Mheshimiwa Sr. Simona Brambila, Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake, ili waendelee kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Bila mchango wa wanawake, Kanisa litapoteza nguvu yake ya kujipyaisha tena. Dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa unajidhihirisha wazi kwa njia ya Bikira Maria, Nyota ya Uinjilishaji mpya. Kumbe, Kanisa linapaswa kushikamana pamoja na “wanawake wa shoka” ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanarithisha: imani, tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kitamaduni na kijamii kwa watoto wao. Itakumbukwa kwamba, wanaume na wanawake, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wapendane na kukamilishana; bila kuwadharau, kuwabeza na kuwanyanyasa wanawake.
Wanawake washirikishwe pia katika malezi na majiundo ya majandokasisi na watawa. Sauti ya wanawake, inapaswa kusikilizwa ndani ya Kanisa. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wanasema, wanawake ni rasilimali muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake washirikishwe katika mchakato wa kufanya maamuzi katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria awe ni mfano bora katika shule ya ufuasi wa Kristo Yesu. Vijana wawe ni nyota ya Msamaria mwema kwa njia ya huduma; nyota ya umisionari, matumaini na majadiliano ya: Kitamaduni, kidini na kiekumene. Kimsingi, Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, dhamana na utume wa wanawake katika Kanisa hauna budi kuimarishwa, kwa kukazia zaidi makuzi, malezi na majiundo ya awali, endelevu na fungamani, ili kuondokana na mfumo dume unaowanyima wanawake haki zao msingi. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni mambo muhimu katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua dhamana na wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa amemteua Mheshimiwa sana Sr. Simona Brambilla, M. C. wa Shirika la Wamisionari wa Consolata kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume na anakuwa ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wajuu kabisa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Ana uzoefu wa maisha na utume wa kimisionari nchini Msumbiji. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteuwa pia Kardinali Ángel Fernández Artime, S.D.B., kuwa ni Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.
Itakumbukwa kwamba, Mheshimiwa sana Sr. Simona Brambilla, M. C. alizaliwa tarehe 27 Machi 1965 huko Monza, Jimbo kuu la Milano. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kitawa, mwaka 1991 akaweka nadhiri zake za kwanza na hatimaye, mwaka 1999 akafunga nadhiri za daima. Kunako mwaka 2011, akachaguliwa kuliongoza Shirika la Masista wa Consolata na kupewa tena dhamana ya kuongoza Shirika hilo kunako mwaka 2017 na kufikia Mwezi Mei 2023 akang’atuka kutoka madarakani. Tarehe 7 Oktoba 2023, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Ufunuo wa Bwana yaani Epifania, tarehe 6 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na za Kazi za Kitume.
Itakumbukwa kwamba, Kardinali Ángel Fernández Artime, S.D.B., Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume alizaliwa tarehe 21 Agosti 1960 huko Gozón-Luanco, Jimbo kuu la Oviedo, nchini Hispania. Baada ya malezi na majiundo yake kwenye Shirika la Wasalesian wa Don Bosco, akaweka nadhiri zake za daima tarehe 17 Juni 1984 na hatimaye, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 4 Julai 1987. Tarehe 25 Machi 2014 akachaguliwa kuwa ni Mkuu wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco hadi tarehe 16 Agosti 2024 alipong’atuka kutoka madarakani. Tarehe 30 Septemba 2023 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Kardinali na kusimikwa tarehe 17 Desemba 2023. Tarehe 5 Machi 2024, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu na kuwekwa wakfu tarehe 20 Aprili 2024. Na ilipogota tarehe 6 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.