Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Jumamosi tarehe 6 Desemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu: “Kutumaini ni kushiriki: Alberto Marvelli.” Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Jumamosi tarehe 6 Desemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu: “Kutumaini ni kushiriki: Alberto Marvelli.”   (ANSA)

Katekesi Kuhusu Mwaka wa Jubilei: Kutumaini Ni Kushiriki: Alberto Marvelli

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Jumamosi tarehe 6 Desemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu: “Kutumaini ni kushiriki: Alberto Marvelli.” Katekesi hii imeongozwa na sehemu ya Neno la Mungu isemayo: “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Ikiwezekana, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Papa Leo XIV amegusia pia wahusika wa Kipindi cha Majilio na Umuhimu wake katika utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Jumamosi tarehe 6 Desemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu: “Kutumaini ni kushiriki: Alberto Marvelli.” Katekesi hii imeongozwa na sehemu ya Neno la Mungu isemayo: “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Ikiwezekana, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.” Rum 12:17-19. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kipindi cha Majilio kinawafunza waamini kusoma alama za nyakati, kwa kuwakumbusha ujio wa kwanza wa Kristo Yesu, Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi, ili kumjifunza, kila mara anapokuja miongoni mwa waja wake na hatimaye, kuwaandaa kwa ujio wa pili, atakapokuja kuwahukumu wazi na wafu na kwamba, Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Kristo Yesu atakuwa pamoja na waja wake pamoja na viumbe wote, ili kutengeneza uumbaji mpya. Ikumbukwe kwamba, Sherehe za Noeli ni funuo wa Mwenyezi Mungu anayeshiriki kikamilifu katika maisha ya waja wake. Na kwa njia ya Kipindi cha Majilio, Mama Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake na hivyo waamini huweza kuchota na kujazwa na neema ya wokovu.

Kipindi cha Majilio ni nafasi kwa waamini kusoma alama za nyakati
Kipindi cha Majilio ni nafasi kwa waamini kusoma alama za nyakati   (@Vatican Media)

Mama Kanisa katika huruma na upendo wake wa daima anapenda kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Mafundisho, Sala pamoja na matendo ya toba na huruma. Rej. Sacrosanctum concilium, 102-111. Kipindi cha Majilio: “Kwa kuadhimisha kila mwaka liturujia ya majilio, Kanisa linahuisha kule kumngojea Masiha, likijiweka katika ushirika wa maandalizi marefu ya ujio wa kwanza wa mwokozi, waamini wakipyaisha tamaa ya ujio wake wa pili.” (KKK 524). Kumbe, Majilio ni kipindi cha upendo, matumaini, furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wahusika wakuu katika Kipindi hiki cha Majilio ni: Nabii Isaya, Yohane Mbatizaji, Zakaria na mkewe Elizabeti, Mzee Simeoni Wengine wanaopamba kipindi hiki ni: Wachungaji wa kondeni, Mamajusi, watu wa kawaida lakini kwa namna ya pekee, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu mifano bora ya kuigwa katika kipindi hiki cha Majilio! Hawa ni watu walioguswa kwa namna ya pekee na maandalizi ya ujio wa Masiha. Bwana wetu Yesu Kristo ndiye nguzo kuu ya tafakari katika kipindi hiki na kwamba, wote wanaitwa kushiriki kikamilifu katika ndoto ya Mungu, ili wote waweze kuwa ni “Mahujaji wa matumaini” kwani hii ni programu ya maisha, inayowawezesha watu wa Mungu kutembea, kungojea, huku wakishiriki kikamilifu katika mpango huu.

Kutumaini ni Kushiriki: Alberto Marvelli
Kutumaini ni Kushiriki: Alberto Marvelli   (ANSA)

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitahidi kusoma alama za nyakati, kwa kuwashirikisha watu wote wa Mungu. Hizi ni alama za ujio wa Mwenyezi Mungu katika Ufalme wake, katika historia na maisha ya watu na kwamba, huyu ni Imanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Mt 1:23. Waamini wanaitwa na kuhamasishwa kumtafuta Mungu katika uhalisia wa maisha, kwa kutumia akili na nyoyo na kwamba, hii ni dhamana na utume wanasema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa ajili ya waamini walei, kwani Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anakuja kila siku katika uhalisia wa maisha ya watu: katika shida na magumu ya maisha na hata katika wema wa Ulimwengu. Kristo Yesu anawasubiri na kuwashirikisha katika maisha na utume wake, ndiyo maana kutumaini ni kushiriki kikamilifu.Baba Mtakatifu Leo XIV katika Katekesi yake, amemkumbuka na kumtaja kijana Alberto Marvelli, kutoka nchini Italia, aliyeishi katika nusu ya kwanza ya karne iliyopita. Ni kijana aliyelelewa katika familia kulingana na Injili, aliyefunzwa katika utendaji wa kikatoliki, akahitimu katika Uhandisi na kuingia katika maisha ya kijamii wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambavyo aliilaani vikali. Huko mjini Rimini na na viunga vyake alijitolea kwa moyo wote kusaidia waliojeruhiwa, wagonjwa, na wahamiaji. Wengi walifurahia kujitolea kwake bila ya kujibakiza, na baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, alichaguliwa kuwa diwani na kuwekwa kuwa ni msimamizi wa Tume ya Nyumba na Ujenzi wa makazi mpya. Kwa hivyo, aliingia katika maisha ya kisiasa, lakini siku moja alipokuwa akiendesha baiskeli kwenda kwenye mkutano, aligongwa na lori la kijeshi. Alikuwa na umri wa miaka 28. Alberto akaonesha kwamba kutumaini ni kushiriki, na kwamba kutumikia Ufalme wa Mungu huleta shangwe na furaha kubwa hata katikati ya hatari kubwa.

Kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani
Kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Ulimwengu unakuwa bora ikiwa kama watu wanapoteza usalama kidogo na hivyo kuwa na utulivu wa kuchagua mema. Hivi ndivyo ushiriki ulivyo. Hebu tujiulize: Je, ninashiriki katika mpango fulani mzuri unaopyaisha vipaji vyangu? Je, nina upeo wa macho na pumzi ya Ufalme wa Mungu ninapotoa huduma fulani? Au mimi hufanya hivyo kwa kunung'unika, nikilalamika kwamba kila kitu kinakwenda vibaya? Tabasamu kwenye midomo yetu ni ishara ya neema iliyoko ndani mwetu anasema Baba Mtakatifu Leo XIV. Kwa hakika: Kutumaini ni kushiriki: hii ni zawadi kutoka kwa Mungu kwetu. Hakuna anayeokoa ulimwengu peke yake. Na hata Mungu hataki kuuokoa peke yake: Angeweza, lakini hataki, kwa sababu kwa pamoja ni bora zaidi. Kushiriki huturuhusu kueleza na kufanya zaidi yetu wenyewe kile ambacho hatimaye, tutatafakari milele, Kristo Yesu atakaporudi kuwahukumu wazima na wafu.

Katekesi Jubilei
06 Desemba 2025, 15:25