2025.10.17 Marina di Ostia - Visita alla Nave-Scuola della Pace "Med 25 Bel Espoir" 2025.10.17 Marina di Ostia - Visita alla Nave-Scuola della Pace "Med 25 Bel Espoir"  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 19 ya Mwaka A: Imani Thabiti Katika Dhoruba

Liturujia ya Neno la Mungu inatutafakarisha juu ya, “Imani thabiti kwa Mungu katikati ya dhoruba za maisha.” Katika safari yetu ya maisha hapa duniani, tunakutana na mawimbi na dhoruba za kila aina. Mungu hatuachi peke yetu, bali anajidhihirisha katikati yetu, akitualika tumtazame yeye kwa imani na matumaini thabiti. Yeye anasafiri daima pamoja na Kanisa lake, akitupa nasi nguvu na imani thabiti ya kushinda hofu na mashaka yote tutakayokutana nayo kila siku!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa familia ya Mungu, ni Dominika ya 19 mwaka A wa Kanisa. Liturjia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “Imani thabiti kwa Mungu katikati ya dhoruba za maisha.” Katika safari yetu ya maisha hapa duniani, tunakutana na mawimbi na dhoruba za kila aina. Mwenyezi Mungu hatuachi peke yetu, bali anajidhihirisha katikati yetu, akitualika tumtazame yeye kwa imani na matumaini thabiti. Yeye anasafiri daima pamoja na Kanisa lake, akitupa nasi nguvu na imani thabiti ya kushinda hofu na mashaka yote tutakayokutana nayo kila mmoja katika ufuasi wetu. Tuombe neema ya kutambua na kukiri nguvu ya Kristo na kuruhusu yeye ayaongoze daima maisha yetu. Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 14:22-33. Katika somo la Injili Takatifu dominika iliyopita, Kristo alifanya muujiza wa kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Kristo anafanya muujiza mwingine katika dominika hii ya 19, ambapo anatembea juu ya maji na anakemea upepo na dhoruba. Kwa nini Kristo alifanya miujiza? Miujiza hii mbalimbali aliyoifanya Kristo Yesu ilikua kimsingi na na lengo la kuwaimarisha mitume na wafuasi wake imani yao. Muujiza huu wa kutembea juu ya maji ni uthibitisho kwa wanafunzi wake na wakristo wa kwanza kwamba Yesu Kristo ni Mungu, mwenye nguvu na uweza juu ya dhoruba na hofu zote za mwanadamu. Hebu tulitazame kwa kina somo hili la Injili Takatifu na kuona jinsi gani linatusaidia kuelewa vyema ujumbe ambao Mama Kanisa amependa kututafakarisha katika dominika hii ya 19A.

Kanisa ni Sakramenti ya Umoja na Wokovu wa watu wote

Kanisa ni Sakramenti ya Umoja na Wokovu wa watu wote   (@Vatican Media)

Fundisho la Kwanza: Katika safari yetu ya maisha, tutakutana na mawimbi na dhoruba za kila namna, ndiyo majaribu mbalimbali dhidi ya imani yetu. Katika somo hili la Injili Takatifu, Mwinjili Mathayo anatueleza mwanzoni kabisa katika aya hii ya 22 kwamba, “Yesu aliwalazimisha mitume wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano” Kristo alifahamu kabisa kwamba mitume wake watakutana na changamoto na hali mbaya ndani ya bahari (kutokana na uhalisia wa kijiografia wa bahari ya Galilaya, ambapo upepo wa ghafla hasa nyakati za usiku ulikua ni jambo la kawaida). Lakini bado akawalazimisha Mitume wapande chomboni na kuvuka kwenda ng’ambo ya pili. Ndugu mpendwa, Mwinjili Mathayo hapa anazungumzia mazingira ya kawaida ya bahari ya Galilaya lakini ndani yake akitoa fundisho kubwa sana la kitelojia juu ya Kanisa na utume wa mitume wa Kristo hasa katika nyakati ngumu katika karne ile ya kwanza na kuendelea hata wakati wetu wa sasa. Chombo hiki anachokizungumzia Mathayo, kimsingi ndilo Kanisa ambalo Kristo aliwaachia mitume wake baada ya kupaa kwenda kwa Baba. Bahari hii yenye upepo na dhoruba ndiyo ulimwengu, ambapo Kanisa linasafiri kwa nyakati mbalimbali mpaka Kristo ataporudi tena. Ni wazi kuanzia ile karne ya kwanza, Kanisa lilikua likipitia majaribu, upinzani, mateso na madhulumu mengi na mitume wengi waliteseka, walidhulumiwa, na kufa kwa sababu ya imani yao. Ndivyo imekua kwa nyakati mbalimbali katika historia ya Kanisa hata sasa. Sisi nasi ndio hao Mitume na Wakristo wa Kanisa la leo. Kanisa ni chombo cha wokovu kinachosafiri katika bahari ya ulimwengu huu wa sasa, kueleka ng’ambo ya pili yaani mbinguni. Kristo ametuita, na ametutuma tupande chomboni, tusafiri na tuvuke. Katika safari yetu hii, tutateseka, tutajaribiwa kwa namna nyingi, tutaumia, tutatukanwa na kudharauliwa, tutabeba misalaba yetu, tutakutana na magonjwa, tutakutana na dhoruba za kila aina za maisha yetu, huo ndio uhalisia wa ulimwengu ambapo Kanisa, linasafiri nasi tukiwa ndani yake.

