Sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Siku ya Sala, Mshikamano, Udugu Na Upendo

Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Hii ni sherehe ya sala na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, huruma na mapendo ya Kimungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Tokeo la Bwana au Epifania ni Sherehe inayokita ujumbe wake katika ufunuo wa Kristo Yesu kama Masiha wa Israeli, Mwana wa Mungu na Mwokozi wa Ulimwengu. Mamajusi wanawakilisha dini za mazingira ya kipagani. Injili inaonesha matunda ya kwanza ya watu wa Mataifa wanaopokea Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Mamajusi wanaonesha ile kiu ya watu wa Mataifa kutafuta kwa Israeli mwanga wa Masiha. Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, Mamajusi wa mashariki, wataalam wa nyota walifika Yerusalemu, wakisema, “Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Rej. Mt 2:1-12. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2025 anasema, Mamajusi kutoka Mashariki, walijitaabisha kumtafuta Mtoto Yesu mjini Bethlehemu, huku wakiongozwa na nyota angavu, lakini wale waliokaa mjini humo, hawakujitaabisha kumtafuta Mtoto Yesu hata kidogo. Lakini Mamajusi walifunga safari, kiasi hata cha kuweza kuhatarisha maisha yao, wakaingia gharama, wakakutana na vikwazo, lakini wakiwa na nia ya kutaka kumwona Mtoto Yesu, kwa hakika hawakutaka kupitwa na fursa hii adhimu.

Siku ya Utoto Mtakatifu ilianzishwa na Papa Pio XII mwaka 1950
Siku ya Utoto Mtakatifu ilianzishwa na Papa Pio XII mwaka 1950

Lakini wale waliokuwa Bethlehemu waliopaswa kuwa na furaha tele, tayari kumpokea na kumkaribisha Mtoto Yesu, walibaki wakiwa wameketi tu. Mapadre na Wanataalimungu, wanafasiri Maadiko Matakatifu kwa ufasaha, kiasi hata cha kutoa maelekezo wapi anazaliwa Mtoto Yesu, lakini hata hawa wanabaki wameketi kwenye viti vyao enzi. Wameridhika na kile ambacho wanamiliki. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujibidiisha kutoka Yerusalemu, ili kuwasindikiza Mamajusi kwenda kumwona Mtoto Yesu, hata kama ni kilometa chache tu. Baba Mtakatifu anawaalik waamini kufahamu wao wanaangukia kundi gani? Je, wako tayari kuondoka kwa haraka, Je, ni kama waamini wanaofanana na wale wachungaji wa kondeni, waliondoka kwa haraka usiku ule kwenda kumwona Mtoto Yesu au wanafanana na Mamajusi kutoka Mashariki, ambao kwa imani kubwa wanajibidiisha kumtafuta Neno wa Mungu aliyefanyika mwili?

Sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Sala, mshikamano na ujenzi wa udugu wa kibinadamu
Sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Sala, mshikamano na ujenzi wa udugu wa kibinadamu

Au waamini wanafanana na wale ambao ingawa wako karibu sana na Mtoto Yesu, lakini hawathubutu kamwe kufungua malango ya nyoyo na maisha yao na matokeo yake wanabaki wakiwa wamejifungia kiasi cha kushindwa kutambua uwepo wa Mtoto Yesu kati yao. Mwenyezi Mungu amekuja kwa watoto wake na hivyo kuwakirimia upendo wake usiokuwa na kifani. Huyu ndiye yule “aliyezaliwa na mwanamke” anahitaji walau kila kitu katika maisha. Je, waamini wanajitaabisha kumwendea au wameamua “kumgeuzia kisogo? Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia, kuwaiga wachungaji wa kondeni pamoja na Mamajusi, kumtambua Kristo Yesu ambaye yuko karibu nao katika: Fumbo la Ekaristi Takatifu, miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na wafungwa kwa kusadaka muda kidogo, nguvu na uwepo wao kwa ajili ya Mungu na jirani zao, ili waweze kupata faraja kwa kuwafariji wengine; kwa kuwainua, ili nao waweze kuinuliwa; kwa kupata maana ya maisha, kwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Malezi makini kwa watoto
Sikukuu ya Utoto Mtakatifu: Malezi makini kwa watoto

Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Hii ni sherehe ya sala na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, huruma na mapendo. Ni Siku ya kutangaza pamoja Injili ya upendo; Kusali kwa pamoja kama ndugu; kucheza pamoja, kielelezo makini cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kutembea pamoja kama mahujaji wa matumaini, kwa kujisadaka bila ya kujibakzia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia. Kauli mbiu inayonogesha maadhimisho haya ni “Vade et invitare omnes ad convivium” yaani “Nendeni mkawaalike wote kwenye sherehe.” Watoto wanapaswa kujifunza na hatimaye, kujenga utamaduni wa: umoja, upendo na mshikamano, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni!

Watoto mashuhuda wa imani
Watoto mashuhuda wa imani

Hii ni changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimissionari tangu sasa, ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, njaa, ujinga na baa la umaskini. Hata katika umaskini wao, watoto wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia! Huu ndio mshikamano wa watoto katika huduma ya Injili ya upendo! Sala ya Watoto wa Utoto Mtakatifu: “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, ni milango mingapi iliyofungwa... Nyuma yao, hadithi za ndugu zetu, machozi na tabasamu za wanadamu. Karibu au mbali, kuna kitu bado kinatutenganisha... Utuwezeshe, wakati wa Maadhimisho ya Jubilei hii, tuwe mahujaji wa matumaini, watoto ambao hawajifungii ndani, tukiwakaribisha watoto wamisionari, tayari kubisha hodi kwenye milango ya wengine. Na hatimaye, na tuache mlango wa moyo wazi, ili kukuruhusu uingie na kusherehekea pamoja na ulimwengu wote. Amina.”

Utoto Mtakatifu: Malezi makini kwa watoto na vijana
06 January 2025, 15:07

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >