Mtakatifu Yohane Paulo II: “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Mtakatifu Yohane Paulo II: “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”  

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Mlinzi na Mwombezi wa Tanzania!

Ilikuwa ni tarehe 8 Novemba 1984, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka unaojulikana kama “Tot tantaeque” yaani “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" Sherehe inayoadhimishwa kitaifa kila mwaka ifikapo tarehe 9 Desemba. Katika mkesha wa uhuru wa Tanganyika, Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanganyika, ili uhuru wake uweze kuwanufaisha watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake mintarafu Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 ya Ukristo, Jumamosi tarehe 6 Desemba 2025 amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kupyaisha ndani mwao tajiriba ya imani, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini katika familia na jamii katika ujumla wake. Katika kipindi hiki cha Majilio, wamwinulie nyuso zao, Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili, aliyejitahidi katika maisha yake, kutekeleza mapenzi ya Mungu. Tajiriba ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, yawe ni chemchemi ya furaha, haki na amani. Waamini wamwombe Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, ili hatimaye, waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani.

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni Mlinzi na Mwombezi wa Tanzania
Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni Mlinzi na Mwombezi wa Tanzania

Ilikuwa ni tarehe 8 Novemba 1984, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka unaojulikana kama “Tot tantaeque” yaani “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” “Ioannes Paulus. Li Litterae Apostolicae Tot Tantaeque Beata Virgo Immaculata Patrona Confirmatur Rei Publicae Tanzaniensis.” Hili ni ombi lililotolewa kwa wakati huo na Askofu Anthony Petro Mayalla wa Jimbo Katoliki la Musoma, ambaye alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, kuomba ili Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili aweze kuwa ni Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia familia ya Mungu nafasi ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya uhuru, siku moja tu, baada ya kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili Tanzania inaadhimishwa 9, Des.
Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili Tanzania inaadhimishwa 9, Des.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka huu wa Kitume, anasema hapa duniani kuna matatizo na magumu mengi yanayowakabili wafuasi wa Kristo Yesu. Kumbe, wanatafuta ulinzi si tu katika hekima ya binadamu, kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hata pia kutoka kwa Bikira Maria, anayewapenda na kulinda watoto wake. Kumbe, Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia ombi la kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kama Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili awakirimie watu wa Mungu nchini Tanzania fadhila ya upendo. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mkutano wake mkuu wa mwaka uliofanyika Juni 2016 liliamua kwamba, kuanzia sasa Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili itakuwa inaadhimishwa kitaifa nchini Tanzania ifikapo tarehe 9 Desemba. Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa katika barua yake kwa ajili ya tukio hili alisema kwamba, uamuzi huu ni utekelezaji wa zawadi iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1984 kwa kuiweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Kumbe, kwa mara ya kwanza, katika historia ya Tanzania, Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili kitaifa nchini Tanzania iliadhimishwa rasmi tarehe 9 Desemba 2016. Hii ni nafasi ya kuombea familia ya Mungu nchini Tanzania ili iweze kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, nguzo msingi ambazo daima zimewatambulisha watanzania katika Jumuiya ya Kimataifa.

Mt. Yohane Paulo II 8 Novemba 1984 akaiweka Tanzania nchini ya Ulinzi wa B. Maria
Mt. Yohane Paulo II 8 Novemba 1984 akaiweka Tanzania nchini ya Ulinzi wa B. Maria

Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanganyika kunako mwaka 1961, Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanganyika ili uhuru wake uwawezeshe watanganyika kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwaombea Watanganyika paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu. Mtakatifu Yohane XXIII aliwaombea watanganyika upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila na utaifa ili watanzania wote waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanganyika na majirani zake; pamoja na viongozi wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni milele na milele, Amina.

Bikira Maria na Tanzania
06 Desemba 2025, 15:59