Bunge la Jumuiya ya Umoja wa Ulaya tarehe 29 Septemba 2021 limejadili kuhusu mazingira na haki msingi za binadamu: haki ya usalama, afya bora na mazingira endelevu. Bunge la Jumuiya ya Umoja wa Ulaya tarehe 29 Septemba 2021 limejadili kuhusu mazingira na haki msingi za binadamu: haki ya usalama, afya bora na mazingira endelevu. 

Papa: Mazingira na Haki Msingi za Binadamu: Usalama na Afya Bora!

Papa Francisko anasema, mazingira ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kutunzwa, kulindwa na kuendelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, afya bora inakwenda sanjari na mazingira bora, kumbe kuna haja ya kutunza mazingira kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya afya ya binadamu. Uzuri wa mazingira uheshimiwe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Bunge la Jumuiya ya Umoja wa Ulaya katika mkutano wake, huko Strasbourg, Ufaransa, Jumatano tarehe 29 Septemba 2021 limejadili kuhusu mazingira na haki msingi za binadamu: haki ya usalama, afya bora na mazingira endelevu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Wabunge hawa amesema, mazingira nyumba ya wote ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kutunzwa, kulindwa na kuendelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, afya bora inakwenda sanjari na mazingira bora, kumbe kuna haja ya kutunza mazingira kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya afya ya binadamu. Uzuri wa mazingira usiokuwa na kifani ni changamoto ya kusimama kidete kuyalinda mazingira na kuyatumia kwa heshima zaidi. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anapenda kuunganisha athari za uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kijamii; vita na kinzani; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi pamoja na baa la umaskini linalopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Anasema lengo la Waraka huu wa Kitume ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaunda mfumo wa uchumi na masuala ya kijamii yanayokita misingi yake katika haki, heshima na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza.

Mkutano wa Bunge la Jumuiya ya Umoja wa Ulaya unafanyika kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scottland, kuanzia tarehe Mosi Novemba hadi tarehe 12 Novemba 2021. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya itaweza kutoa mchango wake mkubwa ili kufanikisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ili kuweza kufikia malengo haya, kuna haja ya kuunda chombo cha kisheria ili kutekeleza maazimio yatakayofikiwa kwa kuzingatia utunzaji bora wa mazingira na haki msingi za binadamu! Hakuna tena muda wa kupoteza katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Kila fursa inaweza kutumiwa vyema ili kukabiliana na changamoto hii, kwa kukazia: umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, demokrasia, utawala wa sheria pamoja na tunu msingi za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Kila mtu anapaswa kuishi kwa heshima na kupewa nafasi ya kujiletea maendeleo endelevu.

Pale ambapo binadamu anageuka kuwa ni mtawala wa kazi ya uumbaji na kuanza kuchafua na kuharibu mazingira nyumba ya wote anakuwa ni chanjo cha majanga makubwa katika maisha yake. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo pamoja na mtazamo mpya kuhusu ulaji, ili kuokoa mazingira nyumba ya wote. Jumuiya Kimataifa isikilize na kujibu kilio cha Maskini na Dunia Mama, ili kuweka uwiano mzuri kati ya binadamu, mazingira na Mwenyezi Mungu, Muumba wa vyote! Uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote ni janga linalogusa masuala ya kijamii na linahitaji majadiliano ya kina, uwajibikaji wa kila mtu na jamii katika ujumla wake, ili waweze kuwa na afya bora kwa kuishi katika mazingira bora na fungamani kwa maisha ya binadamu. Haki na wajibu ni sawa na chanda na pete anasema Baba Mtakatifu Francisko. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Bunge la Jumuiya ya Ulaya litaweza kutoa sera na mikakati itakayosaidia  kuboresha mazingira nyumba ya wote. Haya ni maamuzi magumu yanayopaswa kutekelezwa kwa matumaini, ujasiri na utashi wa kisiasa kwa sababu yanapania kulinda mazingira nyumba ya wote, utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Bunge la Ulaya

 

29 September 2021, 16:46