2025.10.24 Papa akutana na walimu na manafuzni wa Taasisi ya Kipapa ya Yohane Paulo II kwa ajili ya Sayansi ya Ndoa na familia. 2025.10.24 Papa akutana na walimu na manafuzni wa Taasisi ya Kipapa ya Yohane Paulo II kwa ajili ya Sayansi ya Ndoa na familia.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV akutana na Taasisi ya Kipapa ya YP II:familia ilindwe na kudumishwa

Katika miktadha ya kijamii,kiuchumi na kiutamaduni kuna changamoto zinazotuhusu:kila mahali tunaitwa kusaidia,kutetea na kuhamasisha familia hasa kwa mtindo wa maisha yanayoendana na Injili.Udhaifu wake na thamani yake kwa kuzingatia mwanga wa imani na sababu yake safi,ijibidishe katika mafunzo yanayokuza wema wa wachumba watakao kuwa wanandoa na wazazi wajao.Ni katika Hotuba ya Papa Oktoba 24 kwa Taasisi ya Kipapa ya Ndoa na Familia.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Hotuba ya Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 24 Oktoba 2025  kwa Taasisi ya Kitaalimungu ya Papa Yohane Paulo II kuhusu Masomo ya Ndoa na Familia, kwa  walimu na wanafunzi wa Taasisi hiyo, alibainisha kuwa  kila mahali na siku zote, tunaitwa kudumisha, kutetea na kukuza familia, hasa kwa kutazama changamoto kuwa ni tofauti katika miktadha tofauti ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Kwa njia hiyo waamini,  lazima waiunge mkono familia wakati wote, zaidi ya yote kupitia njia ya maisha inayoendana na Injili. “Kutangazwa kwa Injili, ambayo hubadilisha maisha na jamii, kunatuahidi kukuza vitendo na vya pamoja katika kuunga mkono familia. Ubora wa maisha ya kijamii na kisiasa ya nchi, hupimwa hasa kwa jinsi inavyoruhusu familia kuishi vizuri, kuwa na muda wao wenyewe, na kukuza vifungo vinavyoziweka pamoja.” Katika jamii ambayo mara nyingi huinua tija na kasi kwa gharama ya mahusiano, Baba Mtakatifu alisema, inakuwa muhimu kurejesha muda na nafasi katika  familia inayojifunza kuuishi upendo huo.

Papa alikutana na Taasis ya Yohane Paulo II
Papa alikutana na Taasis ya Yohane Paulo II   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo alisema akikumbuka kwa hisia, maneno ya mtangulizi wake, Papa Francisko kwamba alipokuwa akiwahutubia kwa upole wanawake wajawazito aliwaombwa wathamini furaha ya kuleta maisha mapya duniani.' Maneno yake, yanajumuisha ukweli rahisi na wa kina: maisha ya mwanadamu ni zawadi na lazima yakaribishwe kwa heshima, uangalifu, na shukrani kila wakati. Kwa hivyo, Papa akitazama hali halisi ya mama wengi wanaoishi katika hali ya upweke au kutengwa alisema: "Ninahisi wajibu wa kukumbusha kwamba jamii ya kiraia na jumuiya ya Kanisa lazima ijitoe kwa uthabiti ili kurejesha heshima yake kamili kwa umama." Kwa kusudi hilo, mipango thabiti ni muhimu, hasa ikitoa wito wa sera zinazohakikisha hali ya kutosha ya maisha na kazi; mipango ya malezi na kiutamaduni inayotambua uzuri wa kuzalisha pamoja; na utunzaji wa kichungaji unawasindikiza wanawake na wanaume kwa ukaribu na kusikiliza. “Umama na ubaba, unaolindwa hivyo sio mizigo inayoilemea jamii, bali ni tumaini linaloiimarisha na kuihuisha.”

Papa Leo XIV aliwakumbusha maprofesa na wanafunzi waliokusanyika kuhusu jukumu la kuimarisha uhusiano kati ya familia na mafundisho ya kijamii ya Kanisa, ambayo alielezea yanaweza kuendelea katika pande mbili zinazosaidiana, "ile ya kuingiza somo la familia kama sura muhimu ya urithi wa hekima ambayo Kanisa linapendekeza kuhusu maisha ya kijamii," na, "kinyume chake, ile ya kuimarisha urithi huu kwa uzoefu na mienendo ya kifamilia, ili kuelewa vyema kanuni za mafundisho ya kijamii ya Kanisa." “Uangalifu huu, ungeruhusu ukuaji wa hisia iliyokumbukwa na Mtaguso II wa Vatican  na kuthibitishwa tena na watangulizi wangu, kuona katika familia kiini cha kwanza cha jamii kama shule ya asili na ya msingi ya ubinadamu."

Taasisi ya Yohane Paulo II
Taasisi ya Yohane Paulo II   (@Vatican Media)

Akitafakari kichungaji, Papa Leo XIV alithibitisha kwamba "hatuwezi kupuuza tabia, katika maeneo mengi ya dunia, ya kutothamini au hata kukataa ndoa." Kwa mtazao huo Papa alipenda kuwaalika kuwa makini, katika kutafakari kwao kuhusu maandalizi ya sakramenti ya Ndoa, kwa tendo la neema ya Mungu katika moyo wa kila mwanamume na mwanamke. "Hata vijana wanapofanya maamuzi ambayo hayaendani na njia zilizopendekezwa na Kanisa kulingana na mafundisho ya Yesu, Bwana anaendelea kubisha mlangoni mwa mioyo yao, akiwaandaa kupokea wito mpya wa ndani,” Papa Leo XIV alisema,

"Ikiwa utafiti wenu wa kitaalimungu na kichungaji umejikita katika mazungumzo ya maombi na Bwana, mtapata ujasiri wa kugundua maneno mapya yanayoweza kugusa kwa undani dhamiri za vijana,” alisema. Ingawa Baba Mtakatifu aliona kwamba wakati wetu hauashiriwi  na "mivutano na itikadi zinazochanganya mioyo tu, bali pia unaashiriwa na utafutaji unaokua wa kiroho, ukweli na haki, hasa miongoni mwa vijana. Kukaribisha na kutunza hamu hii, ni kwa sisi sote ni moja ya kazi nzuri na za haraka zaidi."

Papa aliwatia moyo kuendelea na safari ya sinodi kama sehemu muhimu ya malezi. Hasa katika chuo kikuu cha kimataifa, ni muhimu kufanya mazoezi ya kusikilizana ili kutambua vyema jinsi ya kukua pamoja katika huduma ya ndoa na familia. Kwa kutazama kuwa  kuna mengi ya kujifunza kuhusu uenezaji wa imani, mazoezi ya kila siku ya kusikiliza na kusali, elimu katika upendo na amani, udugu na mhamiaji na mgeni, na utunzaji wa sayari yetu , Papa aliendelea kusema, "Katika nyanja hizi zote, maisha ya familia hutangulia masomo yetu na kuyafundisha, hasa kupitia ushuhuda wa kujitolea na utakatifu." Hatimaye, Baba Mtakati aliwaomba wanafunzi na maprofesa kuanza mwaka mpya wa masomo kwa matumaini, "wakiwa na uhakika kwamba Bwana Yesu hututegemeza kila wakati kwa neema ya Roho wake wa ukweli na uzima."

Taasisi ya Kipapa ya Yohane Paulo II kuhusu Ndoa na Familia
Taasisi ya Kipapa ya Yohane Paulo II kuhusu Ndoa na Familia   (@Vatican Media)

Taasisi ya Kipapa ya Taalimungu ya Yohane Paulo II  kwa Masomo ya Ndoa na Familia

Taasisi ya Kipapa ya Taalimungu ya Yohane Paulo II kwa Masomo ya Ndoa na Familia ilianzishwa na Barua ya Kitume katika mfumo wa Motu Proprio ya Papa Francisko ‘Summa familiae curae’ ya tarehe 8 Septemba 2017. Taasisi hii inafanikiwa na kuchukua nafasi ya Taasisi ya Kipapa ya "Yohane o II" kwa Masomo ya Ndoa na Familia, iliyoanzishwa na Katiba ya Kitume ya Magnum Matrimonii Sacramentum ya tarehe 7 Oktoba 1982. Taasisi hii imegawanywa vituo, Roma, vituo saba vya nje ya miji nchini Marekani (Washington D.C.), Mexico (Mexico D.F., Guadalajara na Monterrey), Hispania (yenye makao mawili huko Valencia na Madrid), Brazil (Salvador), Benin (Cotonou), India (Changanacherry, Kerala) na Vituo Vinavyohusiana huko Lebanon (Beirut), Ufilipino (Bacolod) na Jamhuri ya Dominika (Santo Domingo). Kituo kinginge kishiriki cha  Yohane Paulo II kipo huko Kitui, (Kenya). Muundo wa kimataifa wa Taasisi unawezesha uhamaji wa wahadhiri na wanafunzi kwa ajili ya elimu ambayo ni nyeti kwa changamoto za kiutamaduni na kimataifa.

Asante kwa kusoma makala hii. Kama unataka kusasishwa zaidi, unaweza kujiandikisha kwa makala zetu za kila siku hapa: Just click here

24 Oktoba 2025, 17:18