Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka  (@Vatican Media)

Lango la Jubilei Kanisa Kuu la Laterano Lafungwa: Ushuhuda wa Imani Tendaji

Katika mahubiri yake, ameunganisha Fumbo la Umwilisho, linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Mtume Yohane na Mwinjili anayeunganisha mbio za Maria Madgalena na zile za Mtakatifu Petro. Huyu ni Mtume aliyefuatana na Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akamsikiliza kwa makini na hatimaye, akawa ni rafiki yake wa karibu sana! Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia imani tendaji, matunda ya Jubilei

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum” lilitabarukiwa na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324, na kuwekwa chini ya ulinzi wa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu, baadaye, likawekwa pia chini ya ulinzi wa Yohane Mbatizaji na Mwinjili Yohane. Haya ni matunda ya uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu uliotolewa kwa Wakristo kuabudu kadiri ya dini yao na Mfalme Costantino kunako mwaka 313. Hili lilikuwa ni Kanisa la kwanza kujengwa mjini Roma na baadaye, kuanzia mwaka 1565 Makanisa yakaanza kujengwa sehemu mbalimbali. Kanisa hili ndilo Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma, ambalo, kwa nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV ndiye Askofu wake mkuu. Kumbe, Kanisa hili pia ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dimbwi la dhambi. Kanisa ni moja: lina bwana mmoja, laungama imani moja tu, lazaliwa kwa Ubatizo mmoja, lafanywa mwili mmoja, lahuishwa na Roho mmoja, kwa ajili ya tumaini moja. Rej. Efe 4: 3-5, na katika utimilifu wote migawanyiko yote itashindwa. Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Mungu aliye mtakatifu sana. Kanisa ni Katoliki latangaza utimilifu wa imani. Kanisa ni la kitume kwa sababu limejengwa juu ya misingi imara ya Mitume kumi na wawili. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la Kitume. Rej. KKK 866-870. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anayakumbuka Makanisa mahalia ambamo Jumuiya za waamini zinakusanyika kuadhimisha mafumbo ya Kimungu kwamba uhusiano wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na Makanisa mahalia usaidie kunogesha furaha kwa kila mwamini ili kutembea pamoja katika huduma ya Injili, sala, ushirika na kama mashuhuda na vyombo vya Injili ya: Imani, Upendo na Matumaini. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza mara baada ya kufunga Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.”  

Lango la Jubilei ya Matumaini lafungwa Kanisa kuu la Laterani
Lango la Jubilei ya Matumaini lafungwa Kanisa kuu la Laterani   (@Vatican Media)

Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yameanza kufunga Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Lakini Kristo Yesu ni Lango la Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake, ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Mtoto aliyezaliwa ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu anakuja kuganga na kuponya madonda yanayo mwandama mwanadamu na kwa wale waliovunjika na kupondeka nyoyo wanapata amani na utulivu wa ndani.

Mtakatifu Maria Magdalena ni shuhuda wa kwanza wa ufufuko wa Kristo
Mtakatifu Maria Magdalena ni shuhuda wa kwanza wa ufufuko wa Kristo

Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Jumamosi tarehe 27 Desemba 2025 Sikukuu ya Mtakatifu Yohane Mwinjili, amefunga rasmi Lango la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum.” Katika mahubiri yake, ameunganisha Fumbo la Umwilisho, linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Mtume Yohane na Mwinjili anayeunganisha mbio za Maria Madgalena na zile za Mtakatifu Petro. Huyu ni Mtume aliyefuatana na Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akamsikiliza kwa makini na hatimaye, akawa ni rafiki yake wa karibu sana.Siku ya kwanza ya Juma, asubuhi na mapema, Yesu akamtokea Maria Magdalena na kumshuhudia kuwa ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu, kiasi cha kudondosha chozi la furaha ya Pasaka. Mtakatifu Maria Madgalena alipata heshima ya kuwa ni mfuasi wa kwanza kushuhudia kufufuka kwa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, pale alipokuta kaburi wazi, Yesu Mfufuka akamwonjesha huruma na upendo wake; chemchemi ya maisha mapya. Yesu akamwambia Maria Magdalena “usinishike mimi” “Non me tangere.” Ni Mtakatifu aliyesikia na kupewa dhamana ya kuwapasha ndugu zake Kristo kwamba kweli Kristo Yesu amefufuka kwa wafu! Maria Magdalena akawa kweli shuhuda na mtangazaji wa Ufufuko wa Kristo Yesu kama walivyokuwa Mitume wengine ndiyo maana Mtakatifu Thoma wa Akwino anamwita kuwa ni “Mtume wa Mitume” kwani anatangaza kile ambacho Mitume watapaswa kukitangaza na kukishuhudia hadi miisho ya dunia.

Mahujaji wa Matumaini, Imani na Mapendo
Mahujaji wa Matumaini, Imani na Mapendo   (@Vatican Media)

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini, waamini wengi wamejitaabisha kufunga safari kumtafuta, ili hatimaye, wakutane na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao! Hili ni jicho ambalo liliwatafuta wadhambi, wakoma, maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hii ndiyo changamoto kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, wanaotakiwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili, kwa kuhakikisha kwamba, Injili inapata nafasi katika maisha, sera na mikakati ya maisha yao; waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya huruma na matumaini, kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; kwa kukiri na kumwilisha imani kama kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kusimama kidete kutangaza haki na amani; kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa hakika wanapaswa kuwa ni vyombo vya Injili ili kutangaza: Kile walichoona, wakasikia na kugusa, uwepo angavu wa Kristo Yesu, ili watu wengine pia waweze kukutana na Kristo Yesu. Huu ni ushuhuda unaosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kwamba, unawagusa watu wote wa Mungu na kwamba, kwa hakika wanapaswa kuwa ni wamisionari wa Fumbo la Bwana kugeuka sura, tayari kuwafunulia wengine ile Sura ya Kristo ambaye ameshinda dhambi na kifo. Maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini yanawachia waamini: Sakramenti ya uwepo wa Mungu katika maisha yao; Huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; mambo yanayofumbatwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili: Rej Mt 25: 31-46 na zaidi ya hayo kuwapenda hata wale wanaodhani kuwa ni adui zao.

Mwaliko sasa ni ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Mwaliko sasa ni ujenzi wa Kanisa la Kisinodi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Waamini wa Jimbo kuu la Roma wanaalikwa kuunganisha sala na nguvu zao, kama ushuhuda wa ujirani mwema, kama afanyavyo Mchungaji Mwema, pasi ya kumsahau mtu awaye yote. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuwajibika katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, sanjari na kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wawe ni Manabii na vyombo vya huruma ya Mungu kwa maskini wa hali na mali; maskini wa kiuchumi, kimaadili ni kihali, huku wakiendelea kutoa dir ana mwongozo bora wa maisha ya vijana. Katika utekelezaji wa awamu hii mpya baada ya kufunga Maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini, Mtume Yohane na Mwinjili na Bikira Maria Mama wa Matumaini wawaombee, ili waunganishe Neno la Mungu pamoja na maneno yao, ili kwa pamoja waweze kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” kwani kwa hakika, Mwenyezi Mungu ametenda makuu katika maisha yao.

Lango la Jubilei
27 Desemba 2025, 17:46