Papa Francisko ametoa onyo la uonevu shuleni na kuweka msingi wa imani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Januari 2025 amekutana Chama cha Walimu wa Kikatoliki cha Italia(AIMC), Umoja wa Waalimu wa Kikatoliki wa Italia,Wasimamizi, Waelimishaji, Wakufunzi(UCIID),Chama cha Wazazi wa Shule za Kikatoliki(AGESC), katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican. Katika hotuba yake ameonesha furaha ya kukutana ikiwa ni katika hafla ya maadhimisho ya Mashirika yao: Miaka 80 ya Chama cha Walimu Wakatoliki wa Italia na Umoja wa Waalimu wa Kikatoliki wa Italia, Wasimamizi, Waelimishaji, Wakufunzi, na Miaka 50 ya Umoja wa Wazazi wa Shule za Kikatoliki. Ni fursa nzuri ya kusherehekea pamoja na kukumbuka historia yao na kutazama siku zijazo. Zoezi hili, harakati hii kati ya mizizi - kumbukumbu - na matunda - matokeo - ni msingi wa kujitolea katika uwanja wa elimu. Papa amebainisha kwamba Mkutano wao umefanyika katika kipindi cha liturujia wa Noeli wakati ambao unatuonesha ufundishaji wa Mungu. Na "njia yake ya elimu ni ipi? Ni ile ya ukaribu. Mungu yuko karibu, mwenye huruma na mpole. Sifa tatu za Mungu ni ukaribu, huruma na upole."
Ukaribu
Papa Francisko aliwaeleza kuwa kuwa kama mwalimu anayeingia katika ulimwengu wa wanafunzi wake, Mungu anachagua kuishi kati ya wanadamu ili kufundisha kupitia lugha ya uzima na upendo. Yesu alizaliwa katika hali ya umaskini na usahili: hii inatuita kwenye ufundishaji unaothamini mambo muhimu na kuweka unyenyekevu, ukarimu na huruma katikati. Ualimu ulio na mbali na watu haufai,hausaidii. Noeli inatufundisha kwamba ukuu hauoneshwi katika mafanikio au utajiri, lakini katika upendo na huduma kwa wengine. Mungu ni mfundishaji wa zawadi, wito wa kuishi katika ushirika naye na wengine, kama sehemu ya mpango wa udugu wa ulimwengu wote, mpango ambao familia ina nafasi kuu na isiyoweza kubadilishwa.
Familia
Zaidi ya hayo, ualimu huu ni mwaliko wa kutambua utu wa kila mtu, kuanzia wale waliotupwa na walio pembezoni, jinsi wachungaji walivyotendewa miaka elfu mbili iliyopita, na kufahamu thamani ya kila awamu ya maisha, ikiwa ni pamoja na utoto. Papa Francisko amekazia kusema kuwa Familia ndio kitovu, wasisahau! Katika hili Papa Francisko amekumbusha tena historia aliyosimuliwa na mtu mmoja kuwa: Dominika moja alikuwa amealika kwa chakula cha mchana kwenye mgahawa na kwenye meza iliyokuwa karibu nao, kulikuwa na familia, ya baba, mama, mwana na binti. Wote wanne wakiwa na simu za mikononi, hawakuzungumza mmoja na mwingine bali walikuwa wakizungumza na simu za mikononi. Bwana huyu alijisikia kitu, ndani mwake na akasogea na kusema: “Lakini nyinyi ni familia, kwa nini msiongee pamoja badala ya kufanya hivyo? Ni jambo la ajabu ... ". Walimsikiliza, wakamwambia aende kuzimu na wakaendelea kufanya mambo yao... Kwa sababu hiyo Papa Francisko ameongeza kusema: “Tafadhali, tuzungumze katika familia! Familia ni mazungumzo, mazungumzo ambayo hutufanya kukua. “
Mahujaji wa Matumini
Mkutano huo Papa alisema pia umefanyika mwanzoni mwa safari ya Jubilei, iliyoanza siku chache zilizopita kwa usahihi kwa kuadhimisha tukio ambalo, kwa kufanyika mwili kwa Mwana wa Mungu, matumaini yaliingiaulimwenguni. Jubilei ina mengi ya kusema kwa ulimwengu wa elimu na shule. Kwa hakika, "mahujaji wa matumaini" ni watu wote wanaotafuta maana katika maisha yao na pia wale wanaosaidia watoto wadogo kutembea kwenye njia hii. Mwalimu mzuri ni mwanamume au mwanamke mwenye matumaini, kwa sababu anajitolea kwa uaminifu na uvumilivu kwa mpango wa ukuaji wa binadamu. Matumaini yake si ya kipuuzi, yamejikita katika uhalisia, yakiungwa mkono na imani kwamba kila juhudi ya elimu ina thamani na kwamba kila mtu ana utu na wito unaostahili kukuzwa. Katika hili hata hivyo Papa Francisko ameonesha masikitiko yake: “Naumia sana ninapoona watoto ambao hawajasoma na wanaokwenda kazini, mara nyingi wananyonywa au wanaokwenda kutafuta chakula au vitu vya kuuza mahali palipo na takataka. Ni ngumu sana! Na kuna hwa watoto wengi!
