Maadhimisho ya Jubilei ya Waromu, Wasinti na Wasafiri: Imani, Tumaini na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 18 Oktoba 2025 amekutana na kuzungumza na: Waromu, Wasinti na Wasafiri, na hatimaye kujibu maswali kadhaa yaliyoulizwa na watoto kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo! Katika hotuba yake amekazia kuhusu umuhimu wa: Imani kwa kujiaminisha kwa Mungu, anayewasikiliza na kujibu kilio chao Sala na Kazi. Siku hii imenogeshwa kwa shuhuda mbalimbali kutoka kwa washiriki na moyo wa sala ulionogeshwa na kauli mbiu “Baba na Mama yangu walikuwa Warami Wasafiri.” Kumb 26:5 na kwamba, matumaini ni safari na zawadi wanayoibeba katika sakafu ya nyoyo zao. Baba Mtakatifu Leo XIV amesifia imani yao thabiti na yenye nguvu, tumaini lao lisilotikisika mbele ya Mungu sanjari na amani inaoyokita mizizi yake ndani mwao pamoja na ile ya wachungaji wao, ambao wameendelea kutembea na kuambana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku bila kuchoka!
Maadhimisho ya Jubilei hii, yanakwenda sanjari na kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Paulo VI, tarehe 16 Septemba 1965 alipokutana pamoja na kuzungumza nao, kumbukumbu ya tukio hili ni Sanamu ya Bikira Maria iliyovikwa taji la Malkia wa Waromu, Wasinti na Wasafiri iliyowekwa mjini Pomezia. Viongozi wakuu wa Kanisa kwa nyakati mbalimbali wamekutana na kuzungumza na watu hawa wa Mungu, kielelezo makini cha majadiliano hai yanayokita mizizi yake katika shughuli za kichungaji kwa watu wapendwa mahujaji wapendwa wa Mungu. Watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwathamini, hali kadhalika, Mama Kanisa anawapenda na kuwabariki. Katika kipindi cha milenia ya ustawi na maendeleo, wamejikuta wakisukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, haki msingi za binadamu, elimu na tamaduni, kiasi cha kuwapoka haki na amani; ukarimu na upendo. Ni kundi ambalo limekumbana na ubaguzi na ukosefu wa haki jamii, kiuchumi, kivita na kimazingira katika ngazi ya Kimataifa!
Lakini katika maisha na utume wao wamekuwa kama alivyosema Kristo Yesu: “Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu?” Mt 21:42. Hiki ni kito cha thamani wanachobeba maskini katika sakafu ya mioyo yao, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika maisha ya: haki, amani na utulivu kwa kujikita katika ujenzi wa umoja, mshikamano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Hii ni jamii ambayo haifungamani na malimwengu kiasi kwamba, iko huru kutembea katika Roho Mtakatifu na kutokana na hali hii wamekuwa kweli ni watu wenye heri, kama alivyowahi kusema Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Hali na mazingira kama haya, kamwe yasiwakatishe tamaa, kwani kimsingi maisha yao yanafanana na yale ya Kristo Yesu; Fukara na aliyenyanyaswa, kielelezo cha maisha ya Kristo Yesu. Waendelee kujiaminisha katika wokovu wa Mungu, huku wakilinda na kuendeleza utu, heshima na haki zao msingi zinazopata chimbuko lake kutoka katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, fursa za kazi, ajira na ujira, pamoja na kujikita katika maisha ya sala; nguvu katika kuvunjilia mbali kuta za kutoaminiana, woga na wasiwasi usiokuwa na mvuto wala mashiko.
Huu ndio wito na utume wao ndani ya Kanisa na kwamba, wanapaswa kujikita kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; wawe na ujasiri wa kuchangia na kushirikisha sifa zao mahususi zinazowaunda na kuashiria njia zao na ambazo zinahitajika sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Wawe ni wadau wakuu katika mabadiliko yanayoendelea sasa katika ulimwengu mamboleo, watembee kwa pamoja, washinde tabia ya kutoaminina, wawe tayari kushirikisha wa utamaduni wao, imani, sala na ujira kwa kazi ya uaminifu. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wote waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, Maadhimisho ya Jubilei hii yanafanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba, wahakikishe kwamba, wanafuatilia na kutekeleza maamuzi yaliyopitishwa katika Maadhimisho ya Kongamano la Tano la Kimataifa kuhusu Shughuli za Kichungaji kwa Waroma kwa kukazia: Shughuli za kichungaji kwa familia na jamii; Uenezaji wa Liturujia na Katekesi makini; Majadiliano ya Kiekumene na Kidini katika Ulimwengu wa Waroma, Wasinti, na Wasafiri na kwamba, kila jimbo linatakiwa kukuza na kudumisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa jamii za Waroma, Wasinti na Wasafiri kwa ajili ya maendeleo ya kweli ya binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yatasaidia kuimarisha imani, matumaini na hija ya maisha yao mintarafu Injili ya Kristo. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awalinde na kuwatunza.
Baba Mtakatifu Leo XIV hatimaye, alijibu maswali kutoka kwa watoto wadogo kwa kuwaambia kwamba, ili kujenga urafiki na Kristo wanapaswa kuheshimiana, kwa kujibidiisha kumfahamu Kristo Yesu kwa njia ya Maandiko Matakatifu, Sala na historia yao binafsi; wajitahidi kuwa wakweli na waaminifu; wanyenyekevu, na wapole wa moyo katika maisha ya kijumuiya na kwa njia ya Kanisa. Wawe ni washiriki waaminifu wa Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho! Watu wa Mungu wanapaswa kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa amani, inayopata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya nyoyo zao! Wajitahidi kujenga majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga amani, ili kweli watu waweze kuishi katika misingi ya haki, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuondokana na maamuzi mbele, wajitahidi kujenga umoja na mshikamano, wakitambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; kumbe, wajenge udugu wa kibinadamu, ili kuweza kuleta mabadiliko ulimwenguni. Kanisa linatoa kipaumbele na huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, maskini wanapaswa kupendwa na kuheshimiwa na wote. Maskini ni shule ya haki, amani na utakatifu.
