Papa Leo XIV: Wakristo wanaitwa kuwa karibu sana na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu; kwa kugusa mateso na mahangaiko ya binadamu katika Ulimwengu mamboleo. Papa Leo XIV: Wakristo wanaitwa kuwa karibu sana na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu; kwa kugusa mateso na mahangaiko ya binadamu katika Ulimwengu mamboleo.   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Mahubiri Noeli Mchana: Waamini Guseni Madonda Matakatifu ya Yesu

Papa Leo XIV: Watoto wa Mungu, wanatakiwa kuadhimisha wakati huu wa Noeli Injili ya Amani, kwa sababu Noeli kimsingi ni sherehe ya furaha, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kuzaliwa mjini Bethlehemu na kwamba, Fumbo la Umwilisho linafikia kilele chake kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Katika kimya kikuu, Fumbo la Umwilisho ni mwaliko wa kutoa huduma, kuonesha moyo wa ukarimu, huruma na kwamba linahitaji maneno ya faraja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anatufundisha kwamba, Kristo Yesu amezaliwa mnyenyekevu zizini, katika familia maskini. Wachungaji wa kawaida ndiyo mashuhuda wa kwanza wa tukio hili kubwa. Katika umaskini huo, utukufu wa mbinguni ulionekana. Mama Kanisa hachoki kuimba utukufu wa usiku wa Noeli. Rej. KKK 525. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu inayomwajibisha mwanadamu kudumisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu pamoja na kazi ya uumbaji. Kwa njia hii, binadamu anaweza kupata amani ya kweli na inayodumu, lakini amani hii inaweza kutoweka kama ndoto ya mchana ikiwa kama hakuna mahusiano mema na Mwenyezi Mungu na hapa ni mwanzo wa: Vita, kinzani na migogoro ya kijamii.  Amani ni zawadi ambayo ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na imetekelezwa licha ya binadamu kuendelea kuogelea katika dimbwi la dhambi na mauti kwa kumkirimia zawadi ya Ukombozi ambayo maandalizi yake yanajionesha kwa namna ya pekee tangu Agano la Kale na kupata utimilifu wake kwenye Agano Jipya linalojikita katika amani. Hili ni Agano jipya na la milele, agano la amani linalowaelekea watu wote. Hii ni amani inayotolewa na Mwenyezi Mungu kwa wale wote anaowapenda.

Noeli ni Sherehe ya furaha, imani na matumaini
Noeli ni Sherehe ya furaha, imani na matumaini   (ANSA)

Ndiyo maana Nabii Isaya anasema: “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu.” Isa 52:9. Kwa hakika amani ipo na iko kati yao! Hii ni amani ambayo Kristo Yesu aliwakirimia wafuasi wake, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha wanafunzi wake miguu, akawataka wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani na kwamba, hii ni dhamana nyeti na endelevu kwa wote ili waweze kutambua kwamba, wao ni watoto wa Mungu, wanaotakiwa kuadhimisha wakati huu wa Noeli Injili ya Amani, kwa sababu Noeli kimsingi ni sherehe ya furaha, Neno wa Mungu alipotwaa na kukaa kati ya waja wake na kuzaliwa mjini Bethlehemu na kwamba, Fumbo la Umwilisho linafikia kilele chake kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Katika kimya kikuu, Fumbo la Umwilisho ni mwaliko wa kutoa huduma, kuonesha moyo wa ukarimu, huruma na kwamba linahitaji maneno ya faraja.

Agano la Amani linawaelekea watu wote wa Mungu
Agano la Amani linawaelekea watu wote wa Mungu   (@Vatican Media)

Yohane katika Dibaji ya Injili yake anasema: “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.” Yn 1:11. Huu ni ushuhuda kwamba, amani ya Mungu iko kati ya waja wake, zawadi ya Mungu inawashirikisha wote, inahitaji kupokelewa na hivyo kujitoa sadaka, lakini jambo la kushangaza, zawadi hii inakataliwa na watu wanaigeuzia kisogo, changamoto na mwaliko wa kuwa kweli ni watoto wa Mungu, nguvu inayosikika katika kilio cha watoto wadogo, katika udhaifu wa wazee na kimya kikuu cha waathirika wanaotendewa maovu na wale ambao wanafanya maovu haya pengine bila hata ya kutaka kuyatenda. Kimsingi hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwenye Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Noeli mchana tarehe 25 Desemba 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kama wakristo wanaitwa kuwa karibu sana na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu; kwa kugusa mateso na mahangaiko ya binadamu katika Ulimwengu mamboleo. Kristo Yesu anatumaini kwamba, wafuasi wake wataacha kutafuta yale maficho binafsi na yale ya kijumuiya yanayowakinga na msukosuko wa msiba wa kibinadamu na badala yake waingie kwenye uhalisia wa maisha ya jirani zao na hivyo kujua nguvu ya upole. Rej Evangelii gaudium, 270.

Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu
Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, sasa ana uwezo wa kuzungumza na anayo hamu ya kutaka kukutana na waja wake kwani ametengeneza makazi yake kati ya watu wake! Haya ni makazi kama yale ya Ukanda wa Gaza ambayo yanakabiliana na mvua, upepo mkali na baridi ya kutisha. Haya ndiyo mazingira na changamoto wanayokutana nayo wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia; au watu wasio na makazi katika miji mbalimbali! Hawa ndio waathirika wa vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii, hawa ni madonda wazi. Hiki ni kielelezo cha vijana wanaolazimishwa kwenda mstari wa mbele na kupotelea huko vitani. Je, ni kwa kiasi gani mateso na machungu ya jirani zao yanapenya na kugusa undani wa maisha ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema? Ikiwa kama yanapenya na kugusa undani wa maisha ya watu, kwa hakika huo ndio mwanzo wa mchakato wa amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, amani ya Mungu inapata chimbuko lake pale kilio kinaposikilizwa; huzaliwa katikati ya magofu ya vita yanayolilia mshikamano mpya, huchipuka kutokana na ndoto na maono ambayo, kama unabii hugeuza mkondo wa historia. Yote haya yapo kwa sababu Kristo Yesu ndiye “Logos” yaani “Neno” chanzo cha kila kitu: “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.” Yn 1:3. Hii ni siri inayotoa changamoto kubwa ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu iliyojengeka, huku ikifungua macho kwa ulimwengu ambao Neno bado linasikika, “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.” Ebr 1:1-2.

Waamini waguswe na Madonda Matakatifu ya Kkristo Yesu katika jirani zao
Waamini waguswe na Madonda Matakatifu ya Kkristo Yesu katika jirani zao   (@Vatican Media)

Neno la Mungu bado linawaita waamini katika toba na wongofu wa ndani. Neno ambalo ni nuru linaendelea kupambana na giza. Hali hii inafafanua njia ya Neno la Mungu kuwa barabara tambarare, iliyojaa vizuizi. Hadi leo, wajumbe wa kweli wa amani hufuata Neno kwenye njia hii, ambayo hatimaye huifikia mioyo: mioyo isiyotulia, ambayo mara nyingi hutamani kile wanachokipinga. Hivyo, maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho hulitia moyo Kanisa la Kimisionari na hivyo kulisukuma kwenye njia ambazo Neno la Mungu limejikita kwa ajili na wala si kwa ajili ya kutawala, kwani Neno hili linasikika kila sehemu, lakini uwepo wake unahamaisha wema, ufanisi na kwamba, halikiti uwepo wake juu ya ukiritimba. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Noeli mchana anasema. Hi ndiyo njia ya utume inayoelekea kwenye njia nyingine. Katika Mwenyezi Mungu kila neno ni neno linalonenwa, mwaliko kwa waamini kujikita katika majadiliano, kwani hili ni neno ambalo kamwe halifanani. Huu ndiyo upya ambao Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wameukuza na kuustawisha ili kuliwezesha Kanisa kutembea kwa pamoja na binadamu wote bila kujitenga nao. Kinyume chake ni pale Kanisa linapoanza kujitafuta lenyewe. Mwendo wa Fumbo la Umwilisho unajikita katika msukumo wa majadiliano. Amani itaweza kupatikana ikiwa binadamu atasitisha majigambo na kuanza kujikita katika mchakato wa kusikiliza, vinginevyo, wataweza kupiga magoti mbele ya utupu wa wengine. Katika jambo hili hili, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa, Nyota ya Uinjilishaji na Malkia wa Amani. Ndani mwake, kila kitu kinazaliwa upya kutoka kwa nguvu ya ukimya wa maisha yanayokaribishwa na kupokelewa.

Papa Leo XIV Noeli Mchana
25 Desemba 2025, 15:04