Hospitalini pawe ni mahali pa kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo na huruma ya Mungu. Hospitalini pawe ni mahali pa kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo na huruma ya Mungu.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Watoto Wagonjwa wa Saratani: Mahujaji wa Matumaini

Papa Francisko anasema: Inasikitisha kuona kwamba, kuna idadi kubwa sana ya watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia, hawana nafasi ya kupata tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasumbua. Pengine ni kutokana na uhaba wa dawa na vifaa tiba; ukosefu wa zahanati na hospitali; wakati mwingine ni kutokana na ukosefu wa madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya. Kwa wote hawa Mama Kanisa anapenda kuwaonesha uwepo wake wa karibu. Matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huduma makini kwa wagonjwa inapaswa kujikita katika usawa na haki, kwa kuzingatia utu na heshima ya wagonjwa wote, hata kama wako kufani! Vatican kwa sasa imeweka sera na mkakati wa kuendelea kuwekeza zaidi katika vifaa tiba na tafiti kama sehemu ya maboresho ya huduma ya upendo kwa watoto wadogo. Hospitalini pawe ni mahali pa kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo na huruma ya Mungu; mahali ambapo wahudumu wa sekta ya afya wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa. Kila mfanyakazi katika nafasi na dhamana yake, ajivike fadhila ya unyenyekevu katika huduma; kwa kukuza na kudumisha nia njema inayomwilishwa katika huduma ya upendo mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake!

Watoto wenye Saratani: Mahujaji wa matumaini
Watoto wenye Saratani: Mahujaji wa matumaini

Inasikitisha kuona kwamba, kuna idadi kubwa sana ya watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia, hawana nafasi ya kupata tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasumbua. Pengine ni kutokana na uhaba wa dawa na vifaa tiba; ukosefu wa zahanati na hospitali; wakati mwingine ni kutokana na ukosefu wa madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya. Kwa wote hawa Mama Kanisa anapenda kuwaonesha uwepo wake wa karibu. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na watoto wagonjwa kutoka Kliniki ya Watoto Wenye Saratani ya Breslavia, nchini Poland, waliokuwa wanafanya hija ya matumaini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo inayonogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini.”

Kristo Yesu ni rafiki wa kweli katika raha na mahangaiko yao
Kristo Yesu ni rafiki wa kweli katika raha na mahangaiko yao

Huu ni mwaka unaopania kutoa faraja na upendo katika mateso; ili hatimaye, kuweza kuunganika pamoja katika mahangaiko ya binadamu; kwa kushirikishana pia furaha na matumaini, kama rafiki, kama jinsi Kristo Yesu alivyofanya kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Wagonjwa ni marafiki wa Kristo Yesu katika furaha na mateso. Rej Yn 15:15. Kristo Yesu ni rafiki wao wa kweli kwa njia ya upendo angavu unaoneshwa na kushuhudiwa na wazazi pamoja na walezi wao; huduma makini inayotolewa na wafanyakazi katika sekta ya afya; wote hawa wanalenga kupyaisha ndoto na matumaini ya maisha yao.

Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu.
Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, hata yeye yuko karibu nao na hivyo akawaomba waendelee kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sala, nia njema pamoja na kutolea mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya huduma kwa Kanisa. Amewataka watoto hawa kuendelea kuwa na ujasiri katika shida na mahangaiko yao, kwa sababu kimsingi wao ni mashuhuda wa matumaini kwa watoto wenzao na kwa watu wazima. Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwashukuru na kuwapongeza wale wote waliofanikisha hija hii ya matumaini kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo.

Watoto Wagonjwa
14 January 2025, 14:35