Kwa njia hiyo aliongeza kusema Papa “Matumaini ndio injini inayomuunga mkono mwalimu katika kujitolea kwake kila siku, hata katika shida na kushindwa. Lakini tunawezaje kupoteza tumaini na kumwilisha kila siku? Kuweka mtazamo kwa Yesu, mwalimu na msindizaji wetu njiani: hii inatuwezesha kuwa kweli mahujaji wa matumaini. Mfikirie kuhusu watu mnaokutana nao shuleni, watoto na watu wazima: «Kila mtu anatumaini.” Papa amewashauri. Katika moyo wa kila mtu kuna tumaini kama hamu na matarajio ya mema, hata bila kujua kesho italeta nini" (Spes non confundit, 1). Matumaini haya ya kibinadamu, kupitia kila mmoja wenu, yanaweza kukutana na tumaini la Kikristo, tumaini linalozaliwa kutokana na imani na kuishi katika mapendo. Na tusisahau: matumaini hayakatishi tamaa. Hamu hukatisha tamaa, lakini matumaini hayakatishi tamaa. Tumaini linalopita kila hamu ya mwanadamu, kwa sababu inafungua akili na mioyo kwa uzima na uzuri wa milele.
Shule inahitaji hii! Kujisikia kuitwa kuendeleza na kusambaza utamaduni mpya, kwa kuzingatia mkutano kati ya vizazi, juu ya kuingizwa, juu ya utambuzi wa kweli, mzuri; utamaduni wa uwajibikaji, binafsi na wa pamoja, kukabiliana na changamoto za kimataifa kama vile migogoro ya kimazingira, kijamii na kiuchumi, na changamoto kubwa ya amani. Shuleni unaweza "kufikiria amani", ambayo ni, kuweka misingi ya ulimwengu wa haki zaidi na wa kindugu, na mchango wa taaluma zote na ubunifu wa watoto na vijana. Lakini ikiwa shuleni mnapigana vita miongoni mwao, ikiwa shuleni inawaonea wasichana na wavulana walio na matatizo, hii ni kujiandaa kwa vita, si kwa ajili ya amani! Tafadhali, kamwe msionee! Je, mnaelewa hili? (walijibu “Ndiyo !”) Sote tuseme pasiwepo uonevu!
Kushehereka Jubilei
Papa Francisko alisema kuwa wao walikuwa hapo kwa ajili ya kusherehekea kumbukumbu muhimu za Jumuiya zao zilizoundwa ili kutoa mchango kwa shule, kwa mafanikio bora ya malengo yake ya kielimu. Na si kwa shule kama chombo, bali kwa watu wanaoishi na kufanya kazi ndani yake: wanafunzi, walimu, wazazi, wasimamizi na wafanyakazi wote. Mwanzoni mwa historia yao kulikuwa na dhana kwamba ni kwa kushirikiana tu, kwa kutembea pamoja, shule inaweza kuboreshwa, ambayo kwa asili yake ni jumuiya, inayohitaji mchango wa kila mtu. Waanzilishi wao waliishi nyakati ambazo maadili ya mtu na ya uraia wa kidemokrasia yalihitaji kushuhudiwa na kuimarishwa, kwa manufaa ya wote; na pia thamani ya uhuru wa elimu.
'Msisahau mlikotoka'
Papa Francisko alisisitiza kuwa wasisahau kamwe walikotoka, lakini wasitembee kwa kuinamisha vichwa chini kwa majuto, wakijutia nyakati nzuri zilizopita! Badala yake, wafikirie juu ya sasa ya shule, ambayo ni mustakabali wa jamii, ikikabiliana na mabadiliko ya nyakati. Wafikirie walimu wvijana wanaochukua hatua zao za kwanza shuleni na familia zinazohisi upweke katika kazi yao ya elimu. Wapendekeza mtindo wao wa elimu na ushirika kwa kila mmoja kwa unyenyekevu na mambo mapya. Papa amewahimiza kufanya haya yote pamoja, kwa aina ya "mapatano kati ya vyama", kwa kwa njia hiyo wanaweza kutoa ushahidi bora katika uso wa Kanisa na shuleni. Matumaini hayakatishi tamaa kamwe, tumaini halijatulia, tumaini huwa linakwenda na kutufanya tutembee. Kwa hivyo wasonge mbele kwa ujasiri! Papa amewabariki na wote wanaowasindikiza na mitandao yote ya mashirika yao. Amewakumbusha wasisahau kumwombea na vile Wasionee kamwe na wajifunze!