Katika dhoruba za maisha, waamini wamkimbilei Kristo Yesu

Katika dhoruba za maisha, waamini wamkimbilei Kristo Yesu   (@VATICAN MEDIA)

Fundisho la Pili: Ni dhahiri kwamba kumfuata Kristo hakutuondolei majaribu na dhoruba za maisha. Tuombe neema ya kubaki ndani ya Kanisa na kuepuka kishawishi cha kukimbilia vyombo vingine. Je bado nipo chomboni? Ndugu mpendwa, ni wazi kabisa kwamba hakuna Ukristo na ufuasi wa bei rahisi ambapo kila mara bahari itakuwa shwari. Kila mmoja katika wito wake, atapitia dhoruba kwa namna mbalimbali, katika ndoa, katika utawa, katika upadre, kama kijana, katika kazi, katika biashara zako, katika uongozi, tutapitishwa wakati fulani katika dhoruba na upepo mkali. Yesu anaruhusu tupite mule mule alimopita yeye. Hiyo ndio njia pekee ya kufika ng’ambo ya pili. Hatupaswi kutoka chomboni, baki ndani ya chombo, baki ndani ya Kanisa, baki katika imani yako, baki ndani ya familia yako, baki ndani ya wito wako, nje hakuna usalama wowote. Mara kadhaa mawimbi yanapokuwa makali sana ndani ya Kanisa au katika maisha ya imani, mwanadamu huingiwa na hofu na kushawishiwa kukimbilia vyombo vingine akidhani vitampa usalama wa haraka badala ya kusubiri muda wa Mungu. Vyombo hivyo vyaweza kuonekana salama sana kwa nje lakini ndani yake Kristo hayupo. Ni rahisi sana kutafuta usalama dhidi ya dhoruba za kidunia katika utajiri, katika mitindo ya kidunia, katika ushirikina, katika madhehebu yanayochipuka kila kukicha yakiahidi maisha yasiyo na dhoruba yoyote, Injili za miujiza na mafanikio ya haraka. Vyombo hivi vinaweza kuonekana imara kwa nje na vyenye kuvutia sana, lakini havina uwezo wa kuhimili dhoruba za kiroho na mwishowe huzama kabisa. Haijalishi tunapitia madhila gani ndani ya imani yetu, hakuna kutoka kwenda popote, tutabaki hapo mpaka zamu ya nne ya usiku, Kristo atakapokuja kutupeleka ng’ambo ya pili.

Boti ni alama ya Kanisa ambacho ni chombo cha wokovu na huruma ya Mungu

Boti ni alama ya Kanisa ambacho ni chombo cha wokovu na huruma ya Mungu   (AFP or licensors)

