vatican inahamasishwa kutoa huduma ya kichungaji kwa Makanisa mahalia pamoja na viongozi wake! Hii ni Sekretarieti inayojitambulisha kuwa ni ya kimisionari, tayari kuangalia changamoto kubwa za kikanisa, kichungaji na kijamii katika Ulimwengu mamboleo, ili kuhakikisha kwamba, kuna uongozi madhubuti. Utume wa Kanisa kwa namna ya pekee unakumbatia ushirika wake, kama kielelezo cha Fumbo la Umwilisho ambalo kwalo “yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake” 2Kor 5:19. Katika Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu anawafunulia Uso wa Mungu anayewapenda, anayewaokoa na kwamba, kwa njia ya Roho Mtakatifu anawawezesha kuwa ni kielelezo cha ubinadamu mpya unaosimikwa katika upendo na mshikamano. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Wakristo wote ni sehemu ya Kanisa na kwamba, wao ni viungo vya mwili wa Fumbo lake, yaani Kanisa. "In illo Uno Unum" yaani "Ingawa Sisi Wakristo ni Wengi, Katika Kristo Mmoja Sisi ni Wamoja. Kumbe, wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican wanapaswa kuwa ni vyombo na wajenzi ushirika na Kristo Yesu, Kanisa la Kisinodi linalowashirikisha waamini wote kila mtu kadiri ya karama na nafasi yake ndani ya Kanisa, kwa kuendelea kujenga umoja na urafiki; udugu wa kibinadamu; mahali pa toba na wongofu wa ndani, mahali pa kumwilisha upendo unaowawezesha kuwa ndugu wamoja katika Kristo Yesu. Hii ni alama inayopaswa kuonekana hata katika Ulimwengu wa nje “Ad extra” uliojeruhiwa kwa kinzani, vita na mipasuko; athari za ulimwengu wa kidijitali pamoja na siasa. Katika Sherehe ya Noeli, Kristo Yesu anawakirimia waja wake zawadi ya amani, mwaliko kwa waamini kuwa ni alama ya kinabii na kwamba, wafanyakazi wa Sekretarieti kuu wanaitwa na kutumwa kuwa niwafuasi na mashuhuda wa Ufalme wa Mungu, chachu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, changamoto na mwaliko kwa wao kuishi kama ndugu wamoja, ili mwanga wa ushirika uendelee kung’ara sehemu mbalimbali za Ulimwengu.

Papa Leo XIV: Jengeni Urafiki na Udugu wa kibinadamu
Papa Leo XIV: Jengeni Urafiki na Udugu wa kibinadamu   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Utume na Ushirika ni mambo yanayowezekana katika maisha na utume wa Kanisa, ikiwa kama Kristo Yesu atapewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, haya ni matumaini yasiyodanganya kamwe kama kauli mbiu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inavyosikika. Mwaka 2025 umekuwa na matukio makubwa ya kukumbukwa: Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea, yanayowarejesha Wakristo katika mizizi ya imani sanjari na Kumbukizi ya Miaka 70 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambayo kwa kumwangalia Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. Gaudium et spes, 1. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume wa “Evangelii nuntiandi” yaani “Kutangaza Injili” uliochapishwa tarehe 8 Desemba 1975 anasema, Uinjilishaji kwa namna ya pekee ni ushuhuda wa waamini wanaokutana na Kristo Yesu katika medani mbalimbali za maisha yao, tayari kurithisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, maadili na utu wema. Kimsingi ushuhuda ni mchakato wa uinjilishaji wenye nguvu na mashiko. Waraka huu, kwa mwaka 2025 umetimiza miaka 50 tangu uchapishwe, baada ya Mkutano Mkuu wa Tatu wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu. Katika huduma zinazotolewa na Sekretarieti kuu ya Vatican wakumbuke kwamba, kazi ya kila mtu ni muhimu kwa ujumla, na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, unaooneshwa katika ushirika, ni huduma ya kwanza na kuu zaidi wanayoweza kutoa kwa Kanisa. Katika Siri ya Noeli anasema Baba Mtakatifu Leo XIV: "Mungu haoni aibu kwa unyenyekevu wa mwanadamu; anaingia ndani yake. […] Mungu anapenda kile kilichopotea, kinachopuuzwa, kisicho na maana, kilichotengwa, kilicho dhaifu, na kilichovunjika.” Mwenyezi Mungu apende kuwakirimia unyenyekevu huohuo, huruma yake ile ile, upendo wake, ili waweze kuwa ni wanafunzi na mashuhuda wa Kristo Yesu, kila siku ya maisha yao. Mwishoni amewatakia Noeli Njema na kwamba, Mwenyezi Mungu awaletee nuru yake na kuupatia Ulimwengu amani.

Makardinali wakisalimiana na Papa Leo XIV
Makardinali wakisalimiana na Papa Leo XIV   (@VATICAN MEDIA)

Wakati huo huo, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa niaba ya Makardinali, Wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na wafanyakazi wa Mji wa Vatican, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Tangu achaguliwe ameendelea kutekeleza utume wake kwa ari na moyo mkuu; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika maadhimisho mbalimbali na mikutano ambayo imekuwa ni fursa ya kukutana na watu wa Mungu ili kuwasalimia na kuwatia shime. Katika kipindi chote hiki, upatanisho, haki, amani "Isiyo na Silaha na Inayopokonya Silaha” ni kati ya mambo makuu ambayo yamekita katika akili na nyoyo za waamini. Mahujaji kutoka pande mbalimbali za dunia wamekuwa wakiongezeka siku kwa siku, huku wakisali na kuimba, kila mmoja katika lugha yake mwenyewe. Kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kilikuwa ni katika Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana wa Kizazi Kipya kutoka katika nchi 146 bila kusahau vijana waliotoka katika nchi zinazokabiliana na vita kama: Ukraine, Israeli, Palestina, Siria, Iran, Rwanda na Sudan ya Kusini.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali
Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali   (ANSA)

Kardinali Giovanni Battista Re amekumbusha kuhusu hija ya kihistoria ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 ambayo ilinogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu.Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Lebanon kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt. 5:9. Baba Mtakatifu amewataka watu wa Mungu nchini Lebanon kujikita kikamilifu katika kutafuta na kudumisha haki na amani hata katikati ya mtutu wa bunduki na kwamba, hii ni changamoto endelevu dhidi ya: chuki, kiburi, utawala wa mabavu, utengano na uhasama! Aliwataka wawe wajenzi, watangazaji na mashuhuda wa amani! Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea pamoja na kumbukizi ya Miaka 60 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV ameendelea kuwahimiza waamini kuwa ni vyombo na wajenzi umoja na ushirika; haki na amani; wajenzi wa majadiliano katika upendo.

Papa Leo XIV Salam za Noeli 2025
22 Desemba 2025, 15:21