Katika Kanisa Katoliki maadhimisho ya Jubilei ni mwaka wa toba na maondoleo ya dhambi; upatanisho, na wongofu wa ndani. Katika Kanisa Katoliki maadhimisho ya Jubilei ni mwaka wa toba na maondoleo ya dhambi; upatanisho, na wongofu wa ndani.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo: Mahujaji wa Matumaini

Katika Kanisa Katoliki maadhimisho ya Jubilei ni mwaka wa toba na maondoleo ya dhambi; upatanisho, na wongofu wa ndani unaojikita katika Sakramenti ya Kitubio. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini. Huu ni muda muafaka wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu; Kusali na kumwilisha sala hii katika matendo ya huruma kiroho na kimwili, ili kuwaonjesha matumaini wale waliopondeka na kuvunjika moyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Kanisa Katoliki maadhimisho ya Jubilei ni mwaka wa toba na maondoleo ya dhambi; upatanisho, na wongofu wa ndani unaojikita katika Sakramenti ya Kitubio. Neno Jubilei linapata chanzo na asili yake kutoka katika Lugha ya Kiebrania (ἀφέσεως σημασία, afeseos semasia) na tafsiri yake kwa lugha ya Kilatini ni “Iobeleus” yaani Jubilei kwa lugha ya Kiswahili. Jubilei ni mwaka wa Kristo Yesu. Katika Agano Jipya, Kristo Yesu anajionesha kuwa ndiye utimilifu wa nyakati akisema “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenipaka mafuta niwahubirie maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafunga kufunguliwa, vipofu kuona tena, kuwaletea wafungwa uhuru, na kutangaza mwaka uliokubalika kwa Bwana.” Lk 4:18-19. Kumbe maadhimisho ya Jubilei yanaitwa kwa haki kuwa ni maadhimisho ya “Mwaka Mtakatifu” kwa sababu unasimikwa katika Liturujia ya Kanisa inayowajenga kila siku wale waliomo katika Kanisa wawe Hekalu la Roho Mtakatifu, Makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo. Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumtangaza  na kumshuhudia Kristo Yesu. Lengo ni kujenga na kukuza umoja na mshikamano wa watoto wa Kanisa. Liturujia ni muhimu kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Kristo Yesu. Liturujia ni utekelezaji wa kazi ya Kikuhani ya Kristo Yesu.

Liturujia: Mungu atukuzwe na binadamu atakatifuzwe
Liturujia: Mungu atukuzwe na binadamu atakatifuzwe

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Liturujia, Ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa Fumbo wa Kristo Yesu, yaani Kanisa. Hili ni tendo takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anaendelea kuwachangamotisha viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika malezi makini ya Kiliturujia pamoja na ushiriki hai wa waamini. Ni Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliotambua na kuthamini umuhimu wa kutafsiri vitabu vya Liturujia ili Ibada mbalimbali ziweze kufahamika na wengi: kwa kukazia ukamilifu na ufahamu wa Ibada inayoadhimishwa. Liturujia irekebishwe kulingana na hali za watu na Mapokeo yao, kwa maneno mengine, huu ni mwanzo wa jitihada za utamadunisho wa Liturujia katika uhalisia wa maisha ya waamini sehemu mbalimbali za dunia. Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji! Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu. Liturujia ni chemchemi ya kwanza ambayo mwamini anaweza kuchota roho ya kweli ya kikristo. Kumbe, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei, pamoja na mambo mengine, yanapania kukuza na kudumisha utakatifu wa maisha.

Liturujia: Mungu Atukuzwe na Binadamu atakatifuzwe
Liturujia: Mungu Atukuzwe na Binadamu atakatifuzwe

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yanayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelelea siku zijazo; ili kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa kujitahidi kupyaisha utambulisho wao na kuwa jinsi walivyo, kwa njia ya imani, tayari kushuhudia ubora wao katika maisha ya kila siku. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 yana mwelekeo wa Kiekumene kwani wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupita katikati ya Mlango wa Imani, sanjari na kutangaza na kushuhudia kanuni ya Imani ya Nicea. Kristo Yesu anasema “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Rej. Yn 10: 1-18. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Mahujaji wa matumaini, imani na mapendo
Mahujaji wa matumaini, imani na mapendo

Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani tayari kuambata utakatifu wa maisha. Bikira Maria, nyota ya alfajiri anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015, Kanisa liliadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu; mwaka ambao uliwawezesha waamini wengi kuvuka Lango la Huruma ya Mungu, ili kuonja upendo unaofariji, unaosamehe na kutoa matumaini. Hii ndiyo hamu inayopaswa kushuhudiwa na watu wote kwa kuwaonjesha jirani zao wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawataka waamini kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha ili kuwaokoa, mwaliko kwao pia ni kujishusha na kuwainamia jirani zao wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali, kwa kuwa na jicho la huduma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuwaonjesha watu wanaoteseka, ile “divai ya furaha na matumaini pamoja na kuwapaka mafuta ya faraja”, kama ilivyotokea kwenye Arusi ya Kana.

Jubilei kuu iwe ni chemchemi ya utakatifu wa maisha
Jubilei kuu iwe ni chemchemi ya utakatifu wa maisha

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwaliko wa kufanya mabadiliko katika maisha; Ni Pasaka ya kufanywa upya, kuingia katika maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu; Hii ni Pasaka ya kupyaishwa katika maisha na utu wa ndani, kwa kukutana na Kristo Yesu, Lango kuu la imani, matumaini na mapendo. Kumbe, maadhimisho ya Jubilei, yanapata chimbuko lake katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ambaye ndiye chimbuko la lengo halisi la imani ya Kikristo. Rej. Yn 10: 7-9. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ushiriki na utume. Kwa kujikita katika hekima na busara, chemchemi ya unyenyekevu, upendo, imani, furaha ya kweli na msamaha kutoka katika undani wa mwamini. Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha moyo wa sala, tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Jubilei kuu 2025
07 January 2025, 16:03