Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza wajumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza wajumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. 

Papa Francisko Simameni Kidete Kulinda: Utu, Heshima Na Haki Msingi za Binadamu

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kulitafakari zaidi Fumbo la Umwilisho na hivyo kujitahidi kuwa ni Wasamaria wema, katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Wawe ni Wasamaria wema wakati binadamu anapopata mafanikio, nyakati za furaha na matumaini; wakati wa shida, majonzi na mahangaiko yake ya ndani. Utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ulimwengu mamboleo unahitaji, kuliko wakati mwingine wowote kutambua na kuenzi utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamepelekea madhara makubwa katika mtindo wa maisha ya kijamii na kiuchumi, kwa kuonesha uadhaifu mkubwa wa binadamu. Hili ni gonjwa ambalo limevuruga mahusiano na mafungamano ya kijamii katika ngazi mbalimbali za maisha; mtindo wa utendaji wa kazi umebadilika kwa kiasi kikubwa. Maisha ya kijamii yamejikuta yakiwa njia panda, kiasi hata cha taratibu za maadhimisho ya Ibada na Sakramenti za Kanisa kubadilishwa kwa kusoma alama za nyakati. Swali msingi ambalo waamini wanapaswa kujiuliza ni kuhusu Mwenyezi Mungu na uwepo wa mwanadamu! “Utu wa binadamu unahitajika” ndiyo kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kuanzia tarehe 5 Novemba 2021 na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akahitimisha kwa ujumbe wake kwa njia ya video tarehe 23 Novemba 2021.

Kipindi hiki kigumu katika historia ya mwanadamu kinahitaji si tu sera na mikakati ya kiuchumi, dawa mpya za kupambana na UVIKO-19, bali pia utu mpya unaofumbatwa katika Ufunuo wa Mungu katika Maandiko Matakatifu na kuboreshwa na amana, utajiri wa Mapokeo ya Kanisa bila kusahau tafakari zinazopatikana katika tamaduni mbalimbali za watu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kulitafakari zaidi Fumbo la Umwilisho na hivyo kujitahidi kuwa ni Wasamaria wema, katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Wawe ni Wasamaria wema wakati binadamu anapopata mafanikio, nyakati za furaha na matumaini; wakati wa shida, majonzi na mahangaiko yake ya ndani. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yamepelekea mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kiasi cha kuanza kumfikiria mwanadamu ni nani? Na nini maana ya kuwa mwanadamu katika hali yake nzima yaani katika umoja wa mwili na roho, wa moyo na dhamiri; wa akili na utashi. Ni katika hali na mazingira kama haya, Kanisa bado lina mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika ulimwengu mamboleo, kama ambavyo inafafanuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwenye “Hati ya Gaudium et spes” yaani Kanisa katika Ulimwengu mamboleo.

Kanisa halina budi kuyapembua na kuyapima mambo kwa mizani ya imani na ujasiri; kwa kuangalia kwa makini mafanikio ya kiakili, maisha ya kiroho na vitu. Kumbe, Mama Kanisa anahitaji nguvu za ubunifu zinazotekelezwa katika matendo. Yote haya yanaonesha ile nguvu ya kufikiri na kuzalisha; nguvu ya kuzaliwa na kuitupa mkono dunia. Hapa kuna haja pia ya kuangalia mahusiano kati ya binadamu na mazingira nyumba ya wote pamoja uhusiano uliopo kati ya binadamu na mashini. Mama Kanisa anapenda kujitambulisha na ubinadamu ulimwenguni mintarafu mwanga wa Mapokeo, ili aweze kuwa kweli ni mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; mjenzi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kukazia mshikamano wa udugu wa kibinadamu, huruma na mapendo. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza wajumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu muumbaji wa vyote; binadamu na utambulisho wake. Je, leo hii binadamu katika mahusiano na mafungamano yake ya kijamii anaona kwamba, tofauti msingi kati ya Bwana na Bibi ni sehemu muhimu katika kukamilishana katika mafungamano yao ya kijamii? Je, maneno, “Baba” na “Mama” yana maana gani? Je, kuna tofauti gani msingi kati ya binadamu a mnyama?

Binadamu anapata wapi nguvu inayomsukuma kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii? Maandiko Matakatifu yanaonesha mambo msingi katika anthropolojia ya binadamu na mahusiano yake na Mwenyezi Mungu. Chanzo na asili ya binadamu pamoja na hatima yake hapa duniani, imefafanuliwa vyema katika Biblia Takatifu na kwenye hekima za wahenga. Kumbe, kuna tamaduni ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuleta uwiano, amani na utulivu kati ya binadamu na mazingira nyumba ya wote; mshikamano wa udugu wa kibinadamu; familia na sherehe za kijamii pamoja na mwono wa maisha ya Kikristo ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake anagusia kuhusu mgogoro na matokeo ya fikra mpya ya mwanadamu akisema, wanadamu waposhindwa kuiona nafasi yao halisi katika ulimwengu, wanajikuta hawajielewi na wanaishia kufanya mambo dhidi yao wenyewe. Rej. Laudato si , 115. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video akisema kwamba, ulimwengu mamboleo unahitaji, kuliko wakati mwingine wowote kutambua na kuenzi utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo.

Utu wa Binadamu

 

29 November 2021, 15:11