Papa kwa Balozi mpya wa Iraq:Umeitwa kulinda mbegu za matumaini na kuhimiza kuishi amani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV aliongoza Ibada ya Misa Takatifu jioni ya Dominika tarehe 26 Oktoba 2025 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kumweka wakfu wa Kiaskofu, Askofu Mkuu Mirosław Stanisław Wachowski,ambaye kwa sasa ni Balozi mpya wa Vatican nchini Iraq. Kabla ya kuteuliwa kwake alikuwa ni Afisa katika kitengo cha Sekretarieti ya Vatican kwa Masula ya Mahusiano na nchi na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu akianza mahubiri yake alisema “Leo, Kanisa la Roma linafurahi pamoja na Kanisa la Ulimwengu wote, zawadi ya Askofu mpya: Askofu Mkuu Mirosław Stanisław Wachowski, mwana wa nchi ya Poland, Askofu Mkuu mteule wa Villamagna wa Proconsolare na Balozi wa Kitume kwa watu wapendwa wa Iraq.
Papa aliendelea, Kauli mbiu aliyochagua ya Gloria Deo Pax Hominibus, inasikika kama mwangwi wa nyimbo za Malaika, za Noeli huko Bethlehemu: "Utukufu kwa Mungu juu, na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema" (Lk 2:14). Ni mpango wa maisha yote: kutafuta kila wakati utukufu wa Mungu ung'ae kwa amani miongoni mwa watu. Hii ndiyo maana ya kina, ya kila wito wa Kikristo, na hasa wito wa kiaskofu: kuonesha, kupitia maisha ya mtu, sifa ya Mungu na shauku yake ya kupatanisha Ulimwengu na nafsi yake (taz. 2 Kor 5:19).
Neno la Mungu lililosomwa, linatupatia sifa muhimu za huduma ya kiaskofu. Katika Injili (Lk 18:9-14) inatuonesha wanaume wawili wakisali hekaluni: Farisayo na mtoza ushuru. Wa kwanza anajitambulisha kwa ujasiri, akiorodhesha matendo yake mwenyewe; na wa pili anabaki nyuma, hakuthubutu kuinua macho yake, na anakabidhi kila kitu kwa ombi moja: "Ee Mungu, unirehemu mimi mwenye dhambi" (rej. Lk 18, 13). Yesu anasema kwamba kiukweli ni yeye, mtoza ushuru, anayepokea neema na wokovu wa Mungu, kwa sababu "kila mtu ajikwezaye atanyenyekezwa, lakini yeye ajinyenyekezaye atainuliwa.” Sala ya maskini inapenya mawingu, Siraki anatukumbusha: “Mungu husikia maombi ya wale wanaojiaminisha kwake kabisa” (taz Sir 35:15-22).
Papa amesisitiza kwamba “Hili ni fundisho la kwanza kwa kila Askofu: unyenyekevu. Sio unyenyekevu wa maneno, bali ule unaokaa moyoni mwa mtu anayejua kuwa ni mtumishi, si bwana; mchungaji, na si mmiliki wa kundi. Katika hilo, Papa alipenda kuelezeze anavyo vutiwa “kufikiria sala ya unyenyekevu ambayo imepanda kama uvumba huko Mesopotamia kwa karne nyingi: mtoza ushuru wa Injili ana sura ya waamini wengi wa Mashariki ambao, kimya kimya, wanaendelea kusema: "Ee Mungu, unirehemu mimi mwenye dhambi." Maombi yao hayakomi, na leo hii Kanisa la ulimwengu wote linajiunga na kwaya hiyo ya uaminifu inayopenya mawingu na kugusa moyo wa Mungu.”
Akimgeukia Askofu Mkuu huyo, Papa alisema: “Mpendwa Askofu Mkuu Mirosław, unatoka katika nchi ya maziwa na misitu. Katika mandhari hizo, ambapo ukimya unatawala, ulijifunza kutafakari; katikati ya theluji na jua, ulijifunza kiasi na nguvu; katika familia ya wakulima, uaminifu kwa ardhi na kufanya kazi. Asubuhi na mapema ilikufundisha nidhamu ya moyo, na upendo kwa maumbile ulikuongoza kugundua uzuri wa Muumba. Mizizi hii si kumbukumbu ya kuthamini tu, bali ni fundisho la maisha yote. Kutokana na kugusana na dunia, ulijifunza kwamba kuzaa matunda hutokana na kusubiri na uaminifu: ni maneno mawili ambayo pia yanafafanua huduma ya maaskofu.”
Kwa njia hiyo. Papa alisisitiza “Askofu ameitwa kupanda kwa uvumilivu, kukuza kwa heshima, na kusubiri kwa matumaini. Yeye ni mlinzi, si mmiliki; mtu wa maombi, si wa kumiliki. Bwana anakukabidhi utume ili uweze kuutunza kwa kujitolea kama mkulima anavyotunza shamba lake: kila siku, kwa uvumilivu, kwa imani.” Na wakati huo huo, Papa Leo aliongeza kusema “tulimsikiliza Mtume Paulo ambaye, akikumbuka maisha yake mwenyewe, alisema: "Nimepigana vita vizuri, nimemaliza mbio, nimeilinda imani" (2 Tim 4:7). Nguvu yake haitokani na kiburi, bali kutokana na shukrani, kwa sababu Bwana alimtegemeza katika kazi na majaribu yake.” Vile vile, Papa alimwambia kuwa Yeye, ambaye alitembea katika njia ya huduma kwa Kanisa katika Uwakilishi wa Kipapa nchini Senegal na katika Poland yako ya asili, katika Mashirika ya Kimataifa huko Vienna na katika Sekretarieti ya Vatican, kama Afisa wa Katibu Msaidizi wa Mahusiano na Mataifa, umeishi diplomasia kama utii kiukweli wa Injili, kwa busara na uwezo, kwa heshima na kujitolea, na kwa hili ninashukuru.”
