Askofu Msaidizi Renato Tarantelli Baccari wa Jimbo kuu la Roma alizaliwa tarehe 15 Aprili 1976 Jimbo kuu la Roma. Askofu Msaidizi Renato Tarantelli Baccari wa Jimbo kuu la Roma alizaliwa tarehe 15 Aprili 1976 Jimbo kuu la Roma.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Uongozi Ndani ya Kanisa Ni Huduma Kwa Watu wa Mungu

Askofu Msaidizi Renato T. Baccari wa Jimbo kuu la Roma alizaliwa tarehe 15 Aprili 1976. Baada ya masomo yake ya Kikasisi, tarehe 28 Oktoba 2017 akapewa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa ajili ya Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 22 Aprili 2018 akampatia daraja takatifu ya Upadre. Na ilipogota tarehe 21 Novemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu Msaidizi Jimbo kuu la Roma na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 4 Jan. 2025.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mataguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kanisa hili la Kristo, Kuhani Mkuu wa Roma, aliye mwandamizi wa Mtakatifu Petro, ambaye Kristo Yesu alimkabidhi kondoo na wanakondoo wake ili awachunge, kwa agizo la kimungu amepokea mamlaka ya juu kabisa, kamili, inayojitegemea na ya jumla kwa uangalizi wa roho za watu (curam animarum). Hivyo yeye, kwa kuwa amewekwa kuwa mchungaji wa waamini wote, ili kukuza manufaa ya wote ya Kanisa zima, na pia ya Makanisa pekee, Baba Mtakatifu anashika mamlaka ya juu ya kawaida juu ya Makanisa yote. Vilevile na Maaskofu, waliowekwa na Roho Mtakatifu kuwa waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu, na, pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya madaraka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo, Mchungaji wa milele, kwa sababu Kristo Yesu aliwapa Mitume na waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha Mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga.

Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo
Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo

Kwa hiyo, kwa njia ya Roho Mtakatifu, ambaye wao walipewa, Maaskofu ndio waliofanywa Walimu kweli na halisi wa imani, Makuhani na Wachungaji. Maaskofu, wakishiriki katika kuyahangaikia Makanisa yote, wanatimiza huduma na majukumu yao ya kiaskofu waliyopokea kwa kuwekwa wakfu, katika ushirika na chini ya mamlaka ya Baba Mtakatifu, katika yote yahusuyo Ualimu na Uongozi wa kichungaji, wote wakiwa wamoja katika urika au mwili, kwa ajili ya Kanisa zima. Maaskofu, kila mmoja kati yao, wanatimiza huduma hiyo kwa ajili ya sehemu za kundi la Bwana zilizokabidhiwa kwao kwa kuwa waangalifu juu ya Kanisa faridi ambalo kila mmoja alikabidhiwa. Lakini inawezekana pia kwamba Maaskofu wengine wasaidie kwa pamoja mahitaji yahusuyo Makanisa mbalimbali. Rej Christus domini, 2.

Askofu anawekwa wakfu ili kuogoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu
Askofu anawekwa wakfu ili kuogoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu

Ni katika muktadha huu, Monsinyo Renato Tarantelli Baccari wa Jimbo kuu la Roma, Jumamosi jioni tarehe 4 Januari 2025 amewekwa wakfu kuwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Roma, Ibada ambayo imehudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Christoph Schönborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu Vienna, Austria pamoja na Askofu Msaidizi Michele Di Tolve, wa Jimbo kuu la Roma. Askofu Msaidizi anateuliwa kwa ajili ya madai mema ya roho za watu, hivyo wanapaswa kutenda kadiri ya matakwa ya Askofu Jimbo, kwa kuonesha utii na heshima kwa Askofu Jimbo; naye kwa upande wake awaheshimu kama ndugu zake. Rej. Christus domini, 25. Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko alimweka wakfu Monsinyo Renato Tarantelli Baccari kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Roma.

