Kipindi Cha Kazi ya Uumbaji 2021: Umoja na Mshikamano wa Kiekumene
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Siku ya VII ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira imeadhimishwa tarehe 1 Septemba 2021 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake” Zab 24:1. Je, kweli hii ni nyumba ya wote? Siku hii ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015 kama sehemu ya mchakato endelevu na fungamani wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba ni Kipindi cha Kazi ya Uumbaji. Matukio kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika Kipindi cha Kazi ya Uumbaji, yanapania pamoja na mambo mengine: Kufafanua na kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu taalimungu ya kiikolojia. Lengo ni kudumisha ukweli kuhusu utu, heshima ya binadamu, haki msingi pamoja na uelewa wa kazi ya uumbaji kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Kazi ya uumbaji iliyokuwa nzuri machoni pa Mwenyezi Mungu na kuikabidhi kwa binadamu kama zawadi imeharibiwa sana kutokana na: Dhambi, ubinafsi na uchoyo unaotaka kuinyonya kwa uchimbaji wa madini na nishati ya mafuta; kilimo cha mashamba makubwa pamoja na uchomaji na ukataji ovyo wa misitu hali ambayo imesababisha kupanda kwa joto duniani pamoja na kuongezeka kiwango cha bahari, kiasi cha kutishia Injili ya uhai. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira unaofanywa kwa kutupa ovyo taka za plastiki; mambo yanayotishia usalama wa maisha ya viumbe hai duniani. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 1 Septemba 2021, amesema, hiki ni kipindi maalum cha kupyaisha “οίκος ya Mungu” yaani “Mazingira nyumba ya Mungu au kazi ya Uumbaji”. Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli pamoja na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani wanaandaa Waraka wa Kiekumene unaotarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia sasa. Lengo ni kuendelea kusali na kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote pamoja na kushirikiana kwa ajili ya kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote.