Papa Leo XIV: Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu lijengwe katika umoja yaani: “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja; na Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya wote. Papa Leo XIV: Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu lijengwe katika umoja yaani: “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja; na Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya wote. 

Papa Leo XIV: Kumbukizi ya Miaka 10 ya Mashuhuda wa Imani Perù

Damu ya mashuhuda wa imani ni kielelezo cha sadaka ya upendo wa Yesu kwa waja wake na kwamba, hii ni nguvu ya sadaka ya maisha na umoja unaopata chimbuko lake katika asili, mifumo, mazingira pamoja na sadaka mbalimbali na kwamba, Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu lijengwe katika umoja yaani: “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja; na Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya wote, anayefanya kazi katika yote na aliye ndani ya yote.” Efe 4:5-6.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Zbigniew Strzałkowski, Michał Tomaszek na Alessandro Dordi hawa ndio mashahidi na  watakatifu wapya kutoka nchini Perù. Huu ulikuwa ni utabiri wa kinabii wa Mtakatifu Yohane Paulo II alioutoa tarehe 13 Agosti 1991, akiwa nchini Poland wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ambao ulitimia tarehe 3 Februari  2015, kwa Mama Kanisa kuwatambua kuwa ni Mashahidi Wafranciskani wawili kutoka Poland, na mmoja kutoka nchini Italia waliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Wenyeheri tarehe 5 Desemba 2015, miaka kumi iliyopita. Watawa hawa walisadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake kutokana na chuki za kidini “Odium fidei.” Hawa ni mashuhuda wa imani ambao hata upanga umeshindwa kuwatenganisha na upendo wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, kumkirimia maisha ya uzima wa milele! Ni Mapadre waliokita maisha na utume wao katika maisha ya kijumuiya, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa lakini zaidi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu; walijisadaka bila ya kujibakiza katika sekta ya elimu, malezi, makuzi na katekesi na kila mmisionari akachangia kadiri ya karama na uwezo wake, kwa ajili ya kuwatangazia watu wa Mungu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Huu ni umoja unaopata chimbuko lake, kwa watawa kuungana na Kristo Yesu, kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Injili ya Kristo Yesu na Kanisa na kwa ajili ya ujenzi, ustawi na mafao ya watu wa Mungu. Ushuhuda huu wa imani ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujishikamanisha na matumaini katika utume wa Kristo Yesu.

Ni wamisionari waliojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Ni wamisionari waliojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi   (ANSA)

Damu ya mashuhuda wa imani ni kielelezo cha sadaka ya upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake na kwamba, hii ni nguvu ya sadaka ya maisha na umoja unaopata chimbuko lake katika asili, mifumo, mazingira pamoja na sadaka mbalimbali na kwamba, Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu lijengwe katika umoja yaani: “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja; na Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya wote, anayefanya kazi katika yote na aliye ndani ya yote.” Efe 4:5-6. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 10 tangu Mashahidi na watakatifu wapya kutoka Perù watangazwe kuwa ni wenyeheri. Katika Ulimwengu mamboleo unaokumbana na changamoto mbalimbali, mwaliko ni kurejea na kutoa kipaumbele kwa Kristo Yesu; kwa kuwa waaminifu kwa tunu msingi za Kiinjili na kwamba, Kristo Yesu anapaswa kuwa ni rejea ya maisha ya kila mwamini.

Miaka 10 tangu Mashuhuda wa Imani Chimbote watangazwe kuwa wenyeheri
Miaka 10 tangu Mashuhuda wa Imani Chimbote watangazwe kuwa wenyeheri

Mchakato wa uinjilishaji ni njia maalum ya kutangaza na kufundisha; ni mkondo wa neema na baraka; na nyenzo ya upatanisho kati ya mwamini mdhambi na Mungu Mtakatifu sanjari na kuendeleza sadaka ya Kristo Yesu kwa njia ya Misa Takatifu, kumbukumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wake uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Kumbukizi hii kwa Kanisa na Jimbo Katoliki la Chimbote, nchini Perù ni changamoto na mwaliko wa kupyaisha tena ule utayari wa shughuli za kitume; tayari kumtangaza na kumshuhudia kwa maneno na maisha; kwa kuendelea kuwa waaminifu; kwa kuwahudumia watu wa Mungu kwa unyenyekevu, ili kuwawashia tena moto wa matumaini, hata pale ambapo bado kuna mashaka na ugumu wa maisha. Hata katika shida na changamoto za maisha, historia ya mwanadamu bado inaendelea. Kwa njia ya mashuhuda hawa wa imani, Kristo Yesu anaendelea kutenda ndani ya Kanisa lake na hivyo kuiongoza historia ya Kanisa hadi utimilifu wa Ufalme wa Mungu na kwamba, hata kifo hakina neno la mwisho: “Nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.” Ufu 1:18.

Papa Leo XIV: Vijana changamkieni wito wa upadre na utawa
Papa Leo XIV: Vijana changamkieni wito wa upadre na utawa

Baba Mtakatifu anasema, ushuhuda wa wafiadini na waungama imani kutoka Jimbo Katoliki la Chimbote, nchini Perù unaonesha kwamba, maisha huzaa matunda kwa kujibu kikamilifu katika wito wa Mungu. Vijana hata katika ujana wao wanaweza kuwa ni mashuhuda wa uaminifu; safari ambayo wanaweza kuigundua taratibu. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kutokuogopa kuitikia miito mitakatifu ya: Upadre, Utawa pamoja na kuwatangazia watu wa Mataifa Habari Njema. Mapadre na hasa Mapadre vijana wajitose bila ya kujibakiza kama zawadi ya imani: “fidei donum” kwa kufuata mifano ya maisha bora ya Mashahidi wa Perù kwa kuwahudumia watu wa Mungu pamoja na kuwatuma Mapadre kutangaza Injili ya upendo wa kichungaji kwenye maeneo yenye mahitaji makubwa. Kumbukumbu endelevu ya mashuhuda hawa wa imani,. Isaidie kuangaza mapito ya Kanisa linalosafiri Jimboni Chimbone na kwa ajili ya wale wote wanaotamani kumfuasa na kumwiga Kristo Yesu kwa moyo wa ukarimu na upendo. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka watu wa Mungu Jimboni Chimbote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa mashuhuda na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Mashuhuda wa imani
06 Desemba 2025, 14:42