2026.08.04 SIGNIS2026:Kardinali Kambanda. 2026.08.04 SIGNIS2026:Kardinali Kambanda. 

Kongamano la Dunia la SIGNIS 2026:Umuhimu wa vyombo vya habari kwa ajili ya uinjilishaji

Changamoto za vyombo vya habari vya kisasa,matumizi ya kimaadili ya teknolojia za kidijitali na akili unde ndio mada iliyoongoza Kongamano la SIGNIS lililowaleta pamoja wataalamu wa mawasiliano na vyombo vya habari kutoka ulimwenguni kote.

Na Angella Rwezaula,Sr Ernestina Patrick Lasway,Sr Michelle Njeri–Kigali, Rwanda

Kongamano la dunia la SIGNIS lililoandaliwa huko Kigali Rwanda liliongozwa na mada: "Mawasiliano ya Kidijitali kwa Uwiano wa Utamaduni na Ustawi wa Mazingira." Kongamano hilo lilifunguliwa Agosti 4 kwa jumbe tofauti za mshikamano, ikiwa ni pamoja na ujumbe kutoka kwa Papa Leo XIV uliosainiwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican, ambao uliwasilishwa na Balozi wa Kitume wa Rwanda, Askofu Mkuu Arnaldo S. Catalan.

Balozi wa Vatican  nchini Rwana akisoma ujumbe wa Papa Leo XIV katika SIGNIS2026
Balozi wa Vatican nchini Rwana akisoma ujumbe wa Papa Leo XIV katika SIGNIS2026

Akirejea katika Waraka wake wa Magnifica Humanitas, Papa Leo XIV alisema: "Mawasiliano ya mtandaoni si upitishaji wa taarifa tu, bali ni uundaji wa utamaduni, kwani una uwezo wa kuunda jinsi watu wanavyouona ulimwengu  na, kwa hivyo, huathiri sana dhamiri ya pamoja.”

Upatanisho, kukuza umoja wa kitaifa na mshikamano

Katika hotuba yake, Kardinali Antoine Kambanda, Askofu Mkuu wa Kigali, na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Rwanda, akirejea mada ya Kongamano alielezea umuhimu wa Vyombo vya Habari kama njia ya mawasiliano na uinjilishaji. Alisisitiza hitaji la kutumia vyombo vya habari kama njia ya uponyaji, upatanisho, kuhamasisha umoja wa kitaifa na mshikamano.

Akirejea fundisho kutokana na Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ya 1994, alielezea juu ya matumizi mabaya ya vyombo vya habari nchini ambayo yalichangia vita. Aliwaalika washiriki kutumia muda wa mkutano huo kutathmini changamoto na madhara ambayo yanaweza kusababishwa na matumizi mabaya ya vyombo vya habari.

Kongamano la SIGNIS Rwanda
Kongamano la SIGNIS Rwanda

Mahali pa mahusiano na mshikamano

Katika ujumbe wake Dk. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano alielezea umuhimu wa kukutana kimwili katika ulimwengu wa kidijitali akibainisha kuwa, "Mikusanyiko kama hii ya ana kwa ana, inatukumbusha jambo ambalo ulimwengu wetu wa kidijitali husahau mara nyingi: kwamba mawasiliano hayaanzii na teknolojia, bali na watu.”

"SIGNIS haipaswi kuwa urasimu wa kikanisa, bali mtandao wa watu, mtandao wa wataalamu wanaoshiriki imani moja. Hapa panapaswa kuwa mahali ambapo mahusiano ya uaminifu yanaanzishwa, taarifa za kweli zinashirikishwa, na mipango mizuri inaundwa," alisema.

Kongamano la Dunia la Signisi Kigali,Balozi wa Vatican akizungumza na Kardinali Kambanda
Kongamano la Dunia la Signisi Kigali,Balozi wa Vatican akizungumza na Kardinali Kambanda

Haja ya mawasiliano kwa ajili ya mshikamano

Bi. Helen Osman Rais wa SIGNIS World,(wa wakati huo) alitoa shukrani kwa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, kwa ushirikiano unaoendelea na SIGNIS. Akitoa wito wa ushirikiano katika roho ya Sinodi alipendekeza kwamba "tunahitaji mtandao imara wa mawasiliano unaoleta mshikamano na umoja wa Kikristo katikati ya shinikizo la kimataifa."

Matunda ya SIGNIS

Fr. Walter Ihejirika, Rais wa SIGNIS Africa,(wa wakati huo) alisisitiza kwamba nguvu ya SIGNIS Africa iko katika uwezo wake wa kuwaleta pamoja mapadre, masista na walei katika roho ya ushirikiano, akibainisha kuwa mtandao huu umekuwa muhimu kwa mafanikio ya shirika. Pia alitoa shukrani kwa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, la Mawasiliano, la Uinjilishaji, pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagaska(SECAM), akisifu kujitolea kwao na kuelezea uwepo wa washiriki katika mkutano huo kama ishara inayoonekana ya roho ya Sinodi ya kutembea pamoja kama Watu wa Mungu.

Katika hotuba yake, Padre Ihejirika pia alitoa wito wa mshikamano mkubwa miongoni mwa mashirika ya vyombo vya habari vya Kikatoliki na ofisi za mawasiliano ya Kanisa ili kwa kufanya kazi pamoja waweze kujenga vyombo vya habari vya Kikatoliki vinavyoaminika vyenye uwezo wa kutumikia Kanisa na jamii ya kisasa. Kongamano la Dunia la SIGNIS 2026 lililoanza tangu tarehe 3 hadi 8 Agosti, liliwaleta pamoja wawasilianaji Wakatoliki kutoka ulimwenguni kote ili kutafakari, kujifunza, kuungana na kujadili masuala yanayoibuka katika mawasiliano. Hii ilikuwa matarajio ya kuimarisha mawasiliano katika utamaduni na maeneo mbalimbali.

SIGNIS:UFUNGUZI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

 

04 Agosti 2026, 16:53