Parokia ya Mtakatifu Anna,mjini Vatican. Parokia ya Mtakatifu Anna,mjini Vatican.  (Lorena Leonard)

Papa Leo XIV ataadhimisha Misa katika Parokia ya Mtakatifu Anna,Septemba 21

Ofisi ya Waandishi wa Habari ya Vatican imetangaza kwamba Baba Mtakatifu Leo XIV atatembelea Kanisa la kale lililoko ndani ya Mji wa Vatican,kuadhimisha Dominika ya 25,kipindi cha Kawaida cha mwaka C.Kanisa hili ni la karne ya 16 ambalo lilikabidhiwa uchungaji wa Shirika la Mtakatifu Agostino tangu mwaka 1929 hadi leo hii.

Na Tiziana Campisi – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV ataongoza Ibada ya Misa saa 4.00 kamili asubuhi, masaa ya Ulaya, sawa na saa 5 .00 kamili masaa ya Afrika Mashariki na Kati, Dominika tarehe 21 Septemba 2025, katika Parokia ya Mtakatifu Anna jijini Vatican. Hii ilitangazwa na Ofisi ya Vyombo vya habari, Vatican. Hata hivyo akiwa kama Kardinali Prevost, aliwahi kuadhimisha Liturujia ya Ekaristi hapo tarehe 26 Julai 2024, katika fursa ya ukumbusho wa kiliturujia ya Watakatifu Joachim na Anna.

Makao makuu ya zamani ya  Chama cha Udugu wa "Palafrenieri"

Kanisa hilo la kale, lililojengwa katika karne ya 16, lilikuwa makao makuu ya  chama cha udugu wa ‘Palafrenieri’ wa Kipapa, uliokuwa unahusika na mabanda ya kipapa, ambao Mtakatifu wake Msimamizi alikuwa Mtakatifu Anna. Baada ya Mkataba wa Lateran, tarehe 30 Mei 1929, Papa Pio XI, pamoja na  Barua ya Kitume ya Ex Lateranensi pacto, aliianzisha kama Parokia na kuikabidhi chini ya uchungaji wake kwa watawa wa Shirika la Mtakatifu Agostino. Paroko wake wa kwanza, Padre Agostino Ruelli, aliteuliwa mwaka huo huo mnamo tarehe 7 Agosti 1929. Paroko wa sasa ni Padre wa Agostino Mario Millardi.

Mapapa katika Parokia ya Mtakatifu Anna, jijini Vatican

Parokia ya Mtakatifu Anna imetembelewa na  Papa Pio XI, ambaye alitamani kuwapo kwenye uzinduzi wa chombo hicho mnamo tarehe 7 Februari 1931; Papa Yohane XXIII, ambaye alitembelea mnamo 20 Januari  1961;  Papa Paulo VI, ambaye aliadhimisha kumbu kumbu ya miaka 50 ya ukuhani wake saa 2:00 asubuhi tarehe 29 Mei 1970; Papa Yohane Paulo II, aliyeiita "Parokia yangu" katika mahubiri yake tarehe 10 Desemba 1978; Papa Benedikto XVI, ambaye aliongoza ibada ya misa  tarehe 5 Februari 2006; na Papa Francisko, ambaye aliichagua  Misa yake ya kwanza kwa umma  tarehe 17 Machi 2013.

.

19 Septemba 2025, 18:53