Fundisho la Tatu: Kristo, Mwana wa Mungu, anajidhihirisha katikati ya dhoruba na mawimbi ya maisha yetu. Yeye ana nguvu na mamlaka juu ya nguvu na mamlaka zote zinazoweza kutuletea hofu. Baada ya kusafiri na chombo na kufika katikati ya bahari, tunaambiwa chombo kilianza kutaabika sana na mawimbi, kwa kuwa upepo ule ulikuwa wa mbisho, yaani upepo unaovuma dhidi (against) ya chombo, au kutoka upande ule chombo kilipokuwa kikielekea. Katika mazingira yale ya bahari ya Galilaya, upepo wa ghafla wa aina hiyo hasa nyakati za usiku lilikua ni jambo la kawaida. Mwinjili Mathayo anatuambia, “Katika zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari” Kwa nini zamu ya nne ya usiku? Wayahudi kawaida waliugawanya usiku katika zamu kuu nne (zamu ya kwanza saa 12 jioni hadi saa 3 usiku, zamu ya pili saa 3 hadi saa 6, zamu ya tatu saa 6 hadi saa 9 na zamu ya mwisho hii ya nne ilikua ni kuanzia takribani saa 9 alfajiri hadi saa 12 asubuhi. Katika mapokeo ya Biblia, zamu ya nne ndio ule muda wa kilele cha giza unaokaribia mapambazuko. Ni kipindi ambacho nguvu na akili zote za kibinadamu zinakuwa zimeisha kabisa na kukata tamaa kuko karibu. Ndiyo hali walikuwa nayo hawa mitume, licha ya kwamba walikua ni wazoefu wa baharini. Mungu anaingilia kati wakati huu ili kudhihirisha kuwa wokovu hautoki kwa nguvu za mwanadamu bali kwa uwezo wake Yeye pekee.

Wakati wote Kristo Yesu yuko pamoja na waja wake.

Wakati wote Kristo Yesu yuko pamoja na waja wake.   (AFP or licensors)

Mwinjili Marko yeye katika simulizi hili katika sura ile ya 6:48 anasema, “Kristo akiwa mlimani aliwaona mitume namna walivyopambana kupiga makasia kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho.” Ndugu mpendwa, katika mapambano mbalimbali dhidi ya dhoruba tunazokutana nazo katika safari yetu ya maisha, Kristo anatuona. Anatutazama kwa huruma na hawezi kutuacha kamwe tukazama. Yeye yupo mbinguni katika enzi na Utukufu, akituombea kwa Baba. Anatupa nguvu za kuendelea kupiga makasia katika zamu zote, mpaka tutakapofikia mapambazuko. Tukisoma katika Agano la Kale, ni katika zamu hii hii ya nne ya usiku kabla ya asubuhi kuchomoza ambapo Mwenyezi Mungu aliwafuatia Wamisri na kuwazamisha, na kuwaokoa Waisraeli walikuwa wamejikatia tamaa na kujawa na hofu, wavuke Bahari ya Shamu kwa ushindi (Kut 14:24-27).

Maana nyingine kubwa zaidi ni kwamba Kristo alifufuka pia mapema asubuhi, ni katika zamu hii ya nne ya usiku, Kristo anafufuka katika wafu, akidhihirisha ushindi wake dhidi ya dhambi na mauti. Kumbe Injili hii inatufundisha kwamba hata dhoruba ya maisha yetu iwe ndefu kiasi gani, Mwenyezi Mungu ana “Zamu yake ya Nne” ya kuleta majibu, anatuona. Wakati mwingine anasubiri hadi dhoruba ifikie kilele ili muujiza wake ulete utukufu mkubwa zaidi na uimarishe imani yetu kabisa. Kristo anajidhihirisha kwa mitume waliokuwa wamejawa hofu na kuchoka, wakifikiri kuwa wanaona kivuli kwamba, “Ni mimi Msiogope... Egó eimí; mé fobéisthe.”  Huu ni utambulisho wa Mungu kama alivyojitambulisha kwa Musa katika kichaka kilichowaka moto bila kuteketea (Kut 3:4). Hapo wanatambua kuwa Kristo ni Mwana wa Mungu, kwa kuwa ni Mungu pekee alikuwa na uwezo wa kutembea juu ya maji, na dhidi ya nguvu na mamlaka juu ya pepo na dhoruba (Zab 107:29, Ayu 9:8).

Fundisho la Nne: Licha ya kwamba Kristo anajidhihirisha kwetu katikati ya dhoruba, kuna nyakati tunakuwa bado na imani haba na kuacha kumtazama yeye. Hata hivyo, bado anatushika mkono na kutuinua tusizame. Kristo akiisha kuwapa moyo wanafunzi wake kwamba, “Ni mimi msiogope”, Mtume Petro, kiongozi wa mitume anapata ujasiri wa kutembea juu ya maji ili kumfuata Kristo. Lakini anapoona tena mawimbi na dhoruba anajawa hofu na mashaka na kuanza kuzama. Hata hivyo anatambua bado kwamba Kristo yupo karibu, kisha anapiga yowe akisema, “Kristo niokoe” Yesu akanyoosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Ndugu mpendwa, Mtume Petro anasimama badala ya Wakristo ambao wana hamu kubwa ya kumfuata Yesu, lakini wanajikuta wakiyumba na kujaa shaka pindi wanapokutana na matatizo. Petro alipoondoa macho yake kwa Yesu na kutazama upepo mkali na dhoruba, alianza kuzama.

