2019.05.14 Robotica  e Intelligenza artificiale - Conferenza organizzata dall' Accademia Pontificia delle Scienze

Papa Leo XIV,Jukwaa la Wajenzi wa AI:Kanisa linawaita wajenzi wa AI kukuza utambuzi wa maadili

Katika ujumbe kwa washiriki katika Jukwaa la “Wajenzi wa AI" katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian,Papa Leo XIV anatafakari kuhusu mzigo wa kimaadili na kiroho unaoambatana na teknolojia mpya huku akikumbusha kwamba kila chaguo la muundo linaonesha maono ya ubinadamu.Katika hilo anarudia kutoa mwaliko wa kuhoji jinsi ambavyo zana tunazojenga zinavyobadilisha wanadamu na kwamba:“Maendeleo ya Akili Unde hayapaswi kuzuiliwa kwenye maabara na uwekezaji.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kwa Washiriki katika Jukwaa la “Wajenzi wa AI” kwa mwaka 2025 linaloendelea katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriana, Papa Leo XIV alituma ujumbe wake huku akiwashukuru waandaaji na wote ambao, kupitia utafiti, ujasiriamali na maono ya kichungaji, wanatafuta kuhakikisha kwamba teknolojia zinazoibuka zinabaki zikilenga heshima ya mwanadamu na manufaa ya wote.

Lengo la Jukwaa kukuza Jumuiya ya utendaji

Papa leo alisema kuwa “Lengo la Jukwaa hili la kukuza "jumuiya mpya ya utendaji ya taaluma mbalimbali iliyojitolea kusaidia maendeleo ya bidhaa za AI zinazohudumia dhamira ya Kanisa" linaonesha suala muhimu la wakati wetu: si tu kile ambacho Akili Unde(AI) inaweza kufanya, bali ni wakina nani tunakuwa kupitia teknolojia tunazojenga. Katika suala hili, Baba Mtakatifu alipenda “kutambua kwamba akili unde, kama uvumbuzi wote wa binadamu, hutokana na uwezo wa ubunifu ambao Mungu ametukabidhi(Antiqua et Nova, 37). Hii ina maana kwamba uvumbuzi wa kiteknolojia unaweza kuwa aina ya ushiriki katika tendo la uumbaji la kimungu. Kwa hivyo, una uzito wa kimaadili na kiroho, kwani kila chaguo la muundo linaonesha maono ya ubinadamu.

Kanisa linawaita wajenzi wa AI kukuza utambuzi wa maadili

Kwa hivyo Kanisa linawaita wajenzi wote wa Akili Unde(AI) kukuza utambuzi wa maadili kama sehemu ya msingi ya kazi yao - kukuza mifumo inayoakisi haki, mshikamano, na heshima ya kweli kwa maisha. Majadiliano yao katika siku hizi mbili yanaonesha kwamba kazi hii haiwezi kuzuiliwa kwa maabara za utafiti au kwingineko za uwekezaji. Lazima iwe ni juhudi kubwa ya kikanisa.” Papa alisisitiza kwamba “ Iwe ni kubuni mfumo wa mashine za elimu ya Kikatoliki, zana za huduma ya afya yenye huruma, au majukwaa ya ubunifu yanayosimulia historia ya Kikristo kiukweli na uzuri, kila mshiriki huchangia katika dhamira ya pamoja: kuweka teknolojia katika huduma ya uinjilishaji na maendeleo fungamani ya kila mtu.

Akili Unde au ya kibinadamu katika ushirikiano inapata maana katika upendo

Ushirikiano kama huo wa taaluma mbalimbali Papa aliongeza "unawakilisha mazungumzo kati ya imani na sababu," (Antiqua et Nova, 83) iliyofanywa upya katika enzi ya kidijitali na kuthibitisha kwamba iwe akili unde  au ya kibinadamu,  inapata maana yake kamili katika upendo, uhuru na uhusiano na Mungu.” Kwa kuhitimisha, Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kuwa kwa hisia hizo anawakabidhi kazi ya Jukwaa hilo kwa maombezi ya upendo ya Maria, Kikao cha Hekima. Ushirikiano wenu na uzae matunda katika Akili Unde (AI) inayoakisi muundo wa Muumba: wenye akili, uhusiano na kuongozwa na upendo. Bwana abariki juhudi zenu na kuzifanya kuwa ishara ya matumaini kwa familia nzima ya wanadamu.”

07 Novemba 2025, 11:28