Papa Leo XIV aliendelea kusema: “Sasa Bwana anaomba kwamba zawadi hii iwe ubaba wa kichungaji: kuwa baba, mchungaji, na shuhuda wa matumaini katika nchi iliyojaa maumivu na shauku ya kuzaliwa upya. Umeitwa kupigana vita vizuri vya imani, si dhidi ya wengine, bali dhidi ya jaribu la kujichosha, kujizuia, kupima matokeo yako, ukitegemea uaminifu ambao ni sifa yako ya kipekee: Uaminifu wa wale ambao hawajitafutii nafsi zao, bali hutumikia kwa weledi, heshima, na uwezo unaoelimisha na usiojionyesha.”
Mtakatifu Paulo VI, katika Barua yake ya Kitume Sollicitudo omnium Ecclesiarum, Papa Leo aliendelea, “anakumbusha kwamba Mwakilishi wa Papa ni ishara ya Mrithi wa kujali kwa Petro kwa Makanisa yote. Anatumwa kuimarisha vifungo vya ushirika, kukuza mazungumzo na mamlaka ya kiraia, kulinda uhuru wa Kanisa, na kukuza mema ya watu. Balozi wa Kitume si mwanadiplomasia yeyote tu: yeye ni uso wa Kanisa linalosindikizana, kufariji, na kujenga madaraja. Kazi yake si kutetea maslahi ya vyama, bali kutumikia ushirika.”
“Huko Iraq, nchi ya utume wako, Papa aliongeza “huduma hii inachukua maana maalum. Huko, Kanisa Katoliki, katika ushirika kamili na Askofu wa Roma, linaishi katika tamaduni tofauti: Kanisa la Wakaldayo, pamoja na Patriaki wake wa Babeli ya Wakaldayo na lugha ya Kiaramu ya liturujia; Makanisa ya Wakatoliki wa Kisiria, Wakatoliki wa Kiarmenia, Wakatoliki wa Kigiriki, na Kilatini. Ni mchanganyiko wa ibada na tamaduni, historia na imani, unaoomba kukaribishwa na kulindwa katika upendo.”
Papa Leo XIV aliendelea kusema “uwepo wa Wakristo huko Mesopotamia ni wa kale: kulingana na utamaduni, alikuwa Mtakatifu Thomas Mtume aliyepeleka Injili katika nchi hiyo baada ya kuharibiwa kwa Hekalu la Yerusalemu; na wanafunzi wake Addai na Mari ndiyo walioanzisha jumuiya za kwanza. Katika eneo hilo, wanasali kwa lugha ambayo Yesu alizungumza: Kiaramu. Mzizi huu wa kitume ni ishara ya mwendelezo ambao vurugu, zilizooneshwa kwa ukatili katika miongo ya hivi karibuni, hazijaweza kuzima. Hakika, sauti za wale walionyimwa maisha kikatili, katika nchi hizo hazijapungua. Wanakuombea leo, kwa ajili ya Iraq, kwa ajili ya amani ya dunia.”
Kwa mara ya kwanza katika historia, Papa alitembelea Iraq Baba Mtakatifu alisisitiza. “Mnamo Machi 2021, Papa Francisko alifika kama mhujaji wa udugu. Katika nchi hiyo, ambapo Ibrahimu, Baba yetu katika imani, alisikia wito wa Mungu, Mtangulizi wangu alikumbusha kwamba "Mungu, aliyewaumba wanadamu sawa katika utu na haki, anatuita kueneza upendo, ukarimu, na maelewano." Pia nchini Iraq, Kanisa Katoliki linatamani kuwa rafiki kwa wote na, kupitia mazungumzo, kushirikiana kwa njia ya kujenga na dini zingine kwa ajili ya amani" (Francisko, Hotuba kwa Mamlaka, Asasi za Kiraia, na Kikosi cha Kidiplomasia, Machi 5, 2021).” Kwa njia hiyo Papa Leo XIV alisema kuwa “Leo umeitwa kuendelea na safari hiyo: kulinda mbegu za matumaini, kuhimiza kuishi kwa amani, kuonesha kwamba diplomasia ya Kiti Kitakatifu inazaliwa kutokana na Injili na kulishwa na sala.”
Papa wa Roma kwa kuhitimisha alisema: “Askofu Mkuu Mirosław, uwe mtu wa ushirika na ukimya kila wakati, wa kusikiliza na kuzungumza. Peleke maneno yako ya upole unaojenga na katika macho yako amani inayofariji. Nchini Iraq, watu watakutambua si kwa unachosema, bali kwa jinsi unavyopenda.” Tunakabidhi utume wako kwa Maria, Malkia wa Amani, kwa Watakatifu Thomas, Addai, na Mari, na kwa mashuhuda wengi wa imani ya Iraq. Wakusindikize na wawe nuru kwenye njia yako. Na hivyo, Kanisa, katika sala, linapokukaribisha katika Baraza la Maaskofu, hebu tuombe pamoja:Utukufu wa Mungu uwe juu yako na kuangaza njia zako naamani ya Kristo ikae popote utakapoweka hatua zako. Gloria Deo, Pax Hominibus. Amina.”
Asante kwa kusoma makala haya. Ikiwa unataka kuendelea kupata taarifa mpya, tunakualika ujiandikishe kwa jarida letu kwa kubofya hapa: Just click here