Viongozi wa Kanisa wawe ni vyombo vya huruma na matumaini
Viongozi wa Kanisa wawe ni vyombo vya huruma na matumaini

Kardinali Baldassare Reina, katika mahubiri yake ameongozwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu yasemayo “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Yn 1:29. Amesema, watu wa Mungu bado wamesheheni furaha ya kipindi cha Noeli na maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo, mwaliko kwa watu wa Mungu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini. Imekuwa ni fursa pia ya kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko, kielelezo cha umoja na mapendo. Yohane Mbatizaji ni shuhuda wa kwanza wa kimisionari, aliyemtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Mchungaji mkuu anapaswa kufanana na Kristo Yesu kwa maneno na matendo yake, anayeliongoza kwa njia ya huduma makini kwa watu wa Mungu. Ni kiongozi anayewaonesha njia waamini kuweza kuutafakaru Uso wa huruma ya Mungu na hatimaye kuwaongoza katika maisha na uzima wa milele.

Maaskofu wanatumwa kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu
Maaskofu wanatumwa kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu

Pili, Kiongozi wa Kanisa anapaswa kutoa mwito wa kumfuasa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kumfuasa Kristo Yesu ni sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani ambao kimsingi ni endelevu. Ni katika muktadha huu, Askofu anaitwa na kutumwa kuwa ni shuhuda wa imani, matumaini na mapendo thabiti. Maaskofu wanapaswa kuwa ni mahujaji wasiochoka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Tatu, Maaskofu wanaalikwa kukaa na Kristo Yesu, katika tafakari ya kina ya Neno la Mungu, ili waweze kujichotea neema na nguvu ya kusamehe watu dhambi zao, tayari kuzaa matunda ya utakatifu wa maisha. Kukaa na Kristo kuna maanisha ya kuwaongoza watu wa Mungu katika sala, ili waweze kupata utimilifu wa maisha. Tatu, Kiongozi wa Kanisa anapaswa kuwa ni shuhuda amini wa huruma na upendo wa Mungu, mtu asiye choka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, tayari kuwarutubisha watu wa Mungu kwa Neno na Sakramenti za Kanisa.

Mahujaji wa matumaini, imani na mapendo
Mahujaji wa matumaini, imani na mapendo

Tukio hili la kumweka wakfu Askofu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kujenga na kudumisha ushirikiano na umoja katika imani na Askofu, tayari kujizatiti kikamilifu katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia mintarafu mwanga na tunu msingi za Kiinjili. Kutangaza, kumfuasa na kushinda pamoja na Kristo Yesu ni mwaliko kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anaishi vyema wito wake wa Kikristo na hivyo kuendelea kupyaisha maisha na utume wake. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma. Kumbe, Uaskofu ni huduma makini kwa watu wa Mungu.

Maaskofu wanaitwa na kutumwa kuongoza, kufundisha na kutakatifuza
Maaskofu wanaitwa na kutumwa kuongoza, kufundisha na kutakatifuza

Mwishoni mwa mahubiri yake, Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, amewaalika watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, kusali na kumwombea Askofu Msaidizi Renato Tarantelli Baccari, ili awe na uwezo wa kumwonesha Kristo Yesu, ili watu waaminifu wa Mungu waweze kumfuasa kwa uaminifu na ari kuu, ili waendelee kubaki ndani ya Kristo Yesu. Na kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, aweze kuwaongoza watu wa Mungu kwenye chemchemi ya maisha ya uzima wa milele, ili Kanisa linalosafiri hapa duniani liendelee kuwa ni Sakramenti ya wokovu na shuhuda amini wa huruma na upendo wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Askofu Msaidizi Renato Tarantelli Baccari wa Jimbo kuu la Roma alizaliwa tarehe 15 Aprili 1976 Jimbo kuu la Roma. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 28 Oktoba 2017 akapewa Daraja Takatifu ya Ushemasi wa mpito kwa ajili ya Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 22 Aprili 2018 akampatia daraja takatifu ya Upadre. Na ilipogota tarehe 21 Novemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu Msaidizi Jimbo kuu la Roma na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 4 Januari 2025 kwenye Kanisa kuu la Yohane wa Laterano, Jimbo kuu la Roma.

Uongozi ni Huduma
05 January 2025, 11:20