Tarehe 19 Oktoba 2008 walitangazwa kuwa ni Wenyeheri na mwaka 2015 Kanisa limewatangaza kuwa watakatifu kwa kuzingatia walivyoishi na kuwalea watoto wao: kiimani, utu wema na katika maadili ya kikiristo. Tarehe 19 Oktoba 2008 walitangazwa kuwa ni Wenyeheri na mwaka 2015 Kanisa limewatangaza kuwa watakatifu kwa kuzingatia walivyoishi na kuwalea watoto wao: kiimani, utu wema na katika maadili ya kikiristo.   (ANSA)

Papa Leo XIV: Utakatifu, Ukuu na Ukweli wa Ndoa na Familia

Imegota miaka kumi, tangu familia ya Mzee Luigi Martin na Zeria Guerin, Wazazi wake Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu watangazwe kuwa ni watakatifu, kioo cha utakatifu na mashuhuda wa utakatifu wa wanandoa, Papa Leo XIV amemwandia ujumbe Askofu Bruno Feillet, ili kuwapongeza Wazazi wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, wanandoa wa kwanza katika historia ya Kanisa kutangazwa kwa pamoja kuwa ni watakatifu, kielelezo cha hija ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utakatifu ni wito kwa watu wote wa Mungu. Ili kufikia azma hii, waamini wanapaswa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao Matunda ya Roho Mtakatifu. Huu ni mchakato wa utakatifu unaosimikwa katika maisha ya kila mmoja, kwa kutumia karama na mapaji aliyokirimiwa na Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu watakatifu wa Mungu. Mababa wa Kanisa wanasema, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu
Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu   (Joachim Schäfer - Ökumenisches Heiligenlexikon)

Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa alishuhudia utakatifu wa maisha kwa moyo wa unyenyekevu. Huyu ni kati ya watakatifu wachache wanaozungumzia na kushuhudia neema ya Mungu na jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anawalinda na kuwatunza watoto wake; anawashika mkono na kuwaongoza polepole kuupanda mlima wa maisha. Theresia wa Mtoto Yesu alizaliwa tarehe 2 Januari 1873 Alencon na baadae kuhamia Lisieux nchini Ufaransa.  Theresia ni mtoto wa tisa kuzaliwa na kitinda mimba kwenye familia ya Mzee Luigi Martin na Zeria Guerin ambao sasa Kanisa limewaweka kuwa mfano na kioo kwa familia zote za Kikristo na Mashuhuda wa utakatifu wa wanandoa. Tarehe 19 Oktoba 2008 walitangazwa kuwa ni Wenyeheri na mwaka 2015 Kanisa limewatangaza kuwa watakatifu kwa kuzingatia walivyoishi na kuwalea watoto wao: kiimani, utu wema na katika maadili ya kikiristo. Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu aliaga dunia tarehe 30 Septemba 1897, akatangazwa Mtakatifu mwaka 1925, mnamo mwaka 1927 Papa Pio XI akamtangaza kuwa ni msimamizi wa utume wa Kanisa.

Miaka 10 tangu wazazi wa Mt. Theresa wa Mtoto Yesu wawe watakatifu
Miaka 10 tangu wazazi wa Mt. Theresa wa Mtoto Yesu wawe watakatifu

Kila mwaka ifikapo tarehe 1 Oktoba, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu; Bikira na Mwalimu wa Kanisa na tangu mwaka 1927 aliteuliwa kuwa ni msimamizi wa wamisionari wote duniani pamoja na Mtakatifu Francisko Xsaveri. Ni katika muktadha wa kumbukumbu ya Miaka kumi, tangu familia ya Mzee Luigi Martin na Zeria Guerin, Wazazi wake Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu watangazwe kuwa ni watakatifu, kioo cha utakatifu na mashuhuda wa utakatifu wa wanandoa, Baba Mtakatifu Leo XIV amemwandia ujumbe Askofu Bruno Feillet wa Jimbo Katoliki la Sèèz, ili kuwapongeza Wazazi wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, wanandoa wa kwanza katika historia ya Kanisa kutangazwa kwa pamoja kuwa ni watakatifu, kielelezo kwamba, kwa hakika maisha ya ndoa na familia ni hija ya utakatifu wa maisha licha ya “patashika nguo kuchanika.” Huu ni mwanga angavu, kioo cha wema na ukarimu, ambao waliamua kuyasadaka maisha yao yote kwa Mwenyezi Mungu na Kanisa, huku wakiendelea kujikita katika uaminifu katika raha na taabu, katika magonjwa na afya, kusudi wapendane na kuheshimiana siku zote za maisha yao!

Waleeni watoto wenu: kiimani, utu wema na maadili ya Kikristo
Waleeni watoto wenu: kiimani, utu wema na maadili ya Kikristo   (@Vatican Media)

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV katika kumbukizi ya Miaka kumi tangu wanandoa hawa watangazwe kuwa ni watakatifu, inakuwa ni fursa kwa waamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya watakatifu Luigi Martin na Zeria Guerin, Wazazi wake Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Ni wanandoa waliosimama kidete katika malezi na makuzi ya watoto wao, mfano bora wa kuigwa katika uhalisia wa maisha yao. Ni wanandoa walioshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa Parokiani, wakatekeleza kwa ari na moyo mkuu huduma yao ya kitaalamu kiasi cha kujipatia tajiriba ya maisha ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, katika hali ya mazingira walimoishi, huku wakimpatia Mungu kipaumbele cha kwanza. Huu ndio mfano bora wa kuigwa unaotolewa na Mama Kanisa, mintarafu udumifu katika imani; malezi na makuzi ya tunu msingi za kikristo; upendo kwa Mungu na jirani; haki jamii na wadumifu katika changamoto katika magumu na katika raha; dhidi ya watu wanaokumbatia utamaduni wa kifo.

Watakatifu hawa ni kioo cha utakatifu na mashuhuda wa utakatifu wa ndoa
Watakatifu hawa ni kioo cha utakatifu na mashuhuda wa utakatifu wa ndoa   (@Vatican Media)

Hawa ni wanandoa waliobahatika kusimika maisha yao katika Injili ya furaha, kiasi cha kujizatiti katika mchakato wa kusadaka maisha yao, ili kurithisha zawadi ya imani kwa watoto wao, ambao leo hii wamekuwa pia watakatifu. Kwa hakika kumbukizi hii ni chemchemi ya matumaini kwa wazazi hawa wawili. Kumbukizi hii ni chemchemi ya furaha, imani na maisha sala. Hata katika shida, mahangaiko na changamoto za maisha, kwao Msalaba wa Kristo Yesu, ulikuwa ni chemchemi ya matumaini na kielelezo cha utukufu wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika wanandoa kudumu katika ujasiri, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo mwanana wa Kristo Yesu kati ya familia yao, katika sera na mipango yao. Wawasaidie watoto wao kuonja upendo, wema na huruma ya Mungu. Wasaidie watoto wao kupenda na kutekeleza mapenzi ya Mungu kati yao kama jinsi wao walivyowapenda Kristo Yesu, Maria na Yosefu. Wawe na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia mafundisho jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha yao! Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka wanandoa wote chini ya ulinzi na tunza ya watakatifu Luigi Martin na Zeria Guerin, Wazazi wake Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, huku akiwaombea neema na baraka kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Familia Takatifu.

Utakatifu na Ukuu wa Ndoa
23 Oktoba 2025, 16:49