Kumbe hali hii inawakilisha udhaifu wetu wa kibinadamu pale tunaporuhusu mawimbi ya maisha, yatuvunje kabisa moyo kwa kuacha kumtazama Kristo aliye daima katikati yetu. Petro alipoona anazama, alipiga yowe, “Bwana niokoe” Ni sauti inayotuwakilisha sisi sote tulio ndani ya Kanisa, pale tunapoelemewa na dhoruba zetu na kukaribia kukata tamaa na kuanza kuzama, kila mmoja katika safari yake ufuasi kwa Kristo. Kinadhihirisha ukweli kwamba binadamu kwa nguvu zake mwenyewe hawezi kujiokoa, bali anahitaji mkono wa neema wa Yesu Kristo unaonyoshwa kumwokoa wakati wowote anapozama. Tunaalikwa katika dominika hii kila mmoja awe tayari kumwita Kristo. Nguvu, maarifa, akili, uwezo wetu haviwezi kukabiliana na mawimbi makubwa na dhoruba tunazokutana nazo. Tumwelekezee macho yetu kwake tu, dhoruba zisitufunge macho, kelele za ulimwengu zisitufunge mioyo na kuona kwamba Kristo yu mbali sana nasi. Tuamini katika nguvu na uweza, enzi na mamlaka ya Kristo juu ya hofu na mashaka yetu. Tumwite, Bwana, niokoe katika vilema na udhaifu wangu, katika dhambi na uregevu wangu, okoa familia yangu, okoa watoto wangu, okoa vijana wetu, okoa taifa letu, okoa ulimwengu wote unaozama katika mambo ya kidunia na kumsahau Mungu na nafasi yake katika maisha. Pale magonjwa yanapotuandama, misiba, ugumu wa maisha, msongo a mawazo, Bwana, niokoe. Kwa hakika Kristo yupo kutushika mkono, akituuliza, nipo karibu nawe siku zote, katika Neno langu, katika sakramenti, kwa nini unaona shaka?

Imani thabiti kwa Kristo Yrsu hushinda hofu ote

Imani thabiti kwa Kristo Yrsu hushinda hofu ote

Fundisho la Tano: Imani thabiti kwa Kristo hushinda hofu zote. Tumruhusu Kristo aingie ndani ya chombo na atuongoze yeye. Sehemu ya mwisho ya Injili inatupa matokeo ya Mitume kumtambua na kumkiri Kristo kama Mungu, mwenye nguvu na mamlaka juu ya nguvu zote zinazoweza kumtia mwanadamu hofu. Alipoingia tu chomboni, upepo uliloma na matokeo yake yalikuwa ni mabadiliko makubwa ya kiroho ndani ya chombo. Wanafunzi waliacha kuogopa dhoruba na badala yake wakajazwa na hofu ya kimungu (reverence). Sehemu hii ya mwisho ya Injili tunaambiwa, “Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.” (Mt 14:33). Ndugu mpendwa, pale Kristo anapochukua nafasi yake ndani ya chombo, vurugu, hofu, na machafuko ya ulimwengu hayana nguvu tena ya kuendelea kutikisa. Tunapomwalika Kristo aongoze maisha yetu, tuna hakika tutashinda hofu na mashaka yote. Mara nyingi tunapambana na dhoruba za maisha kwa nguvu zetu wenyewe huku tukimwacha Yesu nje au pembeni ya maisha yetu. Je, Kristo ana nafasi gani katika maisha yangu? Je, ninazikabili vipi dhoruba za maisha yangu katika safari yangu ya kiimani? Tuombe neema ya kusafiri daima na Kristo katika familia zetu, ndoa, jumuiya zetu, katika kazi zetu zote za kila siku. tumkabidhi Kristo usukukani ayaongoze maisha yetu. Akiwa nasi, hofu za huko nje hazitatusumbua na kutuvunja moyo.

Kristo Yesu akiwa chomboni, mambo yote ni salama

Kristo Yesu akiwa chomboni, mambo yote ni salama   (2025 Getty Images)

Somo la 1: Ni kitabu cha Kwanza cha Wafalme 19:9a, 11-13a. Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Kwanza cha Wafalme linatupatia simulizi ya Nabii Eliya. Mara baada ya kuwashinda manabii 450 wa uwongo wa Baal katika mlima Karmel, Nabii Eliya alifikiri mambo yangekuwa sasa shwari. Alifikiri watu wangebadilika na kuongoka na kumwabudu tena Mungu wa kweli, Mungu wa Israeli. Lakini haikuwa hivyo. Malkia Jezebel, mke wa Mfalme Ahab, alianza kumtafuta Eliya ili amwue. Nabii Eliya akiwa amejawa na hofu, uchovu na kukata tamaa, alikimbilia jangwani, hata mpaka mlima Horebu. Na huko Mwenyezi Mungu anajidhihirisha kwake katika sauti ndogo ya utulivu. Baadaye atapata tena nguvu ya kuendelea na utume wake. Fundisho la Sita: Nasi tunahitaji muda binafsi kukaa na Mungu, katika sala na ukimya, huko tutapata nguvu tena ya kuanza upya hata kama tulikwishakata tamaa kabisa.

Katika Agano la Kale, ilifahamika kwamba Mwenyezi Mungu alijifunua kwa njia ya moto, radi, au upepo (theophany). Tunaona namna alivyojifunua kwa taifa la Mungu pale mlimani Sinai. Eliya hali kadhalika alifikiri Mwenyezi Mungu angejifunua katika hali hizo, lakini ikawa tofauti kabisa. Mwenyezi Mungu anajifunua katika sauti ndogo ya utulivu. Hii ilikuwa ni ishara na utabiri kwamba, Mwenyezi Mungu sasa ataudhihirisha utukufu wake katika unyenyekevu na upole, katika nafsi ya Mwanaye mpenzi Yesu Kristo. Mungu alitumia sauti ya utulivu kumfundisha Kumbe utukufu wa Mungu unadhihirika si katika vurugu na mabavu bali katika Unyenyekevu na upole, katika nafsi ya Neno wake wa milele Bwana wetu Yesu Kristo.

Lengo la miujiza ya Kristo Yesu ni kuimarisha imani ya wafuasi wake.

Lengo la miujiza ya Kristo Yesu ni kuimarisha imani ya wafuasi wake.   (@Vatican Media)

Ndugu mpendwa, sisi pia tunahitaji kuwa na muda binafsi wa kukutana na Mungu kila mara katika ukimya na faragha. Mwanzoni mwa Injili tunaona pia, Kristo akiisha kuwaaga makutano, alikwenda kusali. Matokeo ya sala ni kupata nguvu za kiroho za kutusaidia tena kwenda kukabiliana na changamoto zetu za maisha ya kila siku. Kuna nyakati tunaweza kuona kila kitu tunachofanya hakina maana tena. Tunaweza kuchoka hata kutamani kufa kama alivyotamana Nabii Eliya. Lakini sala inatusaidia kutoka tukiwa imara na wenye nguvu zaidi kuliko mwanzo. Eliya aliposhuka mlimani alikwenda kumpaka mafuta Elisha, na kumwimarisha kuendeleza kazi ile ya unabii. Kumbe sala hazitusaidii tu sisi, zina manufaa mengi na zinawaimarisha hata wengine ambao nao wapo kwenye mahangaiko na mitihani yao ya maisha.

Somo la Pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 9:1-5. Katika Somo hili la Pili, Mtume Paulo anashangazwa na kusikitishwa na ukweli kwamba Wayahudi walikuwa na kila sababu ya kumpokea Yesu kuliko mataifa mengine, lakini wakafanya kinyume. Anataja baraka zote ambazo Wayahudi walipewa na Mungu na wakashindwa kuzitumia vyema. Wayahudi walishindwa kumtambua na wakamkataa Masiha wao wenyewe alipokuja. Kumbe Paulo anatukumbusha sisi sote kuwa, licha ya kupendelewa hivi na Mungu, tukazaliwa upya ndani ya Kanisa, chombo cha wokovu, na kupewa kila kitu tunachohitaji ili tuupate uzima wa milele, ipo hatari pia ya kujisahau na kuona kama wokovu ni haki yetu. Hitimisho Tuombe neema ya kufanya kila mara jitihada na juhidi thabiti, kumtafuta na kumtambua Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliye daima katikati yetu kama njia pekee ya kutufikisha mbinguni, ulipo utimilifu wa wokovu wetu.

Tafakari D 19 Mwaka 4
08 Agosti 2026, 11:36