Papa Leo XIV akutana na Kundi kazi la Mkutano wa 12 kati ya Vatican na Vietnam
Vatican News
Mkutano wa kumi na mbili wa Kikundi Kazi cha Pamoja kati ya Vietnam na Kiti kitakatifu ulifanyika Ijumaa tarehe 12 Septemba 2025 mjini Vatican. Mkutano huo, kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari, uliongozwa na Monsinyo Mirosław Wachowski, Katibu Msaidizi wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa, na mashirika ya kimataifa, akiwa mkuu wa ujumbe wa Kiti kitakatifu na Le Thi Thu Hang, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na mkuu wa ujumbe wa Vietnam.
Katika taarifa hiyo inasomeka kuwa: "Wakati wa majadiliano pande hizo mbili zilishughulikia uhusiano wa pande mbili na hali ya Kanisa Katoliki nchini Vietnam. Mchango wa jumuiya ya Kikatoliki katika maendeleo ya nchi, katika roho ya ushuhuda wa kiinjili na ushirikiano wa kiraia, pia ulitambuliwa.”
Kuridhika na Maendeleo yanayopatikana
Mkutano wa Kiti Kitakatifu na Vietnam, ulidhihirisha kuridhishwa na maendeleo yaliyopatikana kufuatia mkutano wa 11, uliofanyika mnamo Mei 2024 huko Hanoi, mji mkuu wa nchi hiyo ya Asia, tukikumbuka mazungumzo yanayoendelea, mabadilishano ya wajumbe katika ngazi mbalimbali-hasa katika ngazi ya juu-na shughuli za mwakilishi wa Papa mkazi wa Hanoi, Askofu Mkuu Marek Zalewski,” taarifa inasomeka.
Kukuza Zaidi Mahusiano
Wajumbe wote wawili, waraka huo unaendelea, "walithibitisha nia yao ya kuendeleza uhusiano zaidi kupitia mikutano mipya, na pia walikubali kuendeleza mikutano ya Kikundi Kazi cha Pamoja mara kwa mara. Mkutano ulifanyika katika mazingira yaliyofafanuliwa kama ya huruma na yenye kuaminiana."
Mkutano na Papa na Sekretarieti ya Vatican
Taarifa hiyo inahitimisha kwa kueleza kwamba, wakati wa kukaa kwao Vatican, ujumbe wa Vietnam ulipokelewa na Baba Mtakatifu Leo XIV. Ziara za heshima ilifuatiwa na kukutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican, na Askofu Mkuu Paul Gallagher, Katibu wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa.
