Papa Francisko katika malezi na makuzi ya kipadre zingatieni: Majadiliano Ushirika na Utume wa Mama Kanisa kwa watu wa Mungu. Papa Francisko katika malezi na makuzi ya kipadre zingatieni: Majadiliano Ushirika na Utume wa Mama Kanisa kwa watu wa Mungu.  (Vatican Media)

Papa Francisko Zingatieni Yafuatayo: Majadiliano, Ushirika na Utume wa Mama Kanisa

Katika hotuba yake, amegusia: Umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayosimikwa katika hija ya maisha ya kiroho, kwa kujenga utamaduni wa kusikilizana na kumsikiliza Roho Mtakatifu; kwa kufanya mang’amuzi ya pamoja, ili kujenga ushirika na hatimaye, waweze kuwa ni wafuasi Mitume, kwa kukubali kupokea changamoto za Uinjilishaji na kuzitafutia ufumbuzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho haya ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau.

Papa Francisko akutana na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Wamarekani Roma
Papa Francisko akutana na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Wamarekani Roma

Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi katika ngazi ya Kimabara ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Watu wa Mungu kutoka katika Chuo cha Kipapa cha Wamarekani mjini Roma. Katika hotuba yake, amegusia maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa chao kunako mwaka 2015, Umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayosimikwa katika hija ya maisha ya kiroho, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana na kumsikiliza Roho Mtakatifu; kwa kufanya mang’amuzi ya pamoja, ili kujenga ushirika wa watu wa Mungu na hatimaye, waweze kuwa ni wafuasi Mitume, kwa kukubali kupokea changamoto za Uinjilishaji na kuzitafutia ufumbuzi. Hii ndiyo dhamana na wajibu unaowasubiri wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Marekani. Mambo msingi wanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na mchakato wa majadiliano na Kristo Yesu, utakaowawezesha kwenda na kuona mahali anapoishi Kristo Yesu, ili kuonja ndani mwake: imani, matumaini na mapendo. Majadiliano na Kristo Yesu yananogeshwa na: sala, Tafakari ya Neo la Mungu, Kweli za Kiinjili na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kufikiri na kutenda kwa ujasiri, ili kumhudia Kristo Yesu pamoja na waja wake kwa ukarimu na moyo mkuu.

Mambo msingi ya kuzingatia: Majadiliano, Ushirika na Utume
Mambo msingi ya kuzingatia: Majadiliano, Ushirika na Utume

Malezi na majiundo ya Kipadre yanalenga kuimarisha ushirika na Mwenyezi Mungu, Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake; wajitahidi kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kanisa kwa kuzingatia kiini cha Kanisa na tofauti zake msingi; na kuendelea kujikita katika Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi, ili kudumisha upendo wa kidugu na utakatifu wa maisha, kwa kushikamana katika kukabiliana na changamoto pamoja na kuvumilia maudhi ya maisha ya kijumuiya kwa kushikamana na upendo wa Kimungu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rej. Evangelii gaudium, 92. Watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kusikiliza na kujibu kwa ufasaha matamanio yao halali, ili kuwaamshia tena watu wa Mungu matumaini mapya, kwa kuendelea kupyaisha maisha, tayari kutoka na kwenda kutangaza Injili ya upendo inayosimikwa kwenye matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya maandalizi yao ya huduma ya Kipadre kwa siku za usoni. Lengo ni kushirikishana na watu wa Mungu uwepo wao angavu, huruma na upendo wa Kristo. Baba Mtakatifu ameiweka Jumuya Chuo Kikuu cha Kipapa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili Mlinzi na Mwombezi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wamarekani ambaye pia ni Mtu anayeheshiwa sana nchinii Marekani.

Papa Marekani

 

14 January 2023, 16:45