Katika Mkesha wa Sherehe ya Noeli, waamini kwa namna ya pekee wanampokea Kristo Yesu kama Kiini cha Injili ya Matumaini yasiyodanganya kamwe. Katika Mkesha wa Sherehe ya Noeli, waamini kwa namna ya pekee wanampokea Kristo Yesu kama Kiini cha Injili ya Matumaini yasiyodanganya kamwe.  

Papa Leo XIV: Maana ya Kesha la Noeli: Yesu Ni Kitovu cha Historia na Ulimwengu!

Waamini wajiandae kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa kwao kwa: Njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa katika Mkesha wa Sherehe ya Noeli, waamini kwa namna ya pekee wanampokea Kristo Yesu kama Kiini cha Injili ya Matumaini yasiyodanganya; wanahimizwa kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu mintarafu uhalisia wa maisha na utume wa kila mwamini. Yesu ni Kitovu cha historia na ulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Tukio la Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, ni ishara muhimu: Inayowakumbusha binadamu kwamba wao ni sehemu ya safari ya ajabu ya ukombozi na kwamba, kamwe si peke yao na, kama Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa alivyosema, "Mungu alifanyika mwanadamu ili mwanadamu apate kuwa Mungu, [...] ili mwanadamu, mwenyeji wa dunia, apate makao mbinguni" (Sermo 371, 1). Huu ni wito wa kusambaza waraka huu sanjari na kudumisha mila hii hai. Waamini watambue kwamba, wao ni zawadi ya nuru kwa ulimwengu, ambao unahitaji sana kuendelea kujikita katika fadhila ya matumaini kwa kuwa na matumaini. Ni katika maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, Baba Mtakatifu Leo XIV katika Kesha la Noeli, tarehe 24 Desemba 2025 anatarajia kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Maana ya Kesha la Noeli: Utukufu wa Mungu ulipowang'aria wachungaji
Maana ya Kesha la Noeli: Utukufu wa Mungu ulipowang'aria wachungaji   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho haya yataanza majira ya Saa 4: 00 Usiku kwa saa za Ulaya, sawa na Saa 6: 00 Usiku kwa Saa za Afrika Mashariki. Kadiri ya Mapokeo ya tangu zamani za kale Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, yaani Noeli ya Bwana yanafanyika Usiku wa manane, ili kuwakumbusha waamini usiku ule mtakatifu utukufu wa Mungu ulipowang’aria wachungaji waliokuwa kondeni: “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” Lk 2: 8-11. Kama sehemu Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Waamini wampokee Kristo Yesu anayezaliwa tena nyoyoni mwao
Waamini wampokee Kristo Yesu anayezaliwa tena nyoyoni mwao   (Vatican Media)

Waamini wanahimizwa kujiandaa kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa kwao kwa: Njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa katika Mkesha wa Sherehe ya Noeli, waamini kwa namna ya pekee wanampokea Kristo Yesu kama Kiini cha Injili ya Matumaini yasiyodanganya kamwe. Hii ni fursa ya kusikiliza, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu mintarafu uhalisia wa maisha na utume wa kila mwamini. Kitabu cha Orodha ya Majina ya Wafiadini wa Roma “Roman Martyrology” kinaonesha kwamba, Siku Nane Kabla ya Maadhimisho ya Mwaka Mpya Kadiri ya “Kalenda ya Januari” yaani tarehe 25 Desemba, Kristo Yesu anazaliwa na Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa hakika Kristo Yesu ni kitovu cha historia na Ulimwengu.

Maana ya Kesha la Noeli
23 Desemba 2025, 14:35