Matendo ya Huruma Kiroho na Kimwili Ni Dira Na Mwongozo wa Maisha ya Wakristo: Hukumu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea: Makardinali, Mapatriaki, Maaskofu wakuu na Maaskofu waliofariki dunia kuanzia tarehe 5 Januari 2022 hadi tarehe 17 Oktoba 2022, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hawa ni viongozi waliojisadaka kwa ajili ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Sasa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amewaita kwenye makao ya uzima wa milele kwani yote yamekamilika, “Consummatum est.” Mama Kanisa katika kipindi cha Mwaka 2021-2022 amepoteza viongozi 157 kwa kufariki dunia. Kati yao kuna Makardinali na Mapatriaki 9. Kanisa Barani Afrika limewapoteza Maaskofu 18 na Kardinali mmoja. Ibada ya kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaombea Waamini Wote Marehemu inapata chimbuko lake katika asili ya mwanadamu. Kumbukumbu hii inanogeshwa na Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Rej. Kol 1:18. Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanajiunga na Kristo Yesu na kuanza kutembea katika mwanga wa Pasaka. Rej. Rum 6:3-4. Huu ni ushirika na Kanisa ambalo bado linasafiri huku bondeni kwenye machozi na watakatifu wa mbinguni. Rej. LG 49.
Hii ni kumbukumbu ya umati mkubwa wa ndugu, jamaa na marafiki walioshiriki kikamilifu katika hija ya maisha ya hapa duniani, lakini leo hii hawapo tena! Kumbukumbu ya marehemu wote ilianza kushika kasi kwenye Monasteri na nyumba za kitawa kunako Karne VII na hivyo kuanza kuadhimishwa rasmi tarehe 2 Novemba, baada ya kuadhimisha Sherehe ya Watakatifu wote, hapo tarehe Mosi Novemba. Alikuwa Papa Benedikto XV kunako tarehe 10 Agosti 1915 katika Katiba ya Kitume ya “Incruentum Altaris sacrificium” alipotoa ruhusa kwa Mapadre kuweza kuadhimisha Misa tatu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Waamini Wote! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amejikita katika Injili ya Mathayo 25: 31-41 kuhusu hukumu ya mwisho na jinsi ambavyo waamini wanapaswa kujiandaa kushiriki katika Karamu ya watu wote, Mwenyezi Mungu atafuta machozi katika nyuso zao zote na kwamba, Mungu atakuwa ni chemchemi ya matumaini, furaha na wokovu wa watu wake. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanampokea Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni mashuhuda, watoto na warithi wa Mungu; warithio pamoja na Kristo Yesu na kwamba, wanatarajia kwa matumaini utukufu utakaofunuliwa, changamoto na mwaliko kwa waamini kuitamani mbingu, huku wakikaza macho yao kuelekea juu mbinguni na kamwe wasitake kubweteka kwani watajikuta wakiwa wamemezwa na malimwengu.
Utajiri, mali na mafanikio mbalimbali katika maisha ni mambo ya mpito na wala si hatima ya maisha ya mwanadamu. Waamini wajiweke tayari kumlaki Bwana atakapokuja mawinguni, kama Mama Kanisa anavyosadiki na kufundisha “Nangojea na ufufuko wa wafu. Na uzima wa milele.” Waamini wakiwa hapa duniani, wahakikishe kwamba, wanazingatia mambo msingi katika maisha, hii ikiwa ni pamoja na kunogesha matumaini. Wakristo wazingatie matendo ya huruma kimwili na kiroho ili kuzama zaidi katika kiini cha Injili pale ambapo maskini wanaonja kwa namna ya pekee upendo na huruma ya Mungu. Matendo ya huruma ya kimwili ni: kulisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuwaponya wagonjwa, kuwatembelea wafungwa na kuzika wafu. Na matendo ya huruma kiroho ni: kuwashauri walio mashakani, kuwafunza wajinga, kuwaonya wadhambi, kuwafariji waliojeruhiwa, kusamehe maovu, kuchukuliana kwa saburi na wale wanaowatendea maovu, na kuwaombea walio hai na wafu. Waamini siku ya mwisho watahukumiwa ikiwa wamewalisha wenye njaa, na kuwanywesha wenye kiu, kuwakaribisha wageni na kuwavika walio uchi au kuwatembelea wagonjwa na wale walio kifungoni (Rej. Mt 25:31-45).
Zaidi ya hayo, wataulizwa ikiwa kama wamewasaidia wengine kuepuka wasiwasi unaowafanya wakate tamaa na ambao ndio chanzo cha upweke; kama wamesaidia kuushinda ujinga ambao mamilioni ya watu wanauishi, hasa watoto ambao wamenyimwa mambo msingi ya kuwatoa katika vifungo vya umaskini; ikiwa kama wamekuwa karibu na walio pweke na waliodhulumiwa; kama wamesamehe wale waliowakosea na kama wamekataa aina zote za hasira na chuki zinazosababisha ukatili; kama wamekuwa na ule uvumilivu ambao Mungu anawaonesha, ambaye anawavumilia sana; na kama wamewakabidhi ndugu zao kwa Mungu katika sala. Ndani ya kila mmoja wa hawa “wadogo,” Kristo Yesu mwenyewe yu hai. Mwili wake unadhihirika ndani ya wale waliojeruhiwa, waliopondwa, waliokandamizwa, wenye utapiamlo, na walio uhamishoni na ugenini ili wapate: kuguswa, kutunzwa na kuhudiwa vyema. Mtakatifu Yohane wa Msalaba: “Tunapojiandaa kuyaacha maisha haya, tutahukumiwa kwa kigezo cha upendo.” Baba Mtakatifu anakaza kusema, waamini wajifunze kupenda bila kutazamia malipo. Huu ni mwaliko wa kukesha kwa imani na matumaini ili kumngoja Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu.
Maneno ya Injili yanapaswa kupewa uzito unaostahili: Kuwalisha wenye njaa, kuwasaidia maskini sanjari na kuendelea kujizatiti katika kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu ni dhamana nyeti, ambayo haipewi kipaumbele cha kwanza katika vyombo vya mawasiliano ya jamii au hata katika medani za kisiasa. Wakristo wanapaswa kumwilisha ujumbe wa Injili katika uhalisia wa maisha yao. Maswali mazito kuhusu maisha ya mwanadamu yametundikwa juu ya Msalaba, kati ya watu maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa haina budi kung’ara zaidi kwa kuiga mfano wa Msamaria mwema, shahidi amini wa Injili ya upendo, yaani Mkristo anapaswa kuwa ni moyo unaoona na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani yake. Baba Mtakatifu anasema, huu ndio wakati uliokubalika wa kuhakikisha kwamba, waamini wanamwilisha katika maisha na utume wao matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Fumbo la kifo, liwakumbushe waamini kufanya tafakari kuhusu maisha yao na kuendelea kujikita katika matendo ya huruma, kama njia muafaka ya kusubiri ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu, siku ile watakapoitupa mkono dunia, tayari kuungana na Mwenyezi Mungu anayejifunua kati ya maskini na wale waliojeruhiwa sehemu mbalimbali za dunia. Ni wakati wa matendo na wala si wa maneno matupu ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa!
