Dkt Nchimbi: Mchango wa Kanisa Katoliki Tanzania Katika Elimu na Afya
Na Ofisi ya Makamu wa Rais, - Dar es Salaam
Waamini walei wanapaswa kuwa ni uti wa mgongo katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Mtakatifu Paulo anawakumbusha Wakristo kwamba, katika maisha yake, alivipiga vita vikuu, imani akailinda. Huu ni mwaliko pia kwa Wakristo wa nyakati hizi kupambana kufa na kupona, ili kulinda, kutetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, wanao mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo ya Kanisa la Kristo na mafao ya wengi. Waamini wawezeshwe kwa kupewa majiundo makini na endelevu ili waweze kushiriki vyema katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wao ni Familia ya Mungu inayowajibika, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya kwanza ya Maaskofu Barani Afrika. Waamini walei wanapaswa kufundwa, kukua na kukomaa, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa, Familia ya Mungu inayowajibika. Waamini walei wanaowajibika ni nyenzo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa na wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanaendeleza maisha na utume wa Kanisa katika maeneo yao, huku wakitambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya Familia ya Mungu inayowajibika.
Makamu wa Rais Dkt Emmanuel Nchimbi wa Tanzania (©Society of Apostles of Jesus in Tanzania, AJ.)
Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS., wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Tanzania, Jumamosi tarehe 8 Agosti 2026 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, maalum kwa Wanajumuiya wa Uru Seminari, iliyoadhimishwa kwenye Parokia ya Kristo Mchungaji Mwema, Tabata Kimanga, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Askofu Joseph Mlola katika mahubiri yake kwa Wanajumuiya wa Uru Seminari, amewasihi kukumbuka wito muhimu walio nao wa kupeleka tunu njema ya maisha ya kiimani, kuishi kwa kumpendeza Mungu pamoja na wanadamu. Amesema ni muhimu kuwa mstari wa mbele kupeleka matumaini, ukweli, amani na haki. Pia, Askofu Mlola amewasihi waamini kuhakikisha uwepo wa kila mwanajumuiya wa Uru Seminari anakuwa ni chombo cha upendo na matumaini, kwa kutambua kwamba huo ni wito kwao waliolelewa na kufundishwa katika malezi na maadili mema walipokuwa Seminarini. Shirika la Mitume wa Yesu “Apostles of Jesus” AJ., lilianzishwa kunako mwaka 1968 na Padre John Marengoni huko Uganda. Nayo Uru Seminari iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi ilianza kusajiliwa rasmi kama shule kunako mwaka1972 kwa ajili ya malezi na majiundo ya Mapadre wa Shirika la Mitume wa Yesu. Shirika hili limeenea sehemu mbalimbali za dunia. Kazi yao ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya huduma za kichungaji, maisha ya kiroho na maendeleo endelevu ya kijamii.
Askofu Joseph Roman Mlola wa Kigoma akiongoza Ibada ya Misa Takatifu (©Society of Apostles of Jesus in Tanzania, AJ.)
Ni katika muktadha huu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Taasisi za Dini ambazo kwa namna ya pekee zimekuwa zikishiriki katika kutoa mchango kwenye sekta za Afya na Elimu nchini Tanzania. Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu Maalum ya Wanajumuiya wa Uru Seminari, iliyoadhimishwa kwenye Parokia ya Kristo Mchungaji Mwema, Tabata Kimanga Jimbo kuu la Dar es Salaam. Amesema kwa miaka mingi na kwa asilimia kubwa Taasisi za Dini zimechangia katika utoaji wa huduma za elimu na afya, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi hizo ili kufanikiwa zaidi katika kulijenga Taifa. Makamu wa Rais amesema Malezi yanayotolewa katika Taasisi za elimu za dini ikiwemo Shule ya Uru Seminari ambayo husisitiza Sala, Kazi na Masomo yanapaswa kutiliwa mkazo katika malezi ya vijana wa sasa. Amesema vijana watakavyoweza kumjua Mungu, kufanya kazi kwa bidii pamoja na kupata elimu wataweza kulijenga vema Taifa kupitia ujuzi na hivyo kuepusha tabia za kupata kipato kupitia njia zisizo sahihi. Makamu wa Rais amewashukuru, walimu, walezi na wanafunzi waliopata elimu Uru Seminari kwa ushirikiano na malezi mazuri ambayo yalifundisha kumtumikia Mungu pamoja na Wanadamu. Amewasihi Wanajumuiya ya Uru Seminari kuendeleza umoja na kuhakikisha unakuwa wenye tija kwa Taifa, pamoja na kuendelea kuiombea Tanzania na Viongozi wake.