Papa Leo XIV amteua Monsinyo Ekpo kuwa Mtathmini mpya wa Vatican
Na Salvatore Cernuzio – Vatican.
Ni Kijana mwenye asili ya Nigeria. Kufuatia uteuzi wa hivi karibuni wa Padre Edward Daniang Daleng, Mwanashirika wa Shirika la Mtakatifu Agostino,O.S.A., kuwa Makamu Mkuu mpya wa Nyumba ya Kipapa, Baba Mtakatifu Leo XIV amemteua Padre mwingine kutoka Bara la Afrika kuwa katika nafasi muhimu ya Curia Romana(Baraza la Wawakilishi la Roma): Monsinyo Anthony Onyemuche Ekpo, tarehe 19 Novemba 2025, kuwa Mtathmini mpya wa Masuala ya Jumla ya Sekretarieti ya Vatican, sehemu ambayo alikuwa amehudumu karibu miaka sita kabla ya Papa Francisko kumteua kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu.
![]()
Kardinali Parolin akimsalimia na kumkabidhi barua Mtathimini mpya wa Vatican.
Hadi uteuzi alikuwa Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu
Padre huyo alizaliwa Umudike nchini Nigeria, mnamo 1981, na kupewa daraja la Upadre mwaka 2011 na kuteuliwa kuwa Msimamizi wa Kikanisa cha Baba Mtakatifu mnamo Machi 2023. Mafunzo yake ni kwamba alipata Shahada ya Uzamivu katika Taalimungu ya Kimfumo kutoka Chuo Kikuu Katoliki cha Australia mnamo 2013, na Shahada ya Uzamivu katika Sheria ya Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Gregorian Roma mnamo 2021. Alijiung katika huduma ya Vatican kama Afisa wa Kitengo cha Masuala ya Jumla mnamo tarehe 5 Septemba 2016. Mnamo Aprili 2023, aliteuliwa kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu, akisaidiana katika kazi ya Mwenyekiti wa Baraza la kipapa hilo, Kardinali Michael Czerny, pamoja na Katibu Mkuu Sr Alessandra Smerilli, na katibu mwingine msaidizi, Kardinali Fabio Baggio.
"Hamu yangu ni kuweza kushirikiana na wakubwa na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa ili kuendeleza maono ya Baraza la Kipapa na utume wa Kanisa." Ekpo alisema hayo wakati huo katika siku ya uteuzi wake, akiwaaga viongozi na wafanyakazi wenzake, ambao aliwashukuru "kwa urafiki wao na kazi yao ya pamoja katika miaka hii," na akaomba kwamba Mungu ampatie "neema ya kutekeleza, kwa furaha, shauku, na kujitolea" huduma yake kwa Kanisa.
Monsinyo Ekpo anamrithi Monsinyo Roberto Campisi, aliyeteuliwa kunako tarehe 27 Septemba 2025 kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwa UNESCO, akiwa na jukumu la pia kusimamia shughuli za Mashirika ya Kikatoliki ya Kimataifa. Kwa njia hiyo Mtathmini mpya anazungumza lugha nne: mbali na Kiingereza, Kiitaliano, na Kifaransa, pia anazungumza Igbo, lugha ya asili ya nchi yake.
![]()
Wakati wa kuwatangaza viongozi wapya katika Maktaba ya Katibu Mkuu wa Vatican.
Katibu Mpya Msaidizi wa Kitengo cha Mahusiano na Mataifa
Wakati huo huo, Ofisi ya Habari ya Vatican ilitangaza uteuzi mwingine katika Sekretarieti ya Vatican: ile ya wa Monsinyo Mihăiţă Blaj kuwa Katibu Mpya Msaidizi wa Vatican katika Kitengo cha Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa.
Wasifu wake
Mromania aliyezaliwa Gherăeşti mnamo 1978, Monsi Mihăiţă Blaj, hapo awali alikuwa Mshauri wa Ubalozi huku akihudumu katika Kitengo hicho hicho. Alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 29 Juni 2004; akapewa kwa ajili ya Jimbo la Iaşi, Romania; mhitimu wa Taalimungu; alijiunga katika Huduma ya Kidiplomasia ya Vatican mnamo tarehe 1 Julai 2012, na alitumwa katika Ubalozi wa Vatican huko Ecuador, kama Mshirika; akahamishiwa Ubalozi wa Vatican huko Georgia mnamo tarehe 1 Julai 2015; akahamishiwa tena Ubalozi wa Vatican huko Chad mnamo tarehe 5 Januari 2019; Alihamishiwa kwenye Kitengo cha Sekretarieti ya Vatican cha Mahusiano Nchi na Mashirika ya Kimataifa mnamo tarehe 4 Januari 2022. Anazungumza Kiitaliano, Kifaransa, Kiingereza, Kihispania, na Kijerumani
![]()
Kardinali Parolin Katibu wa Vatican akumkabidhi Mons. Blaj, Katibu Mpya Msaidizi wa Kitengo cha Mahusiano na Nchi na Mashirika ya Kimataifa.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here
