2025.11.06 Papa akutana na Bwana Mahmoud Abbas, Rais wa Nchi ya Palestina. 2025.11.06 Papa akutana na Bwana Mahmoud Abbas, Rais wa Nchi ya Palestina.  (@Vatican Media)

Papa akutana na rais wa Palestina:dharura ya kukomesha mzozo Gaza

Alhamisi Novemba 6,Papa Leo XIV alikutana na Rais wa Palestina Bwana Mahmoud Abbas.Kati ya mazungumozo yao walijadili hitaji la dharura la kukomesha mzozo huko Gaza na kuingia kwa misaada ya kibinadamu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, alhamisi tarehe 6 Novemba 2025 alikutana na Mahmoud Abbas, Rais wa Nchi ya  Palestina, na kujadili "hitaji la dharura la kutoa msaada kwa raia huko Gaza".

Mazungumzo hayo, yaliyofanyika mjini Vatican, yalikuwa ya  mkutano wa kwanza kati yao ambao hapo awali walikuwa wamezungumza kwa simu pekee mnamo Juali iliyopita. Katika taarifa kutoka Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican  ilielezea mkutano huo kama "wa kirafiki", ikiongeza kuwa miongoni mwa mada zilizojadiliwa pia ni hitaji la dharura la "kumaliza mgogoro kwa kutafuta suluhisho la Mataifa mawili."

Papa na Abbas
Papa na Abbas   (@Vatican Media)

Siku moja kabla ya mkutano wake na Papa Leo Leo XIV, Rais Abbas alikuwa ametembelea Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu kutoa heshima zake kwenye kaburi la Papa Francisko.

Ziara hiyo ilikuwa hatua yake ya kwanza alipofika Roma Jumatano alasiri tarehe 5 Novemba 2025. Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri kwenye ngazi za Kanisa, Rais Abbas alisema: "Nilikuja kumuona Papa Francisko kwa sababu siwezi kusahau alichofanya kwa ajili ya Palestina na kwa ajili ya watu wa Palestina, na siwezi kusahau kwamba aliitambua Palestina bila mtu yeyote kulazimika kumwomba afanye hivyo."

Ziara ya Rais Abbas kwenye kaburi la Papa  Francisko, ambapo aliambatana na Padre wa Misri, Mfransiskani  Ibrahim Faltas, aliyekuwa Padre Msimamisi wa Nchi Takatifu uliodumu kwa takriban dakika kumi na tano. Rais aliweka shada la maua kwenye kaburi rahisi la marumaru, ambalo lina maandishi ya ‘Franciscus.’

Rais Abbas na Papa Francisko
Rais Abbas na Papa Francisko   (@Vatican Media)

Ziara ya Rais Abbas Jijini Vatican pia iliadhimisha miaka 10 ya kusainiwa kwa 'Mkataba Kamili kati ya Vatican na Palestina'. Maandishi hayo, yaliyosainiwa tarehe 26 Juni 2015, yanaelezea kujitolea kwa pande zote mbili kwa kujitawala kwa Palestina na suluhisho la nchi mbili. Pia inasisitiza umuhimu wa mfano na kiroho wa Yerusalemu kwa Wayahudi, Wakristo, na Waislamu vile vile.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

06 Novemba 2025